loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mpango: Sitakubali Muungano uchezewe

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hatamvumilia yeyote atakayechezea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umetimiza miaka 57 tangu uasisiwe Aprili 26, 1964.

Dk Mpango aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Chimwaga, Dodoma wakati akifungua Kongamano la Miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema lengo la kuweka wizara inayoshughulikia Muungano chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, ni kuulinda na kuuimarisha.

"Kwa kuwa ofisi yangu ndiyo inayoratibu masuala ya Muungano, katika kipindi changu kama Makamu wa Rais wa nchi yetu, sitakubali kabisa wanaochezea Muungano wetu adhimu," alisema Dk Mpango.

Akaongeza: "Kuna baadhi ya mambo watu huwa wanasema mimi ni mpole, lakini kuna vitu huwa nasema mimi si mpole, nilishasema kwa wabadhirifu wa mali za umma mimi si mpole, sasa naongeza na lingine, watakaojaribu kuchezea Muungano, basi hapo sitakuwa mpole."

Dk Mpango alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una mafanikio mengi na kamwe Watanzania wayasibeze mafanikio yaliyopatikana katika miaka 57.

Alisema kuna faida nyingi za Muungano huo ambazo nyingine zinaonekana na nyingine hazionekani moja kwa moja, lakini zinaufanya uendelee kuimarika na kuwanufaisha Watanzania wa pande zote mbili.

Dk Mpango alizitaja baadhi faida za Muungano kuwa ni pamoja na kuimarika kwa udugu wa damu miongoni mwa wananchi kutokana na kuoleana pande zote mbili.

"Niseme tu neno moja hapa kwamba, baba yangu mkubwa amezikwa Zanzibar, kwa hiyo najua wapo ndugu zangu kule Kitope," alisema Makamu wa Rais.

Alizitaja faida nyingine za Muungano kuwa ni pamoja na kudumu kwa umoja na mshikamano wa kitaifa, kuimarika kwa ulinzi na usalama, kukua na kuimarika kwa biashara na shughuli nyingine za kiuchumi na fursa ya kutumia rasilimali zilizopo kwa pamoja ikiwemo ardhi na bahari.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini Rais Dk Hussein Mwinyi, zimeweka suala la kuimarisha Muungano kuwa moja ya vipaumbele vyake, hivyo serikali zote mbili zinaendelea kushirikiana kwa pamoja kudumisha na kuimarisha Muungano wetu," alisema.

Kuhusu changamoto za Muungano, Makamu wa Rais alisema serikali hizo zimefanikiwa kutatua changamoto 15 kati ya 25 na jitihada za kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizobaki zinaendelea.

Dk Mpango alisema kwa kuwa sehemu kubwa ya Watanzania walizaliwa baada ya Mungano mwaka 1964 likiwemo kundi kubwa la vijana, jitihada zinafanyika kukuza uelewa kuhusu historia na matukio muhimu ya taifa.

Alisema kongamano hilo lililenga kukuza uelewa na ufahamu wa jamii kuhusu Muungano na kuenzi mambo muhimu waliyofanya waasisi wa taifa.

Aliwataka Watanzania waendelee kuwaenzi waasisi wa taifa akiwemo Baba wa Taifa, Julius Nyerere (Tanganyika) na Abeid Amani Karume wa Zanzibar kwa misingi imara waliyoijenga iliyoimarisha umoja, amani, utulivu na kujenga uchumi.

GWARIDE

Kutokana na kuzoeleka kwamba kila mwaka wakati wa maadhimisho hayo hufanyika gwaride maalumu, Dk Mpango alisema kwa kuwa Taifa lilipata msiba mkubwa kwa kufiwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli, serikali iliamua lifanyike kongamano badala ya sherehe.

 

Alisema Rais Samia aliagiza fedha zilizopangwa kwa ajili ya maadhimisho hayo zigawanywe kwa pande mbili za Muungano na kila upande uamue namna ya kuzitumia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, alisema Watanzania wanapaswa kuendelea kuuenzi Muungano na kwamba, wengi wao walizaliwa baada ya Muungano huo wa Aprili 26, 1964.

Alisema kongamano hilo liliandaliwa ili kutoa elimu kwa umma kuhusu historia ya Muungano huo na faida zake kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Jafo alisema kaulimbiu ya Kongamano la Miaka 57 ya Muungano inasema "Muungano Wetu ni Msingi Imara wa Mapinduzi ya Kiuchumi, Tuudumishe Muungano Wetu."

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi