loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa aonya urasimu kwa wawekezaji

Majaliwa aonya urasimu kwa wawekezaji

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa serikali kuacha usumbufu na kutengeneza mazingira ya rushwa kwa wawekezaji bali watoe ushirikiano ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

 Aliyasema hayo jana mjini Kibaha Mkoa wa Pwani alipotemebelea kiwanda cha uunganishaji wa mabasi cha BM Motors ambacho ni kampuni ya kwanza kuzalisha mabasi kwa kutumia namba ya utambulisho wa nchi ya Tanzania, na kuelea kuwa usumbufu kwa wawekezaji ni kero na itasababisha washindwe kuwekeza.

 Majaliwa alisema watumishi wa serikali wanapaswa kuwa karibu na wawekezaji na waache usumbufu na kuwa kama mwekezaji anapokwenda ofisini kwa mtendaji kutaka kujua, anaanza kutozwa adhabu hilo halikubaliki na wengine  wanakwenda kuomba ushauri wanaanza kubanwa, hilo halina maana badala yake wawape nguvu.

 “Serikali inapata fursa za kodi tumesisitiza mazingira ulipaji kodi kuondoa usumbufu na kukaa na watendaji wa TRA watumie njia sahihi za sheria za kudai kodi waongeze wigo wa ukusanyaji kodi na kutotumia nguvu ili viwango vibaki vile vile na ikiwezekana walipa kodi waongezeke zaidi,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza, “Changamoto ya ajira sisi mipango yetu ni kuanzisha viwanda kwa kuchukua vijana wengi ili washiriki kwenye shughuli za uzalishaji na hii ni njia mojawapo ya kutatua changamoto ya ajira japo hatuwezi kuajiri wote lakini tunapunguza vijana wengi watapata fursa ya ajira na kuondoa vitendo viovu ndani ya jamii.”

Alisema serikali inalinda bidhaa zinayozalishwa ndani ambazo zina ubora na zikiwa na ubora watapunguza bidhaa kama hizo zinazotoka nje ili kulinda bidhaa za ndani na utaratibu ni kuongeza tozo kwa bidhaa zinazotoka nje, na kuweka tozo rahisi kwa zile za ndani ili hata zikiiingia kwenye soko zifanye vizuri.

 “Umeme uko mwingi na tuanaendelea kuzalisha vyanzo vipya umeme uliopo unaweza kusambazwa kwenye viwanda vyote. Wawekezaji waje kila kitu kipo tutaimarisha barabara…bilioni moja mnaanza nayo ni jambo zuri na fedha iliyotengwa bilioni sita wekeni kwenye mpango ili wawekezaji waweze kupitisha bidhaa na vifaa vyao na wakati mkisubiri kujenga lami babaraba za ndani ziboresheni ili zipitike wakati wote hata wa masika,” alisema Majaliwa.

 Alisema amefurahi kwani nafasi ya kuuza mabasi nchini na nje ipo kwa kuwa yatahitajika mabasi ya mwendokasi katika ujenzi unaofanyika wa Mbagala, Gongolamboto na Tegeta. Pia alisema soko lipo kwa usafiri huo unaweza kwenda hata kwenye mikoa mikubwa kama vile majiji ya Dodoma, Mwanza, Arusha na Mbeya.

“Umepata vibali vyote changamkia fursa zipo na taasisi wezeshi zinapaswa kuwasaidia wawekezaji na hapo waweze kuongeza ajira kwa sasa wameajiri watu 20 waongeze uwekezaji waendelee kuweka mitaji zaidi na pale ambapo haipatikani waongee na mabenki na wamekubali kukopesha wawekezaji endapo wataona mpango kazi mzuri,” alisema.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jonas Nyagawa alisema kwa kuwa amepata namba ya utambulisho ya magari anayotengeneza Tanzania, wana uwezo wa kutengeneza mabasi 10 kwa mwezi, na basi moja gharama yake ni Sh milioni 250 tofauti na mabasi yanayoagizwa toka nchi za nje ambayo yanauzwa hadi milioni 500.

 Nyagawa alisema baada ya kupata vibali vyote anaanza kazi na watasafirisha abiria kwa gharama nafuu na hata yale watakayoyauza watauza kwa bei nafuu na watawakopesha wenye uwezo mdogo ili walipe kwa awamu.

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema eneo la viwanda kwenye Halmashauri ya Mji wa KIbaha kuna hekari zaidi ya 1,600 na kuna viwanja 175 na kati ya hivyo 153 vimemilikishwa ambako kuna viwanda vikubwa 25.

foto
Mwandishi: John Gagarini, Kibaha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi