loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali: Mpo salama

Serikali: Mpo salama

Na Ikunda Erick WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wachape kazi na kwamba serikali ipo imara na inawahakikishia usalama.

Alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo makini na akawataka watumie muda mwingi kujadili mambo ya maendeleo.

Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar e Salaam alipokagua ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota uliofikia asilimia 94. Mradi huo una majengo matano, manne kati ya hayo kila moja likiwa na ghorofa nane na moja tisa.

“Niko hapa kukagua miradi mikubwa ya maendeleo tunayoitekeleza, Rais Samia Suluhu amenituma, na anawasalimu, serikali chini ya uongozi wake iko makini na ametuasa tuchape kazi, tushikamane, ninawaomba tumieni muda mwingi kujadili maendeleo na sio mijadala ya ovyo, sisi tunawahakikishia usalama,”alisema Majaliwa.

Alisema mijadala ya maendeleo ipewe fursa ya kujadiliwa kwa sababu ina tija kwa ustawi wa taifa na kusema serikali itaendelea kusimamia usalama na amani.

“Niwahakikishieni serikali iko makini na inaendelea kusimamia na kuhakikisha usalama upo ili watu wawe huru kufanya kazi za maendeleo kwani tangu awamu ya kwanza hadi sasa jambo muhimu linalowaunganisha Watanzania ni utulivu na usalama wa nchi”alisema Majaliwa.

Alisema ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo uliofikia asilimia 94, na kwamba serikali ilipeleka fedha Februari mwaka huu kwa ajili ya kuukalimisha na kiasi kingine kitatolewa ili asilimia sita zilizobaki zikamilike.

Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 50.58 na jumla ya kaya 644 zilizokuwa zinaishi hapo awali ndizo zitasaini mkataba kuishi eneo hilo baada ya ujenzi kukamilika na kuna nyongeza ya nyumba nyingine za kukaa kaya 12.

Majaliwa aliitaka Wakala ya Majengo Tanzania (TBA) ambao ndio wa wajenzi wa mradi huo wahakikishe asilimia nne zilizobaki zinakamilika na pia wawaandae wahusika kuhamia kwenye makazi hayo.

Aliiagiza TBA iwaandae viongozi wa kaya hizo kwa kuwapa ushauri na maekelezo ya namna ya kutumia maeneo hayo na kuyatunza ili kuhakikisha mandhari nzuri iliyopo inadumu.

Majaliwa alimuagiza Meya wa Kinondoni ashughulikie matengenezo ya barabara za jirani na eneo hilo ili ziwekwe lami na kupendezesha mandhari ya eneo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Daudi Kondoro alisema mradi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli aliyeagiza makazi hayo yaboreshwe.

Alisema mradi huo umejengwa kwa kuzingatia mambo muhimu na kwamba eneo lililotumika la mradi ni asilimia 25 tu na lililobaki litatumika kujenga miradi ya maduka na vitega uchumi.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi