loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sokoine ataendelea kukumbukwa kwa mengi

“ NDUGU wananchi. Leo hii, ndugu yetu, kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tanzania, alipokuwa akirudi Dar es Salaam kutoka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki dunia.

Ndugu Watanzania, naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine,” ilikuwa ni sauti ya majonzi ya Rais Julius Kambarage Nyerere akitangaza moja ya msiba mkubwa uliyolikumba taifa.

Leo ni kumbukizi ya miaka 37 tangu kilipotokea kifo chake Aprili 12, 1984. Sokoine alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la kijiji cha Wami Luhindo (Wami – Dakawa) katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro, umbali wa kilometa 40 kabla ya kufika mjini Morogoro.

Alikuwa akitokea Dodoma baada ya kufunga kikao cha Bunge. Ili kuenzi mchango wa Hayati Sokoine katika kuleta maendeleo kwa Watanzania, katika Kijiji hicho pamejengwa Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine yenye kidato cha tano na sita.

Kwa nini anakumbukwa? Sokoine anakumbukwa sana kutokana na uongozi wake thabiti uliotukuka wa kutetea wanyonge na kulinda maslahi ya taifa. Anakumbukwa sana kwa namna alivyopambana na wahujumu uchumi waliotaka kulichezea Taifa kwa kuficha bidhaa muhimu na adimu ili waje wazilangue kwa kuuza kwa bei kubwa.

Ilikuwa ni wakati taifa linapita katika kipindi kigumu cha kujenga viwanda vyake vya ndani, kipindi ambacho Watanzania wakati mwingine walilazimika kujipangia huduma muhimu kama sukari, unga na sabuni.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alimpenda sana Sokoine kutokana na uadilifu wake, uchapakazi wake usio wa kawaida na ubunifu wake. Sokoine anakumbukwa kwa kuanzisha mapambano dhidi ya majangili na wavamizi wa misitu ambao walishughulikiwa kutokana na wao kushiriki kuunguza miti na misitu, kitendo kilichohatarisha taifa kuingia kwenye jangwa.

Alikuwa kiongozi wa mfano aliyekataa kujilimbikizia mali, bali alikubali kupunguza mali zake ili aweze kuwatumikia vyema Watanzania. Sokoine ataendelea kukumbukwa daima na Watanzania kutokana n uzalendo, ushujaa na nia ya dhati ya ujenzi wa Taifa na alikuwa kiongozi wa mfano ambaye daima alisimama upande wa wananchi hasa wanyonge.

Wananchi watamkumbuka namna alivyoasisi huduma ya usafiri wa magari ya abiria ya watu binafsi ili kusaudia usafiri hususani katika jiji la Dar es Salaam yaliyojulikana kwa jina la ‘chai maharage’. Iltokana na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kuelemewa katika kutimiza wajibu wake ambao ulilenga kuwasaidia uafiri watu wanyonge, wanafunzi na wafanyakazi.

Baadhi ya nukuu zake “Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na wananchi peke yake.

Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna sababu ya kuwapa imani kuwa tutawalinda kama vitendo vyao ni viovu” – Sokoine, 26 Machi 1983 “Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni kujilisha mwenyewe.

Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa” – Sokoine, 4 Oktoba 1983

“Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi miaka thelathini hadi arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae, ‘mali hii umeipata wapi?’” – Sokoine, 23 Oktoba 1983 “Juu ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa kupunguza uongezaji wa wataalamu katika Serikali na mashirika ya umma mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali nzuri” - Sokoine, 23 Oktoba 1982.

“Serikali inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka itasimamia bei ya mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine ni lazima vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha” Sokoine, 24 Septemba 1983.

“Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio wengi” - Edward Moringe Sokoine, 1Februari 1977 Kupambana kuanzishwa kwa SUA Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, anasema hayati Sokoine ambaye chuo anachokiongoza kinatumia jina lake katika kumuenzi, alikuwa ana hitoria kubwa na ya kutukuka nchini.

Anasema Sokoine alikuwa ni mpingania haki na maendeleo ya watu wanyonge na alitamani kuona wanyonge wa nchi wanapiga hatua kwa haraka.

Anasema kutokana na ushawishi wake mkubwa alioufanya bungeni akiwa Waziri Mkuu, wabunge walikubali kupitisha muswada wa uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro.

“Haikuwa jambo rahisi wabunge kupitisha muswada wa sheria wa kuanzishwa wa chuo hiki kikuu lakini kwa ushawishi wake wakakubali,” anasema Profesa Chibunda.

Profesa Chibunda anasema, baada ya kupitishwa na Bunge na kuanzishwa kwa chuo Kikuu hiki, ndipo bahati mbaya wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Dodoma akapata ajali ya gari na kufariki dunia.

Anasema SUA ilianzishwa Julai mosi mwaka 1984 na kuzinduliwa Septemba 25, mwaka huo na Mwalimu Juliaus Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania.

Kwa kutambua mchango wa hayati Sokoine katika chuo hiki, mamlaka za chuo zilifikia uamuzi wa kubadili jina la awali na kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Anasema baada ya kifo chake, mwaka 1991 Seneti ya Chuo Kikuu ilipitisha kuwa na mhadhara wa kuenzi juhudi hizi akiwa chimbuko la kuanzishwa kwa SUA.

Anasema Sokoine alikuwa mpenda mabadiliko katika nchi na alikuwa ni mwaminifu katika utumishi wake aliyependa usawa kwa kila mtu na aliamini kwamba kila mtu anaweza kuleta maendeleo kama akijituma katika kilimo sehemu alipo na hatimaye kujitegemea.

Historia yake Sokoine alizaliwa Agosti 1, mwaka 1938, katika kitongoji cha Kilasho, kijiji cha Emairete, Monduli Juu, mkoani Arusha. Alisoma Shule ya Msingi Monduli kuanzia mwaka 1949 hadi 1953 na kisha akajiunga na Monduli Middle School kutoka mwaka 1953 hadi 1956.

Baada ya hapo alijiunga na Shule ya Sekondari ya Umbwe alikosoma mwaka 1956 hadi 1958, ambapo safari yake ya kisiasa ilianzia pele alipojiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU), Januari 1, 1961 ikiwa ni miezi michache kabla ya Tanganyika haijapata uhuru.

Mnamo Oktoba 25, 1965, akiwa kijana mdogo wa miaka 27 lakini mwenye akili na ubunifu mkubwa, aligombea na kushinda ubunge wa jimbo la Monduli.

Mwaka 1967, Sokoine aliteuliwa na Mwalimu Julius Nyerere kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi. Mwaka 1970, Rais Nyerere, baada ya kuvutiwa na uchapakazi wake, alimteua Sokoine kuwa Waziri wa Nchi na mwaka 1972 akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Hadi taifa linaingia kwenye vita dhidi ya Nduli Idd Amini wa Uganda, Sokoine ndiye alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Baada ya CCM kuzaliwa kutokana na TANU na ASP kuungana Februari 5 mwaka 1977, Sokoine akawa mjumbe wa Kamati Kuu ya C CM.

Februari 13, mwaka 1977, kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka Rais Nyerere alimteua Sokoine kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Hata hivyo, Novemba 7, mwaka 1980, Sokoine alijiuzuru na kwenda masomoni nchini Yugoslavia (wakati huo) na nafasi yake ikachukuliwa na Cleopa David Msuya.

Baada ya kurejea, Rais Nyerere alimteua tena Sokoine kuwa Waziri Mkuu mnamo Februari 24, mwaka 1983. Sokoine ‘alivyoaga’ kablaya kifo Waziri mkuu Sokoine alihudhuria kikao cha Bunge Jijini Dodoma mwezi April 1984, lakini matendo yake kabla ya kifo chake yanaashiria huenda alihisi maisha yake duniani yalikuwa yakifikia tamati.

Inaelezwa kwamba Jumatatu ya Aprili 9, 1984, Sokoine alikwenda kusali kanisa la Mtakatifu Paul la Mjini Dodoma na usiku wa Aprili 10, 1984, aliandaa karamu ya chakula cha jioni kwa mawaziri na wakuu wa mikoa ambapo alionekana kuongea na kila waziri na kila mkuu wa mkoa mithili ya mtu anayeaga.

Jumatano, Aprili 11, 1984, aliandaa chakula cha jioni kwa wabunge wote wa mkoani kwake Arusha ambapo aliwasihi wafanye jitihada kuwaondoa wananchi wao kwenye lindi kubwa la ufukara.

Ndipo siku iliyofuata, Aprili 12, 1984, Waziri Mkuu Sokoine aliondoka na msafara wake Dodoma akiwa ndani ya Mercedes Benz ambapo msafara huo uliongozwa na gari la polisi.

Baada ya msafara huo kufika eneo la Wami Luhindo, gari la Sokoine liligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na Dumisan Dube, mpigania uhuru wa chama cha ANC aliyekuwa akiishi Mazimbu, mkoani Morogoro.

Siku hiyo ya Aprili 12, 1984 saa 11:30 wakati wa kipindi cha salamu cha Jioni Njema cha Redio Tanzania (RTD) kikiwa hewani matangazo yake yalikatishwa ghafla, wimbo wa taifa ukapigwa na kisha Rais Nyerere akatangaza kifo chake.

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi