loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa ataja 6 ya kumuenzi Magufuli

Majaliwa ataja 6 ya kumuenzi Magufuli

OFISI ya Waziri Mkuu imeainisha mambo sita watakayotekeleza katika mwaka wa fedha 2021/2022 kuenzi na kuendeleza jitihada, maono, juhudi za aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli pamoja na kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inakamilika.

Akisoma hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2021/22, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kati ya watakayomuenzi Dk Magufuli ni pamoja na ulinzi wa rasilimali za Taifa, nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuenzi lugha ya Kiswahili.

Mengine ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kuunganisha na kuwajali wananchi wanyonge na kudumisha umoja wa kitaifa huku wakitekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati ambayo inalenga kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na kuongeza fursa za ajira.

“Kwa kasi tuliyoanza nayo, serikali itaendelea kuongeza nguvu zake kuendeleza na hatimaye kukamilisha miradi hiyo,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa

pia wataimarisha huduma za jamii zikiwemo afya, elimu na maji pamoja na utekelezaji wa miradi inayoendelea na uanzishwaji wa miradi mipya.

Alisema katika mwaka huo wa fedha wataimarisha makusanyo ya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na mashine za POS na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuendeleza rasilimali fedha katika miradi ya kimkakati na kielelezo.

Alisema watashirikiana na washirika wa maendeleo katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii.

“Pia tutachukua hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu,” alisema Majaliwa na kuwaomba Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, dini na ukabila waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa ili kulinda mafanikio yaliyopo kwani jitihada hizo ndio zimewezesha kuingiza nchi kwenye uchumi wa kati.

Katika mwaka huo wa fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake imeomba

Bunge liidhinishe jumla ya Sh 116,784,244,000. Kati ya fedha hizo, Sh 93,303,370,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 23,480,874,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Bajeti hiyo ni pungufu ya bajeti ya mwaka unaoisha iliyokuwa Sh bilioni 312.80.

Pia Waziri Mkuu aliomba Bunge kuidhinisha Sh 128,873,377,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ambazo Sh 121,875,906,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 6,997,471,000 ni kwa ajili ya maendeleo.

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu walisema Juni 30, mwaka huu ni mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa

Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 2020/2021).

Alisema kuanzia Julai Mosi 2021, serikali itaanza kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Alisema mpango huo ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 yenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati na hali bora ya

maisha ifikapo mwaka 2025.

“Hata hivyo, hatuna budi kujipongeza kwa nchi yetu kufanikiwa kuingia katika kundi la nchi za uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda tuliojiwekea,” alisema na kubainisha kuwa kuingia katika uchumi wa kati ni kiashirio cha kuongezeka kwa uwezo wa Taifa kugharamia huduma muhimu kwa wananchi sambamba na uwezo wa wananchi kugharamia mahitaji yao.

“Natoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ili kulinda na kuendeleza mafanikio tuliyoyapata,” alisisitiza na kueleza kuwa katika mwaka 2021/2022 mwelekeo wa kazi za serikali utajikita katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/2022 ambao ni wa kwanza katika hatua za utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (2021/2022 – 2025/2026).

Alisema vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2021/2022 vimejikita katika masuala makuu matano ya Mpango wa Tatu. Masuala hayo ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi