loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia: Miradi ya kimkakati ikamilike kwa wakati

Samia: Miradi ya kimkakati ikamilike kwa wakati

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza watendaji wa serikali kuhakikisha urithi wa miradi mikubwa na ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake hayati Dk John Magufuli, inakamilika kwa wakati.

Aidha, ametaka watendaji wa sekta hiyo kuhakikisha nidhamu ya matumizi ya fedha na kupunguza gharama za miradi hiyo kwani kuna baadhi wanatengeza mianya ya kunufaika na riba kwa kulewesha malipo makusudi.

Akizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam baada ya kuwaaapisha makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na wakuu wa taasisi za serikali aliyowateua Machi 4, mwaka huu, Rais Samia alisema nchi imeachiwa urithi mkubwa wa miundombinu na Rais Magufuli na ni lazima iendelee na kukamilika.

“Tuna urithi mikononi mwetu ndugu zangu aliyotuachia marehemu Rais wetu. Ametuachia miradi mikubwa miwili na miradi ya kimkakati lazima iendelee, ule ni urithi wetu.

“Ukifanya vibaya na urithi Mungu anakulaani au aliyekuachia urithi hana radhi na wewe na Mungu hatokuwa na wewe. Naomba sana sana sana twende tukasimamie miradi hii ya kimkakati,” aliagiza Rais Samia.

Alisema kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo wakati mwingine kwa makusudi huku wakijua kuwa mikataba umeweka wazi ukichelewesha fedha ya malipo kuna riba jambo linalosababisha gharama za miradi kuwa kubwa.

“Ucheleweshaji wa malipo sijui unatoka wapi! Mimi nadhani ni mradi wa watu kuna maneno yanafanywa hapo juu. Mkandarasi hana haja na riba yako, anataka atekeleze mradi kwa wakati alete certificate (hati ya malipo) alipwe mambo yaendelee.

“Unapochelewesha malipo ili yatengeneze riba kwa serikali, sikuelewi na ni kuongeza gharama za miradi lakini pia ni ucheleweshaji wa kazi kwa mkandarasi,” alisema Rais Samia.

Alimuagiza Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba aliyewahi kufanya kazi katika wizara hiyo kabla ya kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, kuwa amemrejesha hapo kwa kuwa anapajua nje, ndani hivyo akasimamie vizuri fedha.

“Kasimamieni miradi iendelee lakini kuwe na displine (nidhamu) ya fedha. Fedha za maendeleo zitengwe na ziende kunakohusika kwa utaratibu. Kuna fedha zinaombwa za miradi haziji....kasimamieni hayo,” alisema Rais Samia alisisitiza lazima miradi hiyo itekekezwe na kukamilika kwa wakati.

 

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi