loader
Dstv Habarileo  Mobile
Makubwa aliyofanya hayati   Karume tunayemkumbuka leo

Makubwa aliyofanya hayati  Karume tunayemkumbuka leo

“HAYATI Abeid Amani Karume ameuawa tarehe 7 Aprili, 1972 na kuzikwa lakini kilichokufa na kuzikwa ni kiwiliwili chake tu, mawazo busara na mambo yake yote ya hekima yataendelea kutunzwa kwa faida ya kizazi kijacho.'' 

 

Hilo lilikuwa ni tamko lililotolewa na Baraza la Mapinduzi mara baada ya mazishi ya kiongozi huyo shujaa aliyefanya kazi kubwa kulikomboa taifa la Wazanzibari kutoka utawala wa wageni.

 

Watanzania na Wazanzibari kwa ujumla kila inapofika siku kama ya leo, Aprili 7 kila mwaka ni siku maalumu kwa mashujaa ikiwa ni sehemu ya kukumbuka mchango wa viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliofanya mambo makubwa kwa ajili ya kuikomboa Zanzibar akiwemo Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

 

Hayati Karume aliongoza Zanzibar kwa muda wa miaka tisa tu, lakini mambo makubwa aliyoyafanya yamebakia kuwa alama na kumbukumbu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

 

Mambo makubwa yanayofanya hayati Shehe Karume akumbukwe ni mengi ikiwa ni pamoja na kufanikisha Mapinduzi ambayo aliyatangaza kwa wananchi wa Zanzibar ikiwa ni ahadi za chama chake cha Afro Shirazi (ASP) kilichofanya kazi kubwa ya kufanya Mapinduzi hayo, Januari 12 mwaka 1964.

 

Siku hiyo ndiyo Wazanzibari walikuwa huru katika nchi yao baada ya kufanyika kwa Mapinduzi matukufu yaliyopindua utawala wa Sultani wa mwisho, Jemshid bin Abdalla hadi kulazimika kuikimbia Zanzibar na wananchi wazalendo kushika hatamu ya kuongoza dola.

 

Machi 8 mwaka 1964, Shehe Karume aliitisha mkutano wa kwanza wa hadhara mara baada ya Mapinduzi na kutangaza rasmi kwamba ardhi yote ni mali ya wananchi na kuitaifisha kutoka kwa kundi la mabeberu wachache, uamuzi ambao ulikwenda sambamba na kupiga marufuku vyama vya siasa vilivyokuwa vikiendeshwa kwa misingi ya kikabila na kuwagawa wananchi.

 

 

Novemba 11 mwaka 1965, Karume alianza kazi ya kugawa ardhi ikiwemo ekari tatu tatu kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba kwa shughuli za kilimo na makazi ambapo itakumbukwa wakati wa utawala wa Kisultani ardhi yote ilikuwa chini ya familia yake, ndugu na jamaa zake.

 

Kazi ya kugawa ekari tatu kwa kila mwananchi ilifanywa katika shamba lililokuwa likimilikiwa na ndugu wa familiya ya Sultani Huko Dole na hadi ilipofika mwaka 1973 tayari jumla ya eka 24,000 zilikuwa tayari imegawiwa kwa wananchi.

 

 

Hayati Karume aliwatangazia wananchi kuanza kazi ya utekelezaji wa ilani ya chama cha ASP kilicholeta ukombozi kwa kujenga nyumba bora za makazi kwa wananchi wa Unguja na Pemba pamoja na kujenga nyumba za wazee wasiojiweza huko Sebleni.

 

Ujenzi wa nyumba za maendeleo za mwanzo ulifanyika katika eneo la Kikwajuni Unguja tarehe 16 Januari 1966 kwa msaada mkubwa wa Serikali ya iliyokuwa Ujerumani Mashariki na kumalizika mwaka 1971.

 

Tarehe 1 Julai 1964 Karume alitangaza kutaifisha shule zote zilizokuwa zikitoa elimu kwa njia ya kibaguzi kuwa chini ya serikali.

 

Tarehe 23 Septemba 1964 iliku ni furaha kubwa kwa watoto wa Kiafrika masikini ambapo hayati Karume alitangaza elimu bure kwa wanafunzi wote wa Unguja na Pemba na kutaifisha shule zote zilizokuwa zikitoa elimu kwa njia ya kibaguzi.

 

Tarehe 26 Aprili 1964 taifa jipya la Jamhuri ya Muungano lilizaliwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hayati Julius Nyerere akawa Rais wa kwanza wa Muungano na Shehe Abeid Amani Karume akawa makamu wa kwanza wa Muungano huo.

 

Tarehe 23 Machi 1965 Karume alitangaza matibabu kwa wananchi wote kutolewa bure na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Hizo ni tarehe muhimu za kukumbukwa katika matukio muhimu yaliyofanyika mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964 ambayo yalifanywa na hayati Karume kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi za chama cha ASP ambacho ndiyo kilichoongoza mapinduzi hayo.

 

Baadhi ya wazee wanaoishi katika nyumba za maendeleo Sebleni ambazo zilijengwa na hayati Karume mara baada ya mapinduzi walisema hawatamsahau kiongozi huyo ambaye alikuwa na ari na moyo wa ushujaa wa kuwatumikia wananchi wake.

 

Mzee Haji Simai (83) anasema Karume alikuwa kiongozi mwenye maono, ubunifu na mapenzi ya wananchi wake bila ya kubagua kwa sababu alijikubalisha kwamba yeye ni kiongozi wa wananchi.

 

Kwa mfano anasema mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12 kwamba atajenga nyumba za kuwatunza wazee ambao wataishi kwa muda wa maisha yao yote chini ya uangalizi wa serikali.

 

“Mimi na wenzangu tunaishi katika nyumba hizi kwa zaidi ya miaka mitano sasa huku tukipata huduma zote ikiwemo chakula kwa maana ya mlo kwa siku mara tatu na fedha za kujikimu... Hayo ndiyo mambo aliyoyaagiza Karume wapatiwe wazee watakaoishi katika nyumba hizi,” anasema.

 

Khadija Jabir (82) ambaye alipata kuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja wa wanawake (UWT) na sasa ni kiongozi wa wazee wa Chama Cha Mapinduzi hapo Kisiwandui anasema hayati Karume ndiye aliyewakusanya na kuwataka kuanzisha umoja huo wa wanawake.

 

Anasema lengo lilikuwa ni kujenga umoja na sauti za wanawake ziweze kusikika kila kona.

 

“Karume alituambia kwamba chama cha ASP kinaanza kuingia katika harakati za kisiasa kwa ajili ya kudai uhuru wa Wazanzibari kutoka kwa Sultani kwa hivyo umoja na nguvu za wanawake zinahitajika kwa ajili ya kuunga mkono ikiwemo kuhudhuria mikutano ya kisiasa.

 

''Tuliunda umoja wa wanawake wa chama, mimi, bibi Mwanaidi Dai, Asha Simba Makwega huku tukishirikiana kwa karibu na bibi Fatuma Karume, yaani mjane wa hayati Karume kwa ajili ya kupata nguvu za sauti,'' anasema.

 

Mmoja ya waasisi wa harakati za kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake wa (ASP), Asha Simba Makwega anasema walijenga ushirikiano na uhusiano baina yao na wanawake wa Tanganyika waliokuwa katika chama cha TANU.

 

Anasema ushirikiano wao uliwakutanisha na wanaharakati wengine kama Hayati bibi Titi Mohamed na Lucy Lameck ambao waliwasaidia katika kujenga mikakati na hatimaye umoja wa wanawake wa ASP ukasimama kikamilifu.

 

''Tulifanikiwa kuunda umoja wa wanawake wa ASP kwa msaada mkubwa kwa wenzetu kutoka chama cha TANU wakiongozwa na bibi Titi Mohamed... Hapo harakati za kisiasa kwa wanawake kushiriki katika mchakato wa kampeni za kisiasa kwa ajili ya kudai uhuru zilianza rasmi katika miaka ya 1960,'' anasema Asha.

 

Maua Daftari, mbunge mstaafu na aliyekuwa Naibu Waziri wa Serikali ya Muungano kwa nyakati tofauti anasema yeye ni mmoja ya wanawake waliopelekwa nje ya nchi chini ya ASP kupitia Umoja wa wanawake (UWT) kwa ajili ya kuwa na Vijana watakaokuja kuongoza nchi baadaye.

 

''Nilipelekwa China kwa ajili ya masomo ya juu fani ya udaktari kupitia Umoja wa Wanawake wa ASP... Hizo zilikuwa juhudi binafsi za wazee wetu kuona baadaye tunakuwa na wasomi watakaoongoza nchi,'' anasema.

 

Aliyekuwa Waziri wa Elimu katika Serikali ya Karume, Ali Sultani, anasema alipewa kazi ya kuhakikisha sekta ya elimu inaimarishwa kwa watoto wa Kiafrika pamoja na kujenga shule nyingi katika kila kijiji ili kupunguza masafa ya watoto kutafuta elimu.

 

''Mzee Karume aliponiteua kuwa waziri wa elimu alinipa kazi ya kujenga shule za msingi na sekondari hadi katika visiwa vidogo vidogo ikiwemo Tumbatu. Aliniambia nataka kuona Wazanzibari wanafaidi matunda ya Mapinduzi kwani ndiyo sababu kufanya Mapinduzi hayo,” anasema.

 

Mberwa Hamad Mberwa (76), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba anasema hayati Karume mara baada ya Mapinduzi alifika Pemba na kuwaomba wananchi wa kisiwa hicho kuyaunga mkono na kuyatambua mapinduzi yaliyolenga katika kuleta umoja na mshikamano wa wananchi na kusogeza mbele maendeleo.

 

Mberwa anasema katika kipindi cha mwaka mmoja tu kazi za kujenga nyumba za maendeleo za ghorofa ulianza kwa mikoa mitatu ya Pemba, Mkoani, Chake Chake, Wete pamoja na vijiji vingine ikiwemo Micheweni na Kengeja.

 

“Hizo nyumba za ghorofa unazoziona Unguja basi na huku katika kisiwa cha Pemba zimejengwa kila maeneo... Karume alikuwa na siri moja ya kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja na kusahau tofauti zao za fikra za kutawaliwa na wageni,'' anasema Mberwa.

 

Huyo ndiye hayati Karume ambaye katika uongozi wake wa miaka tisa tu alifanya mambo makubwa na kubakia kuwa kumbukumbu kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi leo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/eae90dc160ae75bf93076ffce3d6ac4c.jpg

JUNI 16 kila mwaka nchi za Afrika wanachama ...

foto
Mwandishi: Suleiman Khatib

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi