loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Trafiki wakiri wenzao kugeuza daladala vicoba

BAADA ya HabariLeo kuandika kuhusu baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Dar es Salaam kugeuza daladala mtaji wa kupokea rushwa ya kati ya Sh 2,000 hadi 5,000, baadhi ya askari hao wamekiri kuwa tuhuma hizo ni za kweli.

Aidha, askari hao wamesema habari hiyo iliyoandikwa jana katika gazeti hili ikihusisha rushwa hiyo iliyopewa jina la ‘vicoba vya trafiki’, imewachafua askari wote wa usalama barabarani na sasa wanajichunguza.

Askari wengine walieleza kushtushwa kwa namna walivyogundulika ‘kuchomewa’ kupokea rushwa hiyo, wakisema wanapokea kiasi hicho kuwasaidia makondakta kupata hesabu za mabosi kuliko kuwaandikia faini ya Sh 30,000.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na HabariLeo jana, askari hao walisema ni kweli baadhi yao wanapokea rushwa na kukichafua kikosi hicho na kuwataka kujirekebisha.

Baadhi ya askari pamoja na kugundulika, walisema watatafuta njia mbadala za kupokea rushwa ili wasigundulike. “Watu wanatuwinda kweli kweli acha tu yaani ndugu yangu.

Ingawa ni kweli wapo wanaochukua rushwa hiyo na hao ndio wanaotuharibia sana na kutudhalilisha, ila kwa kweli hali hii inatisha sana.” alisema na kuongeza; “Unajua hili jambo lina ukweli, unajua mpaka gazeti liandike, limechunguza kwa kina na muda mrefu, hawawezi kuandika vitu vya uongo.

Kwa hiyo inawezekana kabisa wapo wenzetu wanaopokea vijihela hivyo,” alisema askari anayesimama Kimara Bucha, barabara ya Morogoro ambaye jina lake tunalihifadhi.

Askari wengine walidai wanapokea rushwa kutokana na kuwaonea huruma madereva na makondakta kwa kuwa wakiwaandikia kila siku kosa moja linaloanzia Sh 30,000 hawatapata hesabu ya mabosi na wala posho zao, hivyo wanachukua Sh 2,000 hadi 5,000 kuwasaidia.

Katika hatua nyingine, wasimamizi wa askari wa usalama barabarani katika vituo vya barabarani jana walifanya vikao na askari wanaowasimamia na kuwapa tahadhari juu ya suala hilo.

“Vijana wangu nimewaambia wasithubutu kuchukua wala kuomba rushwa, baada ya hii habari tumezungumza na nimewaambia uchunguzi umeanza, ila aisee gazeti lenu limetuchafua sana, askari wote wa usalama barabarani tumechafuka aisee,” alisema msimamizi wa askari ambaye hakutaka jina wala eneo lake litajwe gazetini lakini eneo lake lipo Barabara ya Mandela.

Jana, HabariLEO liliandika kuhusu baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani kugeuza daladala mtaja wa kujiaptia rushwa ya kuanzia Sh 2,000 hadi 5,000 na kusababisha kero kubwa kwa abiria.

Uchunguzi wa HabariLEO HabariLeo

Uchunguzi wa HabariLeo ilibaini kuwa kati ya Sh 17,000 na Sh 30,000 hukusanywa kutoka kila daladala kwa siku kupitia ‘vizuizi’ vyenye wastani wa askari watatu kwa kila kimoja katika maeneo tofauti barabarani.

Katika vituo hivyo askari kila mmoja husimamisha magari kwa zamu na kukabidhiwa rushwa hizo. Kutokana na rushwa hiyo, kwa wastani askari mmoja anaweza kukusanya kati ya Sh 600,000 hadi Sh milioni 1.5 kwa mwezi kwa daladala moja.

Ikiwa ana daladala tatu ni takribani Sh milioni 4.5 kwa mwezi au zaidi kutegemea na idadi ya daladala.

Kuwekewa mtego

Kutokana na vitendo hivyo vinavyotia doa Jeshi la Polisi, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbrod Mutafungwa alisema anaunda timu ya uchunguzi itakayofuatilia kwa siri nyendo za askari hao na wote watakaobainika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria, pamoja na kufukuzwa kazi.

“Ni vitu vya ajabu sana, hao makondakta na madereva kukubali kutoa hizo fedha ni ujinga, wasikubali kwa sababu wanapowapa wanaendelea kulea tatizo. Wakatae na kama wataandikiwa makosa kwa sababu ya kukataa kutoa rushwa watoe taarifa kwangu,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Trafiki wanavyopokea

Timu ya waandishi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam pamoja na baadhi ya maeneo ya Pwani, ilibaini vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika bila kificho kati ya wafanyakazi hao wa daladala na askari.

Madereva na makondakta kwa nyakati tofauti wameiomba serikali iingilie kati kuwanusuru na rushwa hiyo waliyoibatiza ‘vicoba ya trafiki’, wakisema hawawezi kuigomea kwa kuhofu kubambikiwa makosa na kukomolewa kwa kuandikiwa faini ya Sh 30,000 kwa kila kosa.

Baadhi ya madereva walisema ni gari haliwezi kukosa mapungufu kabisa na askari hutumia fursa hiyo kuwatishia kuwaandikia faini ya Sh 30,000.

Katika barabara ya Morogoro, gazeti hili limefuatilia kuanzia kituo cha mabasi cha Kibaha mkoani Pwani hadi Mbezi ambako madereva na makondakta walithibitisha kutoa kati ya Sh 17,000 na 28,000 kulingana na vituo vya ‘makusanyo’ vilivyobatizwa ‘vijiwe vya elfu mbili mbili’.

Kutoka stendi ya Kibaha hadi Mbezi vipo vituo vipatavyo vitano ambavyo kila daladala hutozwa ama Sh 2,000 au Sh 3,000.

Askari wengine maarufu kama wa ‘Oysterbay’ wanatajwa kupokea Sh 5,000. “Katika stendi mpya ya Kibaha tunatoa Sh 5,000 na kwenye vituo vingine tunatoa ama Sh 2,000 au 3,000,” alisema dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo na Mbezi, wilayani Ubungo.

Vituo vingine ambavyo kila daladala hutozwa kati ya Sh 2,000 na Sh 3,000, ni Bwawani, Gogoni, Kwa Mangi, Luguruni na Kwa Yusufu vyote vya wilayani Ubungo, Dar es Salaam. Kwa daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi Luis na Temeke kupitia Barabara ya Morogoro na Mandela, vituo vinavyosifika kukusanya fedha hizo ni Kibanda cha Zamani, Suka, Kimara Bucha, Ubungo Darajani na Mwananchi.

Katika barabara itokayo Tangibovu kwenda Goba, kituo cha kwanza ambacho polisi hukaa ni Kayuni ikifuatiwa na Ulomi na kingine kikiwa kabla ya kilima cha kutokea kituo cha Uwanjani.

Kingine ni Njiapanda Nne eneo la Lilian Kibo na Kwa Zulu mbele ya kituo cha Kanisa na kwenye mzunguko wa Mbezi. Katika kituo cha Goba Mwembe Madole (senta), Polisi wamekuwa wakiangalia usalama wa wanaovuka barabara na kuongoza magari kunapotokea msongamano wa magari kati ya Barabara ya Goba na inayotoka Makongo.

Barabara nyingine yenye vitendo hivyo ni Kigamboni wilayani Temeke. Vituo husika ni Pius, Kwa Kipara, Nyumba ya Njano, Chuo, Kibada kwa Hamisi, Shangwe, Mji Mwema, Kijaruba, Big Ston, Gari Bovu na Malaika Beach.

Maeneo mengine ni bara ya kutoka Segerea hadi Mbezi Mwisho ambako askari hao husimamisha daladala na kupokea rushwa hiyo. Utozaji huo wa fedha unafanyika pia kwa daladala zinazotoka Toangoma kwenda Temeke katika vituo vya daladala vya Njia Panda ya Jeshi, Bakwata, Mbagala Rangi Tatu, Misheni Njiapanda ya kwenda Mtoni Kijichi, Mtoni Mtongani, Kwa Azizi Ali, Temeke Mwisho na kituo cha Big Bonn.

Kwa upande wa Barabara ya Temeke kwenda Tazara (Mandela), vituo maarufu kwa utozaji wa fedha kwa makondakta hufanyika kwenye vituo vya Sokota hadi Magorofa ya Tazara.

Kwa Barabara ya Kivule-Kitunda, maeneo ambayo askari hao husimamisha daladala na kupokea fedha hizo ni Makaburini jirani na Daraja la Sirari. Abiria katika maeneo mbalimbali walilalamikia rushwa hiyo wakisema inasababisha baadhi ya daladala kukatisha njia kwa kutofika katika baadhi ya maeneo wakilenga kupunguza idadi ya vituo vya kutoa fedha hizo.

Aidha, abiria wamelalamika kucheleweshwa kufika kazini na kwenye baishara zao kutokana na daladala kusimamishwa kwa muda mrefu au kila mara bila ukaguzi wowote huku kondakta akishuka kupeleka rushwa kwa askari aliyewasimamisha.

“Daladala wanasema wamechoshwa na vikoba ya trafiki ndiyo maana siku hizi magari ya Makumbusho hayaji Kibamba hususani wakati wa asubuhi. Mengi yanageuzia Mbezi,” alisema mmoja wa abiria katika kituo cha daladala cha Kibamba Shule.

Askari wapeana zamu

HabariLEO limebaini kila kituo huwa na wastani wa askari watatu ambao hupeana zamu ya kusimamisha daladala na kupokea fedha hizo. “Anayekusimamisha ndiye anayempelekea mgao,” alisema kondakta wa daladala inayofanya kazi kati ya Kibamba na Mbezi.

“Sasa fikiria, ukikuta wa 3,000 mara tatu, wa 2,000 mara nne na wa 5,0000 mara mbili ni kiasi gani cha pesa tunatoa? Mapato yote tunawafanyia askari,” alisema.

Suala jingine ambalo gazeti hili limebaini ni vitendo hivyo vya kupokea fedha vinafanyika bila kificho kiasi cha kondakta au dereva kushirikisha abiria pale anaposimamishwa kuwa wavumilie anapeleka mgawo na wakati mwingine kuomba chenji kwa abiria.

Muda ambao matukio haya hushuhudiwa zaidi ni asubuhi kati ya saa 1:00 na saa 4:00 asubuhi na majira ya jioni.

Makondakta wabariki rushwa

Baadhi ya makondakta wanaunga mkono kutoa rushwa kwa kile wanachodai kuwa huwapunguzia kadhia ya kukamatwa na kulipishwa faini ya Sh 30,000 zinazoingia serikalini.

Kondakta aliyezungumza na gazeti hili katika Kituo cha Daladala cha Tabata Relini (Mwananchi), alisema ni kawaida kutoa fedha kwa askari kila siku hususan asubuhi ili kupunguza kadhia ya kukamatwa na kulipishwa faini.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) mkoa wa Dar es Salaam, kuna takribani daladala 600 zilizosajiliwa kutoa huduma katika njia mbalimbali. Taarifa ya Latra inaonesha njia ya Gongo la Mboto-Makumbusho ina daladala 42, Mbagala-Kawe 134, Mbagala-Mbezi Luis 21, Mbagala-Gongo la Mboto 17, MakumbushoMbezi Luis 114, Mbezi Luis-Temeke 208 na Kawe-Mbezi Luis 89

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi