loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia akemea uzandiki

Samia akemea uzandiki

Rais Samia Suluhu Hassan amekemea uzandiki kwenye mitandao ya kijamii.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana kwenye ukumbi wa Chimwaga Dodoma wakati wa kongamano la viongozi wa dini kwa ajili ya kuliombea taifa na kumshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Rais John Magufuli.

“Ukiingia kwenye mitandao ya kijamii kuna uzandiki mkubwa sana. Kila mtu anazua lake. Kila analofikiri kichwani kwake anaweka kule na kuwaaminisha watu wananchi mambo kadhaa, kadhaa, kadhaa”alisema Rais Samia.

Aliomba viongozi wa dini walipige vita jambo la uzandiki. “Sisi tutafanya lakini mkifanya ninyi Mungu anayasukuma kwa haraka zaidi”alisema na kuwaomba pia wakemee yote yanayokiuka maadili na tamaduni za Mtanzania.

“Nawasihi pia viongozi wa dini endeleeni kuhimiza waumini wenu kuchapa kazi kwa bidii na kulipa kodi stahiki na kwa wakati. Nawaomba sana viongozi wetu wa dini muendelee kuwahimiza Watanzania kuwa pamoja na kujenga mshikamano, tusibaguane kwa namna yoyote”alisema

Aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na kusema utamaduni wa kuwasiliana kati ya serikali na viongozi wa dini utaendelea.

“… Viongozi, natambua mchango mkubwa wa Hayati Magufuli kwa jinsi alivyowathamini na mimi pamoja na Dk Mwinyi tutaendeleza utamaduni huo,” alisema Rais Samia

Katika kongamano hilo, Rais Samia alieleza kusikitishwa na kitendo cha wabunge kumlinganisha yenye na Rais Magufuli badala ya kujadili agenda za kitaifa.

Alisema yeye na Rais Magufuli ni kitu kimoja na akasema mijadala inayoendelea bungeni haina manufaa kwa taifa.

"Inasikitisha kuona wanapiga ngoma mitandaoni na kuchezwa bungeni kwa kudemka vizuri. Kulinganisha watu wala si kulinganisha agenda za kitaifa" alisema Rais Samia na kuongeza;

"Naomba sana, wabunge, tunatakiwa kupitisha bajeti za sekta, bajeti ya serikali kwa maendeleo ya taifa, mjikite sana katika jambo hilo, mengine tutazungumza," alisema.

Kuhusu ugonjwa wa Covid_19, Rais Samia alisema tayari ameunda kamati ya kumshauri kuhusu hatua za kuchukua kukabili janga hilo linalosababishwa na virusi vya corona.

"Niwape taarifa kwamba kamati nilishaunda na hivi karibuni nitakaa nao kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha" alisema.

Rais Samia aliwaomba viongozi wa dini wawahimize waumini wao wazingatie tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya kuhusu kujikinga. 

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi