loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali yaipa Sido bil 4.29/- kuendeleza wajasiriamali

SERIKALI imetoa Sh bilioni 4.29 kwa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wajasiriamali zikiwemo za maendeleo ya teknolojia na ujenzi wa majengo ya viwanda kwa wajasiriamali wadogo.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Vunjo, Charles Kimei (CCM), aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani kupitia Sido kutengeneza mashine za gharama nafuu zitakazosaidia kuchakata mazao ya wakulima.

Mashine hizo ni pamoja na za kutengeneza ‘chips’ za ndizi, muhogo, sosi za nyama, karoti, pilipili hoho na mbogamboga.

Akijibu swali hilo, Kigahe alisema fedha hizo zimetolewa katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 na kuwa serikali imeweka mkakati wa  kuendeleza viwanda hususan vidogo sana na vinavyolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na hivyo, kuendelea kuijengea uwezo Sido ili kubuni na kuendeleza teknolojia mbalimbali kutokana na mahitaji.

Alisema Sido ina vituo vya uendelezaji teknolojia katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Lindi, Iringa, Mbeya na Shinyanga kwa ajili ya kutengeneza mashine za kuchakata na kusindika mazao ya kilimo.

“Mashine hizo ni pamoja na za kutengeneza chips za ndizi, viazi na muhogo, kukausha mbogamboga na matunda, kusindika nyanya, karoti na pilipili kwa ajili ya achali kulingana na mahitaji; vile vile aina ya mashine zinazotengenezwa zinapatikana katika tovuti ya Sido na husambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia ofisi za Sido,” alisema.

Alisema licha ya kutengeneza mashine hizo, Sido pia imekuwa ikitoa mafunzo ya usindikaji wa muhogo, ndizi, nyama, karoti, pilipili na mbogamboga katika mikoa yote ya Tanzania Bara na gharama za mashine hizo hutegemea uwezo wa mashine.

 “Vilevile, Sido inasimika mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kutengeneza mashine kwa wingi na kusambaza kwa wananchi kwa gharama nafuu katika vituo vya kuendeleza teknolojia katika mikoa ya Kigoma, Lindi na Shinyanga,” alisema.

Alitoa mwito kwa wananchi wanaohitaji mashine za kuchakata na kusindika mazao, kuwasilisha mahitaji yao katika ofisi za Sido zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amesema serikali imeweza ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi