loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tanzania na sayansi yake katika kudhibiti corona 

Tanzania na sayansi yake katika kudhibiti corona 

“MBINU walizotumia Tanzania katika kupambana na ugonjwa corona hasa unapozungumzia suala hili linalohusua pia kinga za mwili kuweza kupambana nalo, ndizo pia kwa namna fulani zimetumiwa na Sweden, Taiwan na Korea Kusini,” anasema Profesa Patriki Lumumba.

Mwanamajumui hiyo alikuwa akijibu hoja za Tundu Lissu katika mjadala uliorushwa na Sauti ya Amerika (VOA), hivi karibuni.

Katika mjadala huo, Profesa Lumumba alimuunga mkono aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa kitokuwa dodoki linalozoa kila takataka alimradi zinatolewa na mataifa tunayoamini kwamba yameendelea. 

Hakuna ubishi kwamba sayansi inayotumiwa na Tanzania katika kukabiliana na virusi hivi vya corona inaendelea kudhihirisha kwamba inafanya kazi kwa mafanikio kwa asilimia kubwa ikilinganishwa na sayansi inayopigiwa chapuo na mataifa ya Magharibi na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hatua ya kukabiliana na corona iliopendekezwa na Dk Magufuli na ambayo pia ilitangazwa hivi karibuni kuchukuliwa na Uingereza,  yaani kujifunza kuishia na corona, imewasaidia Watanzania kwa kiasi kikubwa kujikinga na kujitibu ugonjwa huopamoja na magonjwa mengine yanayoshambulia mapafu, bila hofu, na huku wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kwa kutambua umuhimu wa dawa za asili katika kupambana na virusi vinavyoshambulia mapafu, Dk Magufuli aliwahimiza Watanzania kuanza kutumia tiba asili kama vile kujifukiza kwa kutumia majani maalumu pamoja na ulaji wa malimao, tangawizi, vitunguu swaumu, machungwa na vyakukla vingine vinavyoimarisha kinga ya mwili.

Watanzania walimsikiliza aliyekuwa rais wao na kufuata sayansi hiyo ya kipekee ingawa ilipingwa na WHO. Baadaye wanasayansi wetu na taasisi zinazohusika na tiba na dawa za asili pamoja na utafiti wa dawa zikatoa dawa zilizotengenezwa kwa kutumia miti shamba na matunda.

Dawa hizo zilizotengenezwa na watafiti mbalimbali wakiwemo wa kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zinaendelea kupatikana katika maduka ya dawa za binadamu na ya tiba asili katika sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Muhimbili.

Mwezi Februari na Machi, kama ilivyokuwa mwaka jana, kulikuwa na habari za kuibuka tena kwa wimbi la ugonjwa wa corona nchini. Zipo habari za watu wakati huo kutoa taarifa za kuzika ndugu zao waliokufa kwa matatizo ya kushindwa kupumua, ingawa hatuwezi kusema wote walikuwa na corona kwani kila anayekufa huwa anashindwa kupumua!

Lakini, kabla ya kuandika makala haya, nimezungumza na watu zaidi ya 50 nikiuliza kama hivi karibuni kuna aliyezika ndugu mwenye tatizo linalofanana na corona, wote wamesema hakuna. Huu ni ushindi mwingine.

Mtoa Huduma wa dawa za asili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Upanga na Mloganzila, Tabibu Seth Korosso, mwezi Machi mwanzoni alikaririwa akisema kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya wananchi waliokuwa wanahitaji dawa hizo, baadhi zikiwa ni tiba-lishe ikiwa ni ishara tosha kuwa Watanzania walielewa umuhimu wa sayansi ya tiba asili. 

Alisema miongoni mwa dawa zinazosaidia mgonjwa mwenye corona ni pamoja na Rona Mixture ambayo ni dawa ya asili ambayo inapambana na tatizo la mfumo wa upumuaji, homa ya mapafu na inadhibiti virusi vinavyochangia dalili za tatizo la upumuaji.

Dawa nyingine ni Covidol ambayo inapambana na maambukizi yote yanayoingia katika mwili wakati kinga ya mwili ikiwa dhaifu kazi ambayo pia inafanywa na Rona Mixture. Pia inadhibiti hali ya mafua makali pamoja na homa kali.

Dawa ya NimriCaf iliyotengenezwa kwa kutumia tibalishe, mchanganyiko wake ukiwa ni malimao, tangawizi, pilipili kichaa, vitunguu saumu na vitunguu maji.

Kazi yake ni kuupa mwili uwezo wa kupambana na matatizo ya mfumo wa upumuaji na kuzuia damu kuganda kutokana na kuwepo kwa kitunguu saumu na kufanya mzunguko wa damu kuwa mzuri. Korosso alitaja aina nyingine ya dawa hizo kuwa ni pamoja na Udanol ambayo kazi yake kubwa ni kujifukiza kwa kuchanganywa kwenye maji ya moto.

Bila shaka dawa hizo ni imara, zimewasaidia na zinaendelea kuwasaidia Watanzania ingawa mataifa makubwa yanaendelea kubeza juhudi za Watanzania katika kutafuta dawa zao kwa ajili ya kupambana na corona.

 

Joseph Sabinus, mkazi wa Mwanagati, Ilala, ni miongoni mwa watu waliokuwa wakisambaza dawa ya Nimricaf. Jana alisema kwa sasa watu wanaoomba bidhaa hiyo wamepungua sana.

“Hii inaonesha kwamba tatizo limekwisha ama watanzania hawaliogopi tena,” anasema Sabinus.

Profesa Yunus Mgaya, Mkurugenzi  Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa (NIMR), anasema mataifa yenye nguvu yanabeza teknolojia na mbinu iliyotumiwa na Tanzania chini ya Dk Magufuli ya kutumia dawa na utaratibu wa asili kupambana na virusi vya corona kutokana na kutafuta soko la chanjo zao nchini Tanzania.

Profesa Mgaya anasema Tanzania imeona hakuna haja ya kuwapanikisha watu kwa kuwa kiuhalisia ugonjwa huo mpaka sasa umeua watu kwa asilimia 0.03 duniani. “Hii ina maana kuwa asilimia za watu kuishi waliopata virusi hivyo na wasiopata ni 99.97,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema Tanzania imechukua hatua sahihi kwa kuwa kwa sasa Tanzania ina wataalamu wa tiba asili zaidi ya 75,000 hivyo njia za kujifukiza, kutumia tangawizi na malimao zimefanyiwa utafiti na mwingine unaendelea ili kuwa na aina mbalimbali za dawa kwa ajili ya kuwatibu Watanzania.

Kwa mujibu wa Profesa Mgaya makampuni makubwa ulimwenguni yanayozalisha chanjo yana lengo la kutawala usambazaji wa chanjo hiyo na kuhakikisha kuwa kila mtu duniani pamoja na Watanzania wanapatiwa chanjo zao ili kujipatia mabilioni ya pesa.

Anasema hata chanjo ambazo zinapigiwa upatu na mataifa ya Magharibi pamoja na WHO hazina ubora wa kitaalamu kuweza kutumiwa na wanadamu kwa sababu ili chanjo ifikie hatua ya kutumiwa na wanadamu lazima ipitie katika hatua nne kuu.

Hatua ya kwanza baada ya chanjo kutengenezwa inapitia katika hatua ya majaribio ambapo inajaribiwa kwa wanyama kama panya, sokwe na sio binadamu. Baada ya majaribio kwenda vizuri chanjo inapitia hatua ya pili kwa kupata kibali cha kutangazwa katika majarida ya kisayansi.

Profesa Mgaya anasema hatua ya tatu ni ya kujaribisha kwa binadamu wachache kutoka katika mataifa mbalimbali duniani ambapo zoezi hilo huchukua miaka zaidi ya mitatu.

Anasema ikiwa chanjo itafanya vizuri, hatua ya nne ni kujaribiwa kwa watu wengi zoezi linaloweza kuchukua miaka minne na mambo yakiwa mazuri chanjo itasambazwa katika masoko kwa ajili ya biashara katika mataifa mbalimbali.

“Cha ajabu chanjo hii haikuvuka hata hatua ya pili ikapelekwa sokoni hali inayoleta hofu kubwa kwa watumiaji, ndio maana Tanzania tumeamua kuwa na utaratibu wetu wa kushughulikia corona tupige nyungu sana, tule tangawizi na malimao, tuko salama,” anasisitiza Profesa Mgaya.

Hoja ya Profesa Mgaya inaungwa mkono kivitendo na mataifa ya Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutoka barani Afrika kwa kukataa na kurudisha chanjo ya AstraZeneca baada ya kubaini kuwa zina madhara kwa wananchi wake.

Hata kwa baadhi ya mataifa ya Ulaya ambayo yalikuwa yakiishinikiza Tanzania kununua chanjo ya AstraZeneca au Modena hata yenyewe yamelazimika kusitisha matumizi ya chanjo hiyo baada ya kuona zinagandisha damu za wagonjwa.

Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uhispania ni mataifa ya hivi karibuni kabisa barani Ulaya kusitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca yakitanguliwa na Denmark, Norway, Ireland, Uholanzi, Iceland, Bulgaria, Ureno na Slovenia

Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi na Siasa nchini, Roy Sarungi anasema ikiwa Bara la Afrika halitakuwa makini linaweza kupata matatizo kutokana na kulazimishwa na mabeberu kutumia chanjo ya makampuni ya nchi zao.

Anasema tofauti na chanjo za mataifa ya Urusi na China zilizopitia katika hatua zote muhimu kabla ya kuanza kutumiwa na wanadamu, chanjo za mataifa ya Magharibi hazikupitia katika mstari sahihi wa majaribio.

Sarungi alishukuru Tanzania kuwa na bahati ya kuwa na Magufuli ambaye alikuwa imara katika kutopokea kikasuku kila kinachotoka Ulaya.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn alisema nchi yake haikukurupuka kuzuia chanjo hiyo bali ilitumia ushahidi uliotolewa na Taasisi ya Paul Ehrlich inayoshughulikia chanjo nchini humo.

“Taasisi yetu imependekeza kuzuia matumizi ya chanjo hiyo ili kufanya uchunguzi zaidi kwa watu saba waliopata mgando wa damu katika ubongo wao,” alisema Spahn.

Kwa upande wake Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema chanjo ya AstraZeneca imezuiwa mpaka hapo Taasisi ya chanjo ya Bara la Ulaya itakapotoa tamko kuhusu tatizo hilo.

Kampuni ya AstraZeneca ilikanusha taarifa kutoka katika nchi washirika mbalimbali kuwa chanjo yake haikupitia katika hatua zote muhimu kuweza kutumiwa na wanadamu.

Peter Drobac ni Mhadhiri kutoka katika Chuo Kikuu cha Oxford ambacho ni mshirika katika kutengeneza chanjo ya AstraZeneca anasema chanjo hiyo imepitia katika hatua muhimu zinazohitajika ili kuweza kutumiwa na mwanadamu.

Ni hatua nzuri ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda kamati ya wataalamu watakaoshauri juu ya mustakabali wa kukabiliana na corona nchini mwetu. Bila shaka timu hiyo, haitaegemea kwenye ushauri wa mataifa ya magharibi pekee bali pia yaliyochukua mbinu kama zetu kwa maana ya nchi kama Sweden, Korea Kusini na Taiwan. Itazingatia au kufanya utafiti wa namna tiba zetu zilivyosaidia na kama Watzania wamejenga kinga za kutosha dhidi ya virusi vya corona.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/972abaf91f978d274ae6c8502bc98158.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi