loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa: Wenye ujuzi watapewa kipaumbele zaidi

Majaliwa: Wenye ujuzi watapewa kipaumbele zaidi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itawapa kipaumbele vijana wenye ujuzi zaidi badala ya kuangalia viwango vya juu vya elimu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 17 katika uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa ya Uwekezaji katika Afya na Maendeleo kwa vijana.

"Hata jana tulizungumza hilo kwamba hatuwezi kuendelea kuangalia wenye shahada ya uzamivu badala yake tutaangalia ujuzi wa mtu kwa nafasi yake, lengo ni kuwapa nafasi vijana," amesema Majaliwa.

Akizungumza Bungeni juzi Waziri Mkuu alisema “Katika mwaka 2020/21 Serikali imechukua hatua za makusudi hususani utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, sambamba na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania, hadi kufikia Februari, 2021 ajira 594,998 zimezalishwa katika Sekta mbalimbali, kati ya hizo, ajira 314,057 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ajira za Serikali na ajira 280,941 zimezalishwa kupitia Sekta binafsi”

Alisema kupitia Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 18,956 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa, kati ya hao, Vijana 5,538 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi ambapo wanufaika 77 ni watu wenye ulemavu.

“Vijana 10,178 wamepewa mafunzo ya kurasimishiwa ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi wa mafunzo ambapo kati ya wanufaika hao 28 ni Watu wenye ulemavu, Vijana 3,240 wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu kazini (Internship) katika Taasisi binafsi na za umma ambapo kati yao wahitimu 92 ni Watu wenye ulemavu.” alisema

Alisema katika mwaka 2021/22, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala ya ukuzaji ajira na kazi za staha katika Sera, Mikakati na Mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahiki pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Aidha amebainisha kuwa vijana wataendelea kupewa nafasi ya kujiimarisha ikiwemo mikopo kwa ajili ya uanzishwaji wa biashara na shughuli mbalimbali.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi