loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mosinyori Mbiku azikwa, amwagiwa sifa

MWILI wa aliyekuwa Mosinyori Paroko wa Parokia ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, Deogratias Mbiku umezikwa katika makaburi ya Kituo cha Hija Pugu jana na kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji.

Mwili huo kabla ya kuzikwa jana, kulikuwa na mkesha wa kumuombea na kuyakumbuka maisha yake uliofanyika usiku wa kuamkia jana katika Parokia ya Chuo Kikuu hicho alipofanya kazi kwa zaidi ya miaka 21.

Katika mahubiri yake kwenye misa ya kumuaga iliyofanyika Kanisa Katoliki-Pugu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Jude Thadeus Ruwa'ichi alisema utumishi wa padri huyo uligusa maisha ya watu wengi kiasi cha kila mmoja kuguswa na kifo chake.

Askofu Mkuu Ruwa'ichi alisema kwa miaka aliyofanya kazi ya upadri amegusa maisha ya watu wengi kuanzia watoto, vijana hadi wazee, wakristo na wasiokuwa wakristu.

“Kama mwanadamu anaweza kuwa na mapungufu yake kadhaa, tunaomba asamehewe na tuendelee kuyaenzi yale mazuri aliyoyafanya katika kutimiza majukumu yake,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Misa ya mkesha chuoni hapo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Gervas Nyaisonga ambaye alisema Monsinyori Mbiku alikuwa mtumishi wa Mungu aliyeiishi, kuitunza, kuipenda, kuienzi na kuipenda Biblia.

Rais huyo wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), alisema Biblia ilimpa nguvu ya kujiamini na kuifanya kazi ya Mungu vema zaidi ya kufanya kazi hasa ikizingatiwa kuwa biblia ilikuwa chemchemi iliyomwezesha kutenda mengi yanayokumbukwa leo na jamii.

“Jamii inapaswa kuiga mazuri kutoka kwa Mosinyori huyu kwa kuwa hata siye ambao tulibahatika kupitia mikononi mwaka tulijifunza mengi na kunufaika nayo. Hakika ametoa funzo kuwa katika maisha ya utumishi tusikubali chochote kuwa kikwazo cha kujitenga na Mungu tuendelee kumtumikia kwa kila hali na kujiweka tayari siku ya mwisho kwenda kwake,” alisema Rais wa TEC.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Padri Mbiku alikuwa padre wa Wakristo wote na si Wakatoliki peke yao.

“Msione mimi ambaye dhehebu langu ni Anglikana ninakuja kusali nanyi mara kwa mara, lakini sishiriki meza ya bwana mkadhania labda sikujiandaa, hapana nimejiandaa. Ila ni mtu ambaye nimekuwa napenda sana kuja kusikiliza mahubiri ya huyu Padri Mbiku tunayemzika leo,” alisema.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma wa UDSM, Profesa Boniventure Lutimwa alibainisha Padri Mbiku mbali na kufanya kazi ya Mungu, lakini pia alikuwa msaada mkubwa wa masuala ya kitaaluma chuoni hapo.

“Chuo Kikuu Dar es Salaam kimepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa kwa kwa kwa miaka yake mingi ametumikia katika chuo hicho cha Dar es Salaam,” alisema.

Wasifu wake unaonesha kuwa Mbiku alizaliwa Agosti 26, 1942 wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi ni mtoto wa tatu kati ya 13 wa Hukumu Liwala Mbiku na Mama Manate Sefu Nakilindo. Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari tatizo lililosababisha umauti wake Aprili 4, mwaka huu.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi