loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kigwangwalla matatani fedha Tamasha la Urithi

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2019/2020 imemtaja aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa alitumia madaraka yake vibaya kuzishinikiza taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kutoa fedha bila kufuata taratibu za matumizi ya fedha za serikali.

Bila kutaja ina la waziri huyo, lakini kwa kipindi hicho aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa Dk Hamisi Kigwangalla.

CAG alisema alibaini jumla ya Sh milioni 487.26 zilipelekwa kwenye taasisi saba kwa ajili ya utekelezaji wa Tamasha la Urithi.

Hata hivyo, hakukuwa na nyaraka zilizowasilishwa kwa ajili ya ukaguzi ili kuthibitisha matumizi hayo na alibaini matumizi ya Sh milioni 585.52 yaliyolipwa na Mhasibu wa Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii bila ya kuwa na nyaraka toshelezi.

“Nilibaini kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ililipa Sh milioni 140 kwa Kampuni ya Wasafi kwa ajili ya wasanii ambao wangetangaza utalii wa ndani katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Moshi, Iringa na Dodoma.

“Hata hivyo, hakukuwa na mkataba wowote uliosainiwa kati ya Kampuni ya Wasafi na Wizara ya Maliasili na Utalii. Hivyo, sikuweza kuhakiki wigo wa kazi pamoja na huduma zilizotolewa na Kampuni ya Wasafi.

“Pia, kulikuwa na maagizo ya Waziri wa Maliasili na Utalii (Dk Hamisi Kigwangalla) yakielekeza malipo kwa Kampuni ya Wasafi. Katika mahojiano na Waziri huyo, alikiri kuwa Kampuni ya Wasafi iliomba zabuni ya kutangaza tamasha hilo kwenye mikoa iliyotajwa na kutoa maagizo ya kufanya malipo hayo.

“Ni maoni yangu kuwa kiasi cha Sh milioni 140 kilicholipwa kwa kampuni ya Wasafi kufuatia maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii, hakiendani na Sheria za Matumizi ya Fedha za Umma.

“Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA) zilifadhili Tamasha la Upandaji wa Mlima Kilimanjaro bila ya kuwapo kwenye bajeti - Sh. 171,998,045.

“Mnamo tarehe 28 Septemba 2019, Waziri wa Maliasili na Utalii alizindua shindano lililoitwa Kigwangalla Kili Challenge la mwaka 2019 lililolenga kuhamasisha watu kupanda Mlima Kilimanjaro. Shindano hilo lilitumia jumla ya Sh milioni 172 zilizotolewa na NCAA (Sh milioni 114.5) na TANAPA (Sh milioni 57.5) bila kuwa katika bajeti zao za mwaka wa Fedha 2019/20.

“Pia, nilibaini kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kupitia kaimu katibu wake, alizielekeza NCAA na TANAPA kufadhili shindano hilo. NMT (Sh 115,020,000), Arusha (Sh 130,000,000), Dodoma (Sh 24,338,000), Dar es Salaam (Sh77,900,000), Mwanza (Sh 60,000,000), Arusha (Sh 30,000,000) na BASAZA (Sh 50,000,000).

“Fedha iliyotolewa na TANAPA ililipwa kwa Kampuni ya Utalii ya Ahsante Tours and Safaris Sh 57,498,045 kwa ajili ya gharama za malazi za wapandaji mlima.

“Nilibaini kuwa, Kaimu Katibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii alitoa maagizo kwa NCAA na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kulipia matumizi ya Ofisi ya Waziri Sh milioni 92.3 na Sh milioni 55.93 kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, mtawalia.

“Taasisi hizo hazikuwa na bajeti ya malipo hayo; na ukaguzi wangu ulibaini baadhi ya shughuli za taasisi zilizowekwa katika mipango yao hazikutekelezwa," alisema Kichere. 

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma jana na kisha kueleza kiundani katika mkutano na waandishi wa habari kwa takriban saa tatu, CAG alisema amebaini usimamizi usioridhisha wa fedha za Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii Sh bilioni 34.985.

Alisema alibaini Sh bilioni 6.875 zililipwa kutoka kwenye mfuko bila ya idhini ya Ofisa Masuhuli kinyume cha Kanuni za fedha.

Pamoja na hayo, CAG pia alibaini matumizi ya jumla ya Sh bilioni 16.363 bila ya kuwa na hati za malipo na matumizi mengine ya jumla ya Sh bilioni 11.157 ambayo hayakuwa na nyaraka toshelezi.

“Sh milioni 89 zilitumiwa na Makumbusho ya Taifa, matumizi yasiyoendana na shughuli za utalii. Pia, ukaguzi wangu ulibaini kuwa kiasi cha Sh milioni 500 kililipwa na Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) moja kwa moja kwa Bodi ya Utalii ya Taifa bila kupitia kwenye akaunti ya Tozo za Maendeleo ya Utalii.

“Hii ni kinyume cha Kanuni ya 9(1) na (2) ya Kanuni za Tozo za Maendeleo ya Utalii za Mwaka 2013. Pia, nilibaini kuwa hadi kipindi cha ukaguzi, Kamati ya Ushauri ya Mfuko haikuwa imeundwa, kinyume cha Kanuni Na. 9(3) na 9 (4) (a-g) ya Kanuni za Tozo za Maendeleo ya Utalii za Mwaka 2013.

“Mapungufu hayo yanaonyesha kuwa akaunti ya tozo hizo haikusimamiwa ipasavyo na Mkurugenzi wa Utalii na mhasibu ambapo walitoa fedha bila ya idhini ya Kamati ya Ushauri na Ofisa Masuuli wa Wizara kufahamishwa.

“Kwa maoni yangu, Mkurugenzi wa Utalii na Mhasibu waliokuwa wanahusika na usimamizi wa Mfuko wa Makusanyo ya Tozo za Maendeleo ya Utalii, walitumia vibaya fedha za tozo za utalii jumla ya Sh bilioni 34.98 kinyume cha Kanuni ya Tozo za Maendeleo ya Utalii za Mwaka 2013,” alisema.

CAG alisema ukaguzi wake kuhusu Tamasha la Urithi ili kukuza utalii na urithi wa kitaifa, alibaini kamati iliyoundwa iliidhinisha bajeti ya Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya utekelezaji wa hafla hiyo. Hata hivyo, alisema bajeti hiyo haikuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi na hakukuwa na mpango wa utekelezaji wa Tamasha la Urithi.

Kutokana na kukosekana kwa mpango wa utekelezaji ulioidhinishwa,CAG alibaini Wizara ya Maliasili na Utalii iliomba wakala wake wanne kuchangia jumla ya Sh bilioni moja ambazo hazikuwa kwenye bajeti zao ili kuwezesha kufanyika kwa tamasha hilo.

“Ili kuongezea bajeti hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii ilichangia Sh milioni 299 na Mfuko wa Tozo wa Maendeleo ya Utalii ulichangia Sh milioni 270.84; jumla ya Sh. bilioni 1.57 zilipatikana ili kufanikisha utekelezaji wa tamasha hilo ambapo fedha zote hizi hazikuwa kwenye bajeti za wizara na taasisi husika.

“Wakati wa utekelezaji, nilibaini kuwa Kituo cha Televisheni cha Clouds na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) walilipwa jumla ya Sh. milioni 629.7 na Sh. milioni 201.46, mtawalia, kwa ajili ya kuonyesha matangazo ya Tamasha la Urithi.

“Hata hivyo, hakukuwa na risiti za kielektroniki zilizotolewa kuthibitisha kupokelewa kwa malipo hayo. Aidha, kodi ya zuio ya Sh milioni 31.49 na Sh. milioni 10.07 kutoka Kituo cha Televisheni cha Clouds na TBC haikukatwa katika malipo yaliyofanyika.

“Vilevile, sikupewa ushahidi unaoonesha kuwa ununuzi wa huduma za matangazo kutoka TBC na Kituo cha Televisheni cha Clouds zilipatikana kwa njia ya ushindani na usawa,” alisema.

SERIKALI imezuia ndege zote zinazofanya safari za kwenda ...

foto
Mwandishi: Maulid Ahmed, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi