loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mkataba mpya na tafsiri pana  unyanyasaji mahala pa kazi

Mkataba mpya na tafsiri pana unyanyasaji mahala pa kazi

“BAADHI ya watu wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu wanawake kubeba ujauzito kwamba akiwa na hali hiyo atashindwa kutekeleza na kusimamia majukumu yake aliyokabidhiwa. Hizi mimba tusipozibeba kizazi kitapatikana wapi? Haya ni maumbile yetu ambayo tumejaaliwa na Mwenyezi Mungu na kamwe sio kigezo hata kidogo cha kudharau uwezo wa mwanamke katika uongozi (au kufanya kazi).''

Maneno hayo aliyasema hivi karibuni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Zena Ahmed Said, wakati akizindua kitabu cha mwongozo wa ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na siasa kilichotayarishwa na asasi za kiraia ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar pamoja na Chama cha Wanasheria Wanawake (Zafela).

Mwakilishi wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Sada Mkuya, aliungana na Zena kukiri kwamba wakati mwingine wanawake wananyimwa fursa za kazi ama uongozi huku wakiwa na sifa kutokana na suala la hilo kubeba ujauzito.

“Nilipokuwa Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilisoma bajeti ya Serikali katika Bunge kwa muda wa zaidi ya saa mbili nikiwa nimesimama. Ni watu wachache sana waliofahamu kwamba nilikuwa na ujauzito wa miezi minane,” anasema Mkuya.

Viongozi hao wamezungumzia suala moja la ujauzito ambalo linaweza kusababisha unyanyasaji au ubaguzi mahala pa kazi. Je, huo ndio unanyasaji pekee unaoweza kutokea mahala pa kazi? Bila shaka si huo pekee. Kuna aina nyingi za unyanyasaji na ukatili kama vile rushwa ya ngono mahala pa kazi, mtu kunyimwa stahiki zake na haki zake, kuumizwa mwili au kisaikolojia, kubaguliwa kwa rangi, kabila au dini na kadhalika. 

Na je, mtu akifanyiwa unyanyasaji na ukatili nje ya maeneo ya kazi, kama vile anapokuwa safari ya kikazi au anapoelekea nyumbani baada ya muda wa kazi inakuwaje? Je, akiyanyaswa baada ya kustaafu sheria zetu zinasemaje? Na wale ambao wanatafuta kazi au wako kwenye mazoezi ya kazi (interns) wanapofanyiwa ukatili na unyanyasaji wanalindwaje na sheria?

Ni kutokana na masuala kama haya na mengine mengi ya aina hiyo, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limekuja na mkataba mpya wa kimataifa kuhusu Ukatili na Unyanyasaji Mahala pa Kazi.

Kifungu cha kwanza cha mkataba huo kinafafanua maana ya ‘ukatili na unyanyasaji’ mahala pa kazi kuwa ni tabia na mienendo isiyokubalika, au vitisho, iwe ni kwa tukio moja au la kujirudia, ambalo linalenga kusababisha, au kuweza kusababisha madhara ya mwili, kisaikolojia, kijinsia au kiuchumi.

Mkataba huo pia unafafanua maana ya unyanyasaji/ukatili wa kijinsia kuwa ni unyanyasaji au ukatili unaoelekezwa kwa mtu kutokana tu na jinsi yake, basi.

Hivi karibuni, Shirika la Actionaid, lilifanya semina kwa waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, iliyolenga kuwaelimisha kuhusu mkataba huo, ili nao watumie kalamu zao kuyajuza makundi mbalimbali kilichomo ndani ya mkataba huo na kuchukua hatua kadri itakavyoonekana inafaa.

Meneja Miradi ya Wanawake wa Shirika Actionaid, Amne Manangwa, anasema mkataba huo namba 190 uliopitishwa Juni mwaka 2019 umekuja kutoa ufafanuzi mpana kuhusu unyanyasaji mahala pa kazi, huku wanawake wakiwa waathirika wakubwa.

Anasema ni muhimu makundi mbalimbali yakauelewa mkataba huo, ili hatimaye sheria za sasa za kazi ziboreshwe kwa kuchota mambo muhimu kutoka kwenye mkataba huo, au kuja na sheria mpya kabisa itakayokomesha ukatili na unyanyasaji mahala pa kazi.

Je, sheria zetu za sasa za kazi zinakidhi kila kitu kama mkataba huo wa kimataifa unavyobainisha?

Akiwasilisha mada kuhusu mkataba huo, Wakili wa Kujitegemea, Anney Nahum, anasema kwamba sheria zilizopo ni nzuri, lakini kuna mapungufu kadhaa mintarafu masuala kadhaa yanayodadavuliwa katika mkataba huo.

Akizungumzia wigo wa mkataba, anatoa mfano kwamba sheria zetu zinajielekeza kwa mtu aliyeko kazini pekee lakini mkataba huo unakwenda mbali na kuwahusisha wanaotafuta au kutuma maombi ya kazi, wafanyakazi wa kujitolea, walioacha kazi, wastaafu na hata wenye mamlaka au walioko kwenye zamu za kazi.

“Mtu anaweza kunyanyaswa wakati anatafuta kazi… Anaweza kunyanyaswa akiwa ameshaacha au kuachishwa kazi na anaweza kunyanyaswa wakati amestaafu akifuatilia mafao yake. Mkataba huu unaangalia haya yote,” anasema mwanasheria huyo.

Anafafanua kwamba Sheria ya Tanzania namba 6 ya Uhusiano na Ajira Kazini ya mwaka 2004 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, hajielekezi katika makundi megine zaidi ya walioko kazini.

Anasema mkataba huo umetoa pia wigo mpana kwenye eneo ambalo ukatili na unyanyasaji unaweza kufayika, zaidi ya mahala anakofanya kazi mtu, yaani kwa maana ya kuhusisha jambo lolote linalohusiana na kazi hata kama ni nje ya kituo cha kazi. 

“Kwa mujibu wa mkataba huu, ukatili au unyanyasaji unaweza ukatokea katika safari ya kikazi, kupitia simu au mitandao ya kompyuta, pale mtu anapokuwa anatoka au kuelekea kazini, sehemu ya chakula, maliwatoni, sehemu ya kubadilishia mavazi, kwenye mafunzo, kwenye shughuli za kijamii au katika eneo la makazi yanayotolewa na mwajiri,” anasema.

Anasema kimsingi mkataba huo unatilia mkazo mambo matatu muhimu ambayo ni kuheshimu haki na utu wa mtu mwingine, kuimarisha na kuboresha usalama na haki za mwingine mahala pa kazi na unasisitiza utambuzi wa haki ya mtu mwingine.

Anasema mktaba huo pia unaendana na malengo yote ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa yanayohimiza usawa na haki za watu. 

Wakili Nahum anasema mkataba huo, baada ya kutoa mwelekeo kuhusu masuala ya kisheria, pia unapendekeza mifumo ya vyombo vya kisheria vya nchi mbalimbali na vya usuluhishi katika kutatua migogoro ya kikazi.

Hadi makala haya yanakwenda mitamboni ni nchi tano pekee duniani ambazo zilikuwa zimeshauridhia mkataba huo wa kimataifa ulionza mchakato wa kuuandaa mwaka 2015. Nchi hizo ni Argentina, Fiji, Namibia, Somalia na Uruguay.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/bd2f7b3c8b5f380eab7e6f0d1c2d37ed.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi