loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Trilioni 68/- zatumika Mpango wa Maendeleo

KATIKA miaka minne ya utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano 2016/17 – 2020/21, sekta ya umma imetumia Sh trilioni 34.9, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 45.

Aidha, sekta binafsi imetumia jumla ya shilingi trilioni 32.6 sawa na asilimia 85 ya lengo la miaka minne la shilingi trilioni 38.4.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa  wa mwaka 2021-2026.

Mwigulu alisema utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa taifa  ulikadiriwa kutumia jumla ya shilingi trilioni 107 ambapo shilingi trilioni 59 ni kutoka sekta ya umma na shilingi trilioni 48 kutoka sekta binafsi. 

Alisema, katika utekekezaji huo pato la taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.9; mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 4.1 kwa mwaka ikiwa ni ndani ya lengo la kutozidi asilimia 5

Mwigulu alisema akiba ya fedha za kigeni ilitosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.9 ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne huku nakisi ya bajeti ilikuwa ndani ya lengo la kutozidi asilimia 3 kwa kipindi chote. 

"Katika kipindi hicho, deni la serikali lilikuwa himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu."alisema.

Mwigulu alisema pia pato la wastani la kila mtu liliongezeka kutoka Sh 2,225,099 (sawa na dola za Marekani 1,022) mwaka 2016 hadi shilingi 2,577,967 (sawa na Dola za Marekani 1,080) mwaka 2019. 

"Kielelezo kikuu cha mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ni Tanzania kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha chini Julai mwaka 2020,”alisema.

Kuhusu ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, Mwigulu alisema utekelezaji wa mpango huo umefanikisha kujengwa kwa jumla ya viwanda vipya 8,477 kati ya mwaka 2015 – 2019 vikiwemo vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. 

"Ujenzi wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110 mwaka 2019."alisema Mwigulu na kuongeza;

"Viwanda hivyo vimechangia ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika soko la ndani na la nje ikijumuisha bidhaa za ngozi, nguo, ujenzi (nondo, mabati, saruji, misumari, marumaru na rangi), plastiki, zana za kilimo na vinywaji."

Mwigulu alisema uwekezaji huo ulileta mafanikio kwa kuongezeka kwa mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa kutoka asilimia 7.9 mwaka 2015 hadi asilimia 8.5 mwaka 2019; kukua kwa sekta ya uzalishaji viwandani kwa wastani wa asilimia 8.3; kuzalishwa kwa fursa za ajira kutoka ajira 254,786 mwaka 2015 hadi ajira 482,601 mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 47.2.

Alisema uwekezaji huo pia ulisadia kuchangia katika mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 13.8 mwaka 2016/17 hadi asilimia 14.2 mwaka 2019/20. 

"Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 45.3 kimetumika kuchochea miradi ya uzalishaji viwandani"alisema Mwigulu.

Alisema katika sekta ya kilimo ilijengwa miundombinu ya umwagiliaji iliyoongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 76,726 mwaka 2020; kukamilika kwa ujenzi wa maabara ya mbegu katika makao makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro; na kuanzishwa kwa soko la bidhaa. 

"Hatua hizi zimechangia  kuongezeka kwa utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 118 mwaka 2019/20; kupungua kwa mfumuko wa bei za chakula kufikia wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2020 kutoka asilimia 8.6 mwaka 2015; na kupungua kwa Umaskini wa Chakula kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia asilimia 8.0 mwaka 2017/18. Katika kipindi cha utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 188.9 kimetumika kuendeleza sekta ya kilimo;"alisema Mwigulu.

Kwa upande wa mifugo, alisema kulikuwa na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama nchini kutoka 25 mwaka 2015/16 hadi viwanda 32 mwaka 2019/20 na viwanda vya kusindika maziwa kutoka 82 mwaka 2015/16 hadi 99 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usambazaji wa mitamba katika mashamba ya serikali kutoka mitamba 11,449 mwaka 2015/16 hadi mitamba 18,255 mwaka 2019/20.

Mwigulu pia alisema, kulikuwa na ongezeko la maeneo ya malisho ya mifugo kutoka hekta milioni 1.4 mwaka 2015/16 hadi hekta milioni 2.85 mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na zao la ngozi kutoka shilingi bilioni 1.73 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 9.1 mwaka 2019/20.

"Katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huu kiasi cha shilingi bilioni 5.66 kimetumika kutekeleza miradi na programu za sekta ya mifugo”alisema Mwigulu.

Alisema kwa upande wa uvuvi mpango ulisaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili kutoka tani 362,645 mwaka 2015/16 hadi tani 497,567 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/16 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/20.

Mwigulu pia alisema kulikuwa na ongezeko la huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya Ulaya na kwamba mwaka 2019/20 jumla ya tani 777.750 za mabondo zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya nchi kutoka shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 506.24 mwaka 2019/20; na kuanza maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi. 

"Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, jumla ya shilingi bilioni 33.5 zimetumika kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi;"alisema.

Katika sekta ya madini Mwigulu alisema kulikuwa na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini kutoka Dola za Marekani bilioni 1.91 (sawa na shilingi trilioni 4.46 mwaka 2015/16 hadi Dola za Marekani bilioni 2.9 (sawa na shilingi trilioni 6.77) mwaka 2019/20; na kuongezeka kwa maduhuli kutoka shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 528.3 mwaka 2019/20.

"Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, jumla ya shilingi bilioni 83.4 zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya madini”alisema

Mwigulu alisema kwa maliasili na utalii, mpango uliongeza idadi ya watalii na mapato kupitia Mradi wa Kujenga Uwezo katika Hifadhi za Taifa; kudhibiti ujangili kwa asilimia 90; kubadilishwa na kupandishwa hadhi kwa mapori ya akiba,  na kuendelea kutangazwa kwa vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani. 

"Hatua hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii walioingia nchini kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 hadi 1,527,230 mwaka 2019; kuongezeka kwa wastani wa idadi ya siku zinazotumiwa na watalii kukaa nchini kufikia siku 13 mwaka 2019 kutoka siku 10 mwaka 2015.

Mwigulu alisema, mpango pia uliongeza mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 (sawa na shilingi bilioni 4,436.7) mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 2.6 (sawa na shilingi bilioni 6,071.3) mwaka 2019.

"Katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huu jumla ya shilingi bilioni 269.7 zimetumika kuboresha na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii”alisema.

SERIKALI imezuia ndege zote zinazofanya safari za kwenda ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi