loader
Karibu Samia kilingeni CCM

Karibu Samia kilingeni CCM

KESHOKUTWA Ijumaa, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kukabidhiwa kijiti cha kukiongoza Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho tawala jijini Dodoma.

CCM ambayo imeiongoza Tanzania tangu kuasisiwa kwake Februari 5, 1977, imekuwa na utaratibu wa kofia mbili zote; ya Urais wa Tanzania na ya Uenyekiti wa Taifa wa CCM tangu enzi za Baba wa Taia, Mwalimu Julius Nyerere kumkabidhi mtu mmoja.

Rais Samia alishika hatamu za kuiongoza Tanzania, Machi 19, mwaka huu kutokana na kifo cha Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 kutokana na maradhi ya moyo.

Hivyo, inatarajiwa kuwa keshokutwa wajumbe takribani 2,000 wataendeleza utamaduni huo wa kumfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayetoka CCM kuwa pia Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kikongwe nchini.

Julai 23, 2016, Rais Magufuli alikabidhiwa kiti cha Uenyekiti wa CCM Taifa kutoka kwa mtangulizi wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, kuendeleza utamaduni huo ambao umekuwa na nia ya kuhakikisha Rais na Mwenyekiti wa CCM anaongoza nchi akiwa na kofia zote mbili ili kumrahisishia katika utendaji wake.

Rais Samia ni mwanachama wa CCM mwenye uzoefu mkubwa katika siasa za Tanzania akiwa amewahi kuwa katika nafasi ya juu kabisa ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM – chombo ambacho hupanga mwelekeo wa chama na serikali kwa kuwa ndicho hutoa dira ya nini cha kufanya kwa chama na serikali yake.

Kamati Kuu ndicho chombo chenye nguvu katika uendeshaji wa CCM ikifuatiwa na Mkutano Mkuu ambao ndio wenye maamuzi makubwa kikatiba ambayo yamewekwa kwa chombo hicho ambacho Ijumaa wiki hii kitakutana jijini Dodoma kumpitisha Rais Samia kushika wadhifa wa Uenyekiti wa CCM Taifa.

Mbali ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Rais Samia pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na pia Mkutano Mkuu hivyo ana uzoefu mkubwa katika masuala ya siasa, na katika muktadha huo, kukabidhiwa nafasi ya kuiongoza CCM, hakuna shaka yoyote kwamba atakiendesha vyema kwa sababu anakijua kwa upana wake.

Vikao hasa Kamati Kuu ni sehemu ambayo Rais Samia amekaa kwa muda mrefu na humo amejifunza kupitia kwa viongozi au marais waliomtangulia, jambo linaloonesha hatakuwa na shida katika kuendeleza chama hicho na serikali kwa ujumla katika kuiongoza Tanzania.

Aidha, uzoefu wake wa kuwa mbunge ambaye anaingia katika vikao vya chama kuanzia ngazi ya wilaya, ni kete nyingine ya uzoefu wake mkubwa katika Chama Cha Mapinduzi, hivyo hatakuwa mgeni katika kukiongoza. 

Lakini turufu yake nyingine ni jinsi alivyoweza kuongoza kwa umahiri mkubwa vikao vya Bunge la Katiba mwaka 2014 akimsaidia Mwenyekiti wake, Samuel Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania.

Alionesha umahiri mkubwa katika Bunge hilo la Katiba ambalo lilisheheni watu wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi wanaoheshimika nchini, lakini akamudu kuliongoza vizuri akimsaidia Sitta.

Haikushangaza alipopendekezwa na Dk Magufuli kuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais wa Tanzania mwaka 2015 na baadaye mwaka jana, na wawili hao kuibuka washindi kwa kishindo katika awamu zote mbili.

Katika mahojiano na waandishi wa Kampuni ya Uhuru Media Group, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amesema imani yake kwa Rais Samia inatokana na uzoefu wa nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika ndani ya chama na serikali ambazo zimemjengea uwezo na umahiri katika uongozi.

Amesema Rais Samia amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, Taifa (NEC), kadhalika Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, pia uzoefu wake unabebwa na nafasi za juu alizowahi kushika serikalini.

Kikwete amesema sifa ya CCM ni kujali maslahi ya wananchi wakiwemo wafanyakazi, kusimamia haki na kwamba Rais Samia ameyathibitisha hayo kupitia hotuba ya mwelekeo wa serikali yake, hivyo huo ni mtaji wa kufanya vizuri.

“Kwenye NEC, tulikuwa tunakaa naye na alikuwa mchangiaji mzuri wa mawazo. Unajua wakati mwingine kuna watu wanakuwa wajumbe lakini toka amechaguliwa mpaka siku uchaguzi unaofuata mwingine, hata siku moja hajasimama kusema jambo lolote, wako wengi tu, lakini Samia alikuwa mshiriki mzuri sana anayetoa mawazo mazuri mazuri, mawazo yanayojenga,” anasema Kikwete.

Hivyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM keshokutwa wanatarajiwa kufanya kazi moja tu – kumuidhinisha kwa kura kukalia kiti hicho na kuendeleza walipoishia watangulizi wake akiwamo Dk Magufuli ambaye kiuzoefu, hakuwa mwanasiasa kama alivyo Rais Samia au wenyeviti wengine waliotangulia, akina Mwalimu Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete.

Kumekuwapo na maneno mengine mitandaoni ya kudaiwa kuwa baadhi ya wanaCCM wanafikiria kutenganisha kofia hizo mbili – Urais na Uenyekiti wa CCM.

Mwishoni mwa wiki, Rais mstaafu Kikwete amekaririwa akisema kuwa hatarajii utamaduni tofauti kwa chama kuitenganisha kofia ya uenyekiti na urais.

Katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari kutoka Kampuni ya Uhuru Media Group (UMG), Kikwete alisisitiza kuwa hilo halitarajii kwa kuwa halina tija wala afya kwa Chama Cha Mapinduzi na nchi kwa ujumla.

Kuhusu historia ya kofia mbili, amesema CCM imewahi kupitia katika historia ya kiongozi mmoja kuwa na kofia mbili kipindi ambacho katibu wa chama wa wilaya ndiye aliyekuwa mkuu wa wilaya na katibu wa mkoa alikuwa mkuu wa mkoa.

Utaratibu huo uliondolewa kupitia mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika mwaka 1982 ambayo kofia hizo mbili zilitenganishwa na kila moja kusimama peke yake.

“Mimi sifikirii kwamba kutakuwa na utaratibu tofauti na tukitengeneza utaratibu huo tofauti utakuwa hauna maslahi kwa chama na taifa... Busara iliyotumika kutotenganisha kofia mbili urais na uenyekiti wa chama iendelee kutumika,” alisema Kikwete, mmoja wa viongozi waliolelewa na kukulia ndani ya CCM kabla ya kuingia serikalini.

Aidha, Kikwete amesema pamoja na kwamba yeye na wenzake sasa ni wastaafu, wamebaki kuwa washauri kwa ajili ya ustawi wa CCM na nchi kwa ujumla, lakini haamini kama kuna mwana-CCM anayeweza kukubali kujaribu kufanya jambo linaloweza kusababisha mustakabali wa maendeleo ya chama kuwa finyu.

Ni vyema Rais Samia akapewa kiti cha uenyekiti wa CCM ili ayasimamie na kuyatekeleza kikamilifu yale ambayo ameyaahidi katika hotuba yake bungeni Alhamisi iliyopita, akisema mwendo ni ule ule aliouanzisha mtangulizi wake, Dk Magufuli wa kulinda rasilimali za umma na kuonya wale wote watakaofanya mambo ya ovyo.

“Naomba kutumia jukwaa hili la Bunge kusema mambo mawili. Kwanza ni kuwaonya wale wote wanaodhani kuwa usimamizi wa mali za umma, kusimamia ukwepaji wa kodi, kusimamia uzibaji wa mianya ya kupoteza mapato, kukemea uzembe na wizi, yameondoshwa kutokana na kuondoka kwa Mheshimiwa Hayati Dk John Magufuli,” alisema Rais Samia.

“Mheshimwa Spika, nataka niseme hayati mpendwa wetu amekwenda peke yake na kama nilivyosema wakati siku ile tunamsindikiza kwamba maono, falsafa na mikakati aliyotuachia tunaendelea kuyafanyia kazi, hivyo basi wale wanaodhani yale amekwenda nayo wamejidanganya yapo na tunayatekeleza.”

Ni imani ya wengi kuwa kama ambavyo Rais Samia ameahidi kuendeleza mwendo ule ule serikalini, atakuwa na nafasi kubwa ya kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM akiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa. Apewe kofia ya pili akamilishe utekelezaji wa ilani hiyo iliyosheheni mambo mengi mazuri kwa Watanzania.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f23e098643accc5cf8e55458107b4759.jpg

SERIKALI hivi karibuni ilitangaza nyongeza ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi