loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mapungufu saba mashirika ya umma

RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali imebaini mapungufu zaidi ya saba katika baadhi ya mashirika ya umma ikiwemo kutengeneza hasara, udhaifu katika usimamizi na udhibiti wa mapato, ubadhirifu wa fedha, kuwa na wadaiwa sugu na mapungufu katika kusimamia masurufu.

Mashirika yaliyobainishwa kuwa na mapungufu zaidi ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Masoko la Kariakoo (KMC), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere wakati akitoa matokeo ya Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 jijini Dodoma jana.

Alieleza kuwa alibaini vitendo vya ubadhirifu katika Bandari ya Mwanza na Bandari ya Kigoma ambako katika Bandari ya Mwanza, Sh. bilioni 3.27 zilitolewa katika akaunti ya benki ya TPA iliyopo CRDB kupitia miamala 737. Vitabu vya fedha havikuonesha hati za malipo na pia matumizi ya fedha hizo hayakuoneshwa.

Alisema katika Bandari ya Kigoma, Sh. milioni 655.90 zilitolewa kutoka benki kwa kutumia hundi 30 bila kuwa na hati za malipo kuthibitisha malipo yaliyofanywa, na hundi hazikusajiliwa kwenye daftari la udhibiti wa hundi, na vipande vitano vya hundi havijaonekana katika daftari la udhibiti wala katika taarifa za benki. 

“Nyaraka kama vitabu vya hundi, hati za uhamishaji fedha na taarifa za bodi ya zabuni hazikutolewa kwa uchunguzi zaid,” alieleza na kuongeza kuwa katika Bandari ya Kigoma, alibaini ukosefu wa ripoti za mapato za kila siku ili kuhakiki ripoti za mapato ya kila mwezi kwa kipindi cha miezi saba. 

CAG alisema pia alibaini uwepo wa mashirika saba yaliyofanya vikao vingi vya bodi kwa mwaka wa fedha 2019/20, kinyume cha Waraka wa Msajili wa Hazina Namba 12 wa Mwaka 2015 unaotaka mashirika ya umma kufanya vikao vinne vya bodi kwa mwaka. Mashirika hayo yalifanya vikao 77.

Alitaja mashirika hayo kuwa ni Shirika la Wakala wa Meli Tanzania vikao 13, Benki ya Posta Tanzania vikao 11, Shirika ya Nyumba la Taifa (NHC) vikao 11, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) vikao 11, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania vikao 10, Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere vikao tisa na Chuo Kikuu cha Mzumbe vikao tisa.

Kwa upande wa ATCL, Kichere alisema alibaini kuwa hadi kufikia Juni 30, 2020, serikali ilikuwa imenunua ndege nane kwa gharama ya Sh trilioni 1.028 katika juhudi ya kuifufua kampuni hiyo.

Alisema ndege hizo zinamilikiwa na Wakala wa Ndege za Serikali na ATCL huzikodisha, lakini pamoja na kununua ndege kwa miaka mitano yaani kuanzia 2015/16 hadi 2019/20, serikali imeisaidia ATCL kiasi cha Sh bilioni 153.711 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na maendeleo.

Alisema kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza hasara kwa miaka mitano mfululizo na mwaka huu ilitengeneza hasara ya Sh bilioni 60.246. Kwa miaka mitano imetengeneza hasara ya Sh bilioni 153.542.

Alisema kwa upande wa Bodi ya Usanifu wa Majenzi na Upimaji (AQSRB), alibaini kuwa mwaka wa fedha wa 2019/20, ilitoza kiasi pungufu Sh milioni 21.02 katika kusajili miradi 14 yenye thamani ya Sh bilioni 143 kinyume cha tozo zilizoidhinishwa kwa ajili ya usajili wa miradi.

CAG alisema katika Chuo cha Taifa cha Sukari (NSI), chenye nyumba 123 za makazi zilizo katika muundo na ukubwa tofauti zilizoingiza mapato ya kodi ya pango ya Sh milioni 111.24 kwa mwaka 2019/20, alibaini kutokuwepo kwa mikataba ya upangishaji kati ya NSI na wapangaji 123.

“Na makusanyo ya mapato yalifanyika bila kutumia ankara za Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG), na hakukuwa na viwango vya kodi vilivyoainishwa kwa kila aina ya nyumba. Kitendo hiki kinatoa mianya ya upotevu wa mapato,” alieleza Kichere.

Alisema katika Shirika la Masoko la Kariakoo (KMC), alibaini usimamizi hafifu wa mapato ya ukodishaji wa pango; soko lilitakiwa kukusanya Sh milioni 597.54 kwa wapangaji 963 kulingana na taarifa za Kitengo cha Biashara kwa kiasi cha Sh 1,700 kwa mpangaji mmoja kwa siku moja. 

Hata hivyo, alisema zilikusanywa Sh milioni 285.22 na Sh milioni 312.32 hazikukusanywa. “Hii inaashiria kuwa Shirika la Masoko la Kariakoo linapoteza mapato kutokana na usimamizi hafifu wa wapangaji,”

Pamoja na hayo, Kichere alisema alibaini taasisi sita zilikusanya mapato yanayofikia Sh bilioni 7.12 nje ya mfumo wa GePG kinyume cha matakwa ya sheria, kitendo kilichotoa mianya ya upotevu wa mapato.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni NSI Sh milioni 111.24, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Sh milioni 731.73, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) Sh milioni 16.79, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Sh milioni 6,251.23, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Sh milioni 5.28 na Shirika la Posta Tanzania Sh milioni 114.51.

Alisema katika ukaguzi wake alibaini kuwa taasisi na mashirika ya umma yana kiasi kikubwa cha madai, ambapo kati ya mashirika 165 aliyoyakagua, mashirika 66 yana madai ya muda mrefu yanayofikia Sh trilioni 1.01 (sawa na 70%) ya madai yote.

Alisema kwa kiasi kikubwa madai hayo yanatokana na huduma zilizotolewa kwa wateja. “Pia, nilibaini kuwa asilimia 14 sawa na Sh. bilioni 203.96 ya madai hayo yameishapendekezwa kufutwa,” alisema.

Alisema kwa upande wa EPZA yenye lengo la kuvutia na kuchochea uwekezaji kwa ajili ya kuuza bidhaa za viwanda nje ya nchi lakini baada ya kukaguliwa alibaini kushuka kwa uwekezaji wa mitaji mipya katika

kanda maalumu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2015/16 mpaka mwaka 2019/20.

Alisema katika eneo la mwenendo wa uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), alibaini kushuka kwa idadi ya miradi inayosajiliwa na TIC katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/16 mpaka mwaka 2019/20.

Alitolea mfano idadi ya miradi iliyosajiliwa na kituo mwaka 2015/16 ilikuwa ni 420, wakati katika kipindi cha mwaka 2019/20 ilikuwa ni 219, hivyo idadi hiyo ya miradi katika miaka hii imepungua kwa asilimia 48.

Alisema ripoti hiyo pia ilibaini mashirika 29 yalikuwa na masurufu yafikiayo Sh bilioni 9.40 ambayo yalikuwa hayajarejeshwa mpaka mwishoni mwa mwaka yakiwa yamezidi siku 14 baada ya kukamilika kwa kazi. 

Kwa upande wa NSSF, alisema alibaini vyama 14 vilivyokopeshwa Sh bilioni 14 havifanyi marejesho ya mikopo hali inayosababisha hasara kwa NSSF na ukosefu wa fedha za kugharamia kazi zingine.

Alisema pia alibaini katika UDSM kilikuwa na deni la Sh bilioni 2.31 mpaka kufikia Juni 30, mwaka jana, ikiwa ni malimbikizo ya kiinua mgongo kwa watumishi wake ambao mikataba ya kazi ilikuwa imeisha kwa kipindi cha mwaka 2016 na miaka ya nyuma ya hapo. 

“Nilifahamu kuwa kiinua mgongo hulipwa na Serikali na Chuo kilionesha deni hilo katika vitabu vyake lakini hakikuonesha kama kinaidai serikali fedha hizo,” alisema.

Alitaja pia kampuni tanzu tano zilizopata hasara kutokana na kutofanya vizuri kibiashara ambazo ni Kampuni ya Mkulazi NSSF, Kituo cha Uwekezaji cha APC, Kampuni ya Uwekezaji ya NHC & PPF, Kampuni ya TTCL Pesa, Kampuni ya kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imeweza ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi