loader
Dstv Habarileo  Mobile
Ushujaa wa JPM ulivyochagiza Uchumi, ujasiri wa Afrika

Ushujaa wa JPM ulivyochagiza Uchumi, ujasiri wa Afrika

KIFO cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kimeendelea kuwaibua wachumi, wasomi na wanataaluma mbalimbali wanaomuelezea kuwa alikuwa jabali la uchumi aliyethubutu kudhihirisha kwa vitendo kuwa, yaliodhaniwa hayawezekani, yanawezekana.

Alichokifanya kwa miaka mitano na miezi kadhaa kimedhihirisha wazi safari yake ya kisiasa iliyojitokeza wazi mwaka 1995 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Jimbo la Chato, iliyokuwa wilayani Biharamulo.

Magufuli ametajwa na kada zote nchini nan je ya nchi kwamba alikuwa ni kiongozi jasiri, nembo ya mzalendo halisi wa Afrika, aliyewajibu kwa vitendo mabeberu kuwa nchi za Afrika ni tajiri na zinaweza kujiendesha bila utegemezi mkubwa kutoka nje.

Wanasema ni kiongozi shupavu aliyejenga ujasiri na imani kwa Watanzania na Waafrika kuwa Afrika inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa za kulisha dunia na kuwa mfadhili wa dunia badala ya kuwa tegemezi.

Kwa miaka hiyo mitano na miezi mitano, Rais Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya umeme wa moyo, alidhihirisha hayo na kuwa sehemu ya kiongozi wa kuigwa na wa mfano kwa nchi nyingi za Afrika na dunia kwa ujumla.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda anasema wachumi na Watanzania wanajifunza mambo mengi kutoka kwa Rais Magufuli kwani ni jabali la Afrika, jasiri aliyeonesha kwa vitendo kuwa mambo watu wanayodhani hayawezekani, yanawezekana tena kwa kipindi kifupi.

“Alikuwa ni mtu mwenye maono, mwenye jicho la tatu ambalo hata wasaidizi wake wasingeweza kuona matokeo yake. Aliposema kuhusu mradi wa Bwawa la Umeme la Nyerere (NHPP) na ujenzi wa treni ya umeme (SGR) ilionekana haiwezekani,” anasema Mwang’onda.

Mwang’onda anasema Magufuli alikuwa anajua kuna mapato makubwa yanatakiwa kutekeleza miradi hiyo na akawekeza kwenye kilimo na madini ikiwamo kubadili Sheria ya Madini Julai mwaka 2017 hatua iliyowezesha kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini na kuzuia utoroshwaji wa maliasili hiyo huku mauzo yakipanda mara dufu.

Anasema hatua ya elimu bure ilirejesha matumaini kwa Watanzania masikini kwa kuwa aliposema kwenye kampeni, wengi walidhani hilo halitekelezeki lakini akalifanya mpaka leo linaendelea.

Kuhusu afya, Mwang’onda anasema amejenga hospitali nyingi na vifaa vizuri vya kisasa katika hospitali hizo ikiwamo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo hivi sasa watu kutoka nchi nyingi duniani, wanatibiwa hapo.

Anasema anamtumaini kwamba Rais Samia Suluhu Hassan atavaa viatu hivyo licha ya kupoteza jabali la Afrika na kwamba matumaini kwa nchi zinazotuzunguka, kiunganishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika maendeleo, ujasiri.

“Watu wa Kenya, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameonekana wakimlilia sana, alikuwa analeta matumaini hata kwa nchi nyingine. Watu walipowahoji viongozi wao, walitoa mfano kwake, kwanini msiwe kama Magu fuli.

Wafanyabiashara wa kawaida amewajengea uthubutu, ametuachia ujasiri na imani kwamba vitu vinawezekana,” anasema. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Profesa Raphael Chigunda anasema amempoteza rafiki na mwalimu.

Anasema Magufuli alikipenda chuo chao na alikuwa ni kiongozi aliyetamani vyuo vikuu visiishie kutoa taaluma tu bali majibu kwa changamoto za wananchi.

Profesa Chigunda anasema Magufuli aliwatembelea chuoni hapo na kuwapa matrekta 10 na kama haitoshi katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/2019, walitengewa Sh bilioni 10 za kujenga jengo la maabara mtambuka ambalo sasa limefikia asilimia 90 kukamilika.

“Natoa mwito kwa wana taaluma wenzangu kuendeleza maono ya Magufuli kwamba vyuo vikuu visiwe tu vya kitaaluma bali viguse maisha ya watu wa kawaida kwa kufanya utafiti unaogusa maisha yao.

Hakika nimepoteza mwalimu na rafiki wa karibu,” anasema Profesa Chigunda. Aidha, Mwalimu wa Ushairi katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Shani Mchepange, anasema Rais Magufuli alikienzi Kiswahili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

“Kwa hakika mpendwa wetu Rais Magufuli amekienzi sana Kiswahili. Katika eneo la kisiasa, tutakumbuka aliwezesha kikao cha SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) kupitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo, EAC pia ni lugha rasmi inayotumika kuimarisha uchumi na kuleta utangamano na umoja zaidi,” anasema Profesa huyo

. Profesa Mchepange anasema katika eneo la kijamii na kiutamaduni, Magufuli alirejesha heshima ya taaluma ya Kiswahili na kufungua njia na kushauri juhudi zifanyike ili iwe lugha ya kufundishia katika elimu ya ngazi za juu kwani Magufuli amefungua njia, inapaswa isifungwe.

“Lugha hii ingekuwa ni binadamu, ingelia sana kwa kifo hiki lakini yote ni mapenzi ya Mungu hatuwezi kuyatengua, tumuombee kwa Mungu apumzike kwa amani,” anasema Profesa Mchepange.

Naye Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Eliaza Mkuna, alisema Rais Magufuli alikuwa na ujasiri na moyo wa kuthubutu ulio urithi mkubwa kwa Tanzania.

“Mara zote alisema Tanzania ni nchi tajiri na kila wakati alitumia mazungumzo yake kueleza hilo. Ni wazi kwamba nchi yetu ina rasilimali nyingi, lakini imekuwa ikikosa utawala bora.

Kwa hivyo, Dk Magufuli alitaka taifa lote kufaidika na rasilimali hizo,” anasema Dk Mkuna. Mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo ya jamii ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie, anasema Dk Magufuli alijipanga vizuri kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo ya nchi kupitia miradi mikubwa na imani yake yalioanzishwa yatakamilishwa na mrithi wake.

Baada ya kushika madaraka ya urais kwa mujibu wa, Rais Samia amekuwa akiahidi kutekeleza yale yalioachwa na mtangulizi wake huku akisisitiza kuwa, wakati huu si wa kunyosheana vidole, si wa chuki bali wa umoja, mshikamano na upendo ili kufikia malengo makubwa na ndoto za Rais Magufuli

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/5d8b73cc96c6466df4ae48491be92219.jpeg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi