loader
Dstv Habarileo  Mobile
‘Mafiga makubwa’ yanayomuanika Samia kiuongozi

‘Mafiga makubwa’ yanayomuanika Samia kiuongozi

SAMIA Suluhu Hassan, ameweka historia duniani kwa kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kuwa Rais. 

Ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuapishwa Machi 19, mwaka huu kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kilichotokea Machi 17, mwaka huu.

Kabla ya kuwa Rais wa Tanzania, Samia alikuwa na historia ya kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza mwanamke nchini Tanzania, baada ya kuteuliwa na Magufuli kuwa Mgombea Mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 na hata Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, rais wa nchi akifariki dunia, makamu wa rais ataapishwa kuwa rais na atashika wadhifa huo kwa muda uliobaki kufikia uchaguzi unaofuata. 

Kimsingi, nimechunguza na kubaini mambo na sifa nyingi zinazozidi kumstahilisha Samia kuwa kiongozi wa juu wa taifa hili, lakini hapa, nitazungumzia mambo machache tu miongoni mwa mengi, ninayoyaita ‘mafiga makubwa.’

Moja ya mafiga hayo makubwa, ni uwezo wake uliowafanya wajumbe 390 kati ya wajumbe 523 waliopiga kura katika Bunge la Katiba, kumchagua na kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.

Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka anatoa sababu za kumwona Samia Suluhu Hassan kama aliyefanya kazi kubwa kwa nafasi yake mintarafu namna alivyoendesha Bunge la Katiba la Mwaka 2014.

Profesa Sedoyeka anasema: “Kutokana na ajenda iliyokuwa mezani na wajumbe wengi kuwa wapya, Bunge la Katiba lilikuwa gumu sana kuliko mabunge mengine. Kiongozi legelege asingeweza kumudu kuendesha vikao katika bunge lile…”

Wajumbe wa Bunge la Katiba walikuwa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na wajumbe 201 walioorodheshwa kwa mujibu wa Kifungu Na. 22 (1c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayoonesha makundi mbalimbali 10 yanayohusika.

Ikumbukwe kuwa, Bunge la Katiba wakati huo lilikuwa na mchanganyiko wa wajumbe wenye itikadi mbalimbali hata wengine, wakiwemo hata walioweka kando maslahi ya nchi na kutanguliza maslahi binafsi na ya wafadhili wa vyama vyao walio hata nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Sedoyeka, uimara mwingine wa kiongozi huyu wa kitaifa ulianza kubainika siku za nyuma kuwa ni kiongozi mpole kwa sura na sauti, lakini mwenye uamuzi mgumu, makini, anayezingatia sheria, kanuni na taratibu kutokana na taarifa za kitaalamu.

Anathibitisha hilo akisema: “Hata uamuzi alioutoa hivi karibuni wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, ulitokana na taarifa ya uhakika ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)…”

Anasema: “Watanzania wana imani na uongozi wa Rais Samia kwa kuwa kwa asili, wanawake ni viongozi wazuri wanaosimamia haki na wajibu kwa kila mmoja, ni wasimamizi wazuri wa miradi, waadilifu, waaminifu, wanaojali na wafariji wanaotumia lugha nzuri kuelekeza.”

“Rais Samia ni makini, ana uwezo mkubwa wa kiuongozi kwa kuwa ni mcha Mungu, mwadilifu na anayeongozwa na sheria, kanuni na taratibu za nchi ndiyo maana kwa kuwa kwake hapo akiwa rais, nchi ipo katika mikono salama kabisa.” 

Hili linathibitisha zaidi uwezo mkubwa wa kiuongozi alio nao Samia Suluhu; Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba, alistahili na anastahili kabisa kuwa Rais. Mungu azidi kumtia nguvu na Watanzania wampe ushirikiano wa dhati.

Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba alifanya kazi kwa karibu na Mama Samia katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2020 wakati Samia akiwa Makamu wa Rais na January akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, anasema Samia ni miongoni mwa wanasiasa wenye uwezo mkubwa aliowahi kufanya kazi nao.

January ananukuliwa akisema: “Ni bahati mbaya tu kwamba wengi wa Watanzania, hawajapata fursa ya kuliona hilo.”

Anaongeza: “Mama Samia ana uwezo mkubwa wa kufanya aonekane ni mwanasiasa wa kawaida, lakini ukweli ni kwamba uwezo wake ni mkubwa sana na hili sijasimuliwa na mtu, bali nimeliona kwa kufanya naye kazi kwa karibu." 

Katika mazungumzo kwa nyakati tofauti, Mhariri wa Habari wa Gazeti la Sauti ya Mara lenye makao yake wilayani Tarime, Christopher Gamaina na mkazi wa Kijiji cha Sirorisimba wilayani Butiama katika Mkoa wa Mara, John Chacha Igotti, wanasema katika jamii, familia yenye mafanikio ina mchango mkubwa wa mwanamke.

Igotti anasema: “Kama ilivyo kwamba familia inayoongozwa na baba ikiwa na mafanikio, ujue kuna mchango mkubwa wa mama na familia inayoongozwa na mama ukiona imefanikiwa basi ujue pia kuna mchango mkubwa wa baba, ndivyo ilivyo kwamba nchi ikifanikiwa kwa jambo lolote, ujue kuna ushirikiano na mchango mkubwa wa makamu wa rais.”

Gamaina anasema: “Unaposema au kuona mafanikio yoyote ya Tanzania enzi za uongozi wa Rais John Magufuli, basi ujue kuna mchango mkubwa wa Makamu wa Rais (Samia Suluhu) kwa kuwa ndiye msaidizi wa karibu kabisa wa rais.”

Hili nalo, ni miongoni mwa mafiga mengi yanayothibitisha uwezo na umakini mkubwa wa Rais Samia. 

Inapaswa pia izingatiwe kwamba Magufuli alikuwa na haraka sana ya kuona matokeo na hivyo hakuwa mvumilivu abadani kwa mtu ambaye anaona hana uwezo wa kutimiza kile alichotarajia afanye. 

Kumchagua tena kuendelea naye katika kipindi cha pili cha uongozi wake ni ishara wazi kwamba, aliridhika sawia na uwezo wake wa kuongoza na kumsaidia.

Figa lingine miongoni mwa sifa nyingi zinazombeba na kuuonesha uwezo mkubwa wa Rais Samia, ni namna alivyomudu kupokea taarifa za kifo cha Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021, kuendesha msiba wa kitaifa na hata kupanga vizuri zaidi serikali tangu mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu wa wizara.

Abiria mmoja aliyekuwa akizungumza ndani ya daladala kutoka Buza kwenda Kawe Dar es Salaam alisikika akisema: “Huyu mama naye ni ushahidi kwamba kuwa mwanamke si sababu ya kushindwa uongozi.”

Akaongeza: “Mama Samia ameonesha uwezo mkubwa sana katika uongozi na ameonesha kuwa dhana kwamba mwanamke hawezi kuongoza, ni ya kizamani na haina mashiko.”

“Kitendo cha Mama Samia kuongoza nchi na kuapa kuwa Rais, kuongoza msiba hadi jana nchi ilipomaliza siku 21 za maombolezi na namna anavyoipanga serikali yake katika kipindi cha mpito, inaonesha kuwa Tanzania imepewa zawadi ya Rais wa Sita (Samia Suluhu) na wanawake wanaweza.”

Wadau mbalimbali wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia wanasema tangu akiwa makamu wa rais na hata baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu ameonesha wazi kuwa wanawake wanaweza kushiriki siasa na uongozi kwa mafanikio makubwa.

Hili linathibitisha juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi mbalimbali kuhamasisha wanawake kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi kwa ustawi wa jamii kwani, yapo mambo mengi ya kijamii ambayo mwanamke anayajua zaidi kuliko kiongozi mwanaume.

Mfano, ni adha ya ukosefu wa maji safi na salama na madhara ya kuwapo kwa huduma duni za afya maana aijuaye adhabu ya kaburi ni maiti.

Kwa mnsingi huo, taasisi zikiwamo za kimataifa kama UN- Women (Tanzania) inayofadhili mafunzo kwa wandishi wa habari kupitia Mradi wa Wanawake Wanaweza kutoa mafunzo hata kwa wanahabari kupitia Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na wadau wake, waendelee kuchochea ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika siasa na uongozi nchini.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8e2a1458c315992bb86404fa0bd7a961.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi