loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Soka ya Ulaya zogo tupu

KUMEKUWA na zogo kwenye soka la Ulaya tangu kutangazwa kwa European Super League inayohusisha miamba 12 ya Ulaya.

Klabu hizo zikiongozwa na Real Madrid chini ya Rais wake, Florentino Perez ni AC Milan, Arsenal, Atletico Madrid, Chelsea, Barcelona, Internazionale, Juventus, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur. 

Kwa mujibu wa umoja huo, michuano hiyo yenye fedha nyingi itakuwa ikichezwa katikati ya wiki.

Tangu kutangazwa kwa taarifa hizo ambazo uundwaji wake ulifanyika kwa siri kubwa, kumekuwa na sintofahamu, huku mashabiki wengi wa soka wakipinga suala hilo.

Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin amezitupia lawama klabu hizo, akidai kitendo hicho ni kama kuwatemea mate usoni mashabiki wa soka na kukiita cha kuanzisha michuano pinzani kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya na si cha kiungwana.

Ceferin ambaye amefanya marekebisho kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka timu 32 mpaka 36 kuanzia msimu wa mwaka 2024/25, amezungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu Uropean Super League (ESL) ilipotangaza michuano hiyo juzi.

Kuanzishwa kwa michuano hiyo kumelaumiwa na mashabiki wa soka, vyama vya soka na viongozi wa timu za taifa, kwani inaonekana ni kupingana na Uefa na Fifa ambazo zinaendesha michuano mikubwa. 

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kupitia mtandao wa zoom nchini Uswisi, Ceferin alimshutumu Mwenyekiti wa Juventus, Andrea Agnelli na Makamu Mwenyekiti wa Manchester United, Ed Woodward kuwa wamesaidia kuundwa ESL na kujiuzulu nyadhifa zao kwenye umoja wa klabu za Ulaya, taasisi iliyoziunganisha klabu 246.

"Siwezi kujihuzunisha zaidi kwa tukio hili kwamba Uefa na dunia ya soka zisiwe pamoja, kitendo cha kuchagua klabu chache Ulaya si sawa,” alisema Ceferin na kuongeza:

"Wazo hili ni kama kuwatemea mate usoni wapenzi wa soka na jamii kwa ujumla, hatupaswi kuwaachia waichukue (soka) kutoka kwetu, nimeona mambo mengi kwenye maisha yangu, nilikuwa wakili kwa miaka 24, nimeona watu wengi lakini sikuona aliyesimama na hili.”

"Kama nitaanza na Ed Woodward, alinipigia simu Alhamisi iliyopita akinieleza jambo hili na kwamba ametoa sapoti yake, lazima alikuwa tayari ameshasaini kitu. Nimekatishwa tamaa sana, sitaki kuwa mbinafsi sana, lakini sijaona mtu kama yeye ambaye anadanganya mara nyingi, nilizungumza nae Jumamosi na akaniambia hizo ni tetesi tu hakuna kitu kama hicho kisha akazima simu yake, ni vizuri kwenye maisha kufahamu nani ni nani.”

Ceferin alionya kuwa, wachezaji watakaocheza timu zitakazoshiriki ligi hiyo watafungiwa kucheza Kombe la Dunia na michuano ya Euro na hawataruhusiwa kuziwakilisha timu zao za taifa kwenye mechi yoyote.

"Hatukujua kama tulikuwa na nyoka wanaofanya kazi na sisi kwa karibu, lakini sasa tumejua. Super League ni kufuata fedha tu, sitaki kuwaita kwamba wana fedha chafu, lakini Uefa ni kuhusu kuendeleza soka na kuhusu fedha kwa kile kinachostahili kulipwa, hiyo ndio soka yetu, utamaduni wetu na baadhi ya watu hawaelewi hili.”

"Tuna Shirikisho la Soka England (FA), Hispania, Italia, Ligi Kuu, La Liga, Serie A na FIFA, sisi wote tunaungana kupinga mpango huo wa kipuuzi,” alisema.

Katika kujibu hoja hizo, Rais wa Real Madrid,  Perez ambaye ndio kinara wa mpango huo, ametamba kuwa Uefa haiwezi kuziondoa timu zao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Alisema ana hakika Real Madrid na washirika wake wa Super League hawawezi kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na kutuhumu mtindo wa sasa wa kuendesha michuano hiyo akisema unavutia tu kuanzia kwenye robo fainali na klabu zote zitakufa kama hautabadilishwa mfumo wa michuano hiyo.

"Tunacheza dhidi ya timu ndogo ambazo hazivutii, watu wadogo wanafaa kujiburudisha wenyewe na vitu vingine, lakini kama tutafanya hivi msimu mzima, mechi tano Jumanne, tano Jumatano, haitasimama.”

"Kitu gani kinapatikana kwa klabu 15 kucheza kila wiki, itakuwa shoo kubwa duniani. Real Madrid, Manchester United au Barcelona, Milan inavutia zaidi kuliko Manchester United dhidi ya klabu ndogo,” alisema na kuongeza:

"Dunia inataka nini? Tuna mashabiki Singapore, China, duniani kote unaona hilo kwenye mitandao ya kijamii, wafuasi walio nao, hayo yanaleta fedha.”

Perez alisema klabu tatu zaidi zinatarajiwa kuungana nao huku nyingine tano zitafuzu kutokana na viwango vyao. 

Perez anakuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Super League huku Andrea Agnelli wa Juventus na Joel Glazer wa Manchester United wakitajwa kuwa makamu wenyeviti. 

Madrid inatarajiwa kucheza na Chelsea kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza Jumanne Aprili 27 kabla ya kurejeana Jumatano ya Mei 5. 

"Hawawezi kuiondoa Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa hakika, Si Madrid wala Manchester City au yeyote, nina hakika,” alisema Perez.

Jesper Moller, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Uefa kutoka Denmark alisema anatarajia Madrid, Chelsea na Manchester City zitaondolewa kwenye michuano ya Uefa. 

Hata hivyo, klabu za Bundesliga, Borussia Dortmund na Bayern Munich zimeamua kuendelea na Ligi ya Mabingwa na hazitashiriki kwenye michuano hiyo mipya. 

Mtendaji Mkuu wa Dortmund, Hans-Joachim Watzke alisema klabu hizo zipo kwenye Ligi ya Mabingwa. 

RB Leipzig imeungana na Bayern na Dortmund na Mtendaji Mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge. "FC Bayern haijihusishi na mpango huo wa kuunda Super League. Tuna amini kwamba utaratibu wa sasa wa soka uko vizuri. FC Bayern ilikubali muundo mpya wa Ligi ya Mabingwa kwa sababu tunaamini wako sahihi kwenye kuleta maendeleo ya soka Ulaya. Siamini kama Super League itatatua changamoto za fedha kwenye klabu za Ulaya.”

Mapema juzi, Watzke alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema kwamba Dortmund na Bayern hazipo kwenye umoja huo mpya. 

Kwenye mkutano na waandishi wa habari juzi, kocha wa Bayern Hansi Flick alisema haiungi mkono ligi mpya. 

"Naungana na taarifa ya klabu yangu na Dortmund, sipo tayari kwa michuano hiyo,” alisema. 

Leipzig ambayo ni ya pili kwenye Bundesliga, imesema haivutiwi na mpango huo wa ligi mpya. "Tunakataa mpango wowote wa kuitangaza Super League," imesema klabu hiyo.

Dortmund na Bayern zilikuwa miongoni mwa klabu tatu kwenye tetesi kwamba ziko njiani kuungana na klabu 12 kwenye Super League, ambayo huenda ikaanza msimu wa mwaka 2023/24.

MANCHESTER United leo itaikaribisha Liverpool katika ...

foto
Mwandishi: LONDON, England

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi