loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujenge utamaduni wa kusoma vitabu ili kupata maarifa zaidi

USOMAJI wa vitabu barani Afrika ni utamaduni ambao haujazoeleka, na hata wanaonunua vitabu ukiwauliza kama wamevisoma wanakuwa na sababu za kushindwa kusoma.

Ijumaa iliyopita ilikuwa Siku ya Kimataifa ya Vitabu na Hakimiliki. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limekuwa likiadhimisha siku hii kila Aprili 23 kwa miaka 26 sasa.

Nchi wanachama wa Unesco huadhimisha siku hii kwa kutambua umuhimu na uwezo wa vitabu kuwaleta watu pamoja na kuelimisha kuhusu utamaduni wa watu na ndoto zao za mustakabali bora hapo baadaye.

Aprili 23, 1616 ndiyo siku ambayo wanafasihi wakubwa wa zama hizo, Miguel de Cervantes, William Shakespeare na Inca Garcilaso, walifariki dunia na kuacha hazina kubwa ya kazi za fasihi nyuma yao, hazina ambayo hadi leo bado inaendelea kuvunwa na vizazi vyetu.

Aidha tarehe hii ni siku ambayo, kwa miaka tofauti waandishi wengine wakubwa duniani walizaliwa.

Ni kwa misingi hiyo, Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni uliofanyika jijini Paris mwaka 1995 liliamua kuifanya tarehe hiyo kuwa siku ya vitabu na hakimiliki duniani.

Lengo kubwa ni kuvienzi vitabu na waandishi wa vitabu duniani kote, na kwa kufanya hivyo, kuwahamasisha watu hususan vijana ili kutambua umuhimu wa kusoma vitabu na kuhuisha heshima kwa mchango usiohamishika wala usiofutika wa waandishi na wote waliowekeza katika kukuza fasihi andishi na kuleta maendelea ya ufahamu, utamaduni na uelewa duniani, kupitia maandishi yao.

Kama sehemu ya mila hii inayokubalika na mataifa yote duniani, kila mwaka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni likishirikiana na mashirika mengine ya kimataifa yanayowakilisha mihimili mikuu mitatu ya tasnia ya vitabu (wachapishaji vitabu, wauzaji vitabu na maktaba) huchagua mji mkuu wa vitabu ambao hudumu kwa mwaka mmoja kuanzia Aprili 23 ya kila mwaka.

Mji mkuu wa vitabu uliochaguliwa kwa mwaka 2021 ni mji wa Tbilisi, Georgia.

Wakati fulani unaweza kujiuliza, kwa nini watu wanapenda sana kusoma vitabu? Kwa nini watu wanaweka malengo ya usomaji wa vitabu? Zipo faida nyingi mno za usomaji wa vitabu.

Kwa hakika kuna maarifa mengi yaliyofichwa kwenye vitabu na hivyo waandishi na wadau mbalimbali wa usomaji vitabu huitumia siku hii kujadili kuhusu vitabu, hakimiliki na kufanya maonesho ya vitabu.

Mtu huongeza maarifa kwa kusafiri maeneo mbalimbali na kukutana na watu wengine wenye mtazamo, mawazo, uzoefu tofauti na wake. Lakini anaweza kuongeza maarifa kwa kusoma vitabu; kwani kwa kusoma vitabu atajikuta akisafiri sehemu mbalimbali duniani huku akiwa amekaa tu kwenye kiti chake na kitabu chake mkononi, akisoma na kujipatia ujuzi, uzoefu na mawazo ya watu mbalimbali kutoka kila kona ya dunia.

Kwenye vitabu pekee ndiyo mahali unapoweza kukutana na watu waliokwisha kufa, na ukawasikia mawazo yao.

Kila jambo utakalolisoma kwenye kitabu hukupa taarifa mpya. Huwezi fahamu ni wakati gani maarifa hayo yatakusaidia katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha yako.

Kuwa na utajiri wa maarifa ni nyenzo muhimu sana ya kukabiliana na changamoto pindi zinapojitokeza maishani mwako. Katika maisha, unaweza kupoteza vitu vingi kama kazi, cheo, fedha, marafiki na kadhalika, lakini huwezi kuyapoteza maarifa uliyonayo.

Hata hivyo, kwa nchi nyingi za Afrika ni watu wachache sana ndio wanaopenda na wanafahamu umuhimu wa kusoma vitabu. Watu wengi hawapendi kusoma vitabu ikiwa hakuna kinachowalazimisha kufanya hivyo kama vile mtihani, kazi n.k.

Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi. Hivyo kwa kusoma vitabu unapata maarifa mbalimbali yaliyowekwa kwenye kitabu husika.

Hivi leo kuna vitabu vinavyohusu takriban kila kitu; kwa hiyo maarifa yoyote unayoyahitaji unaweza kuyapata kwenye vitabu.

Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi, mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.

Pia mbinu kubwa ya kuongeza uwezo wa lugha ni kusoma machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha unayotaka kujifunza. Kwa kusoma vitabu utaongeza misamiati, utajifunza sarufi ya lugha au hata mbinu mbalimbali za matumizi ya lugha.

Unachotakiwa kuzingatia hapa ni kusoma vitabu bora mara nyingi kadri uwezavyo.

Maisha yana changamoto mbalimbali, hivyo tunahitaji kitu cha kutuhamasisha kutoka hatua moja hadi nyingine. Kwa kusoma vitabu vya hamasa kuhusu masuala mbalimbali ya maisha tutaweza kuhamasika zaidi.

Haijalishi unapitia magumu yepi mahala pa kazi, ama migogoro mikubwa kiasi gani katika uhusiano ama masaibu yasiyohesabika katika maisha yako ya kila siku; hayo yote hupunguza kukuzonga kadri unavyozama katika kusoma simulizi kabambe ya kusisimua.

Riwaya iliyoandikwa kiustadi huweza kukusafirisha hadi katika ulimwengu mwingine kabisa na kukuondoa katika hali ya sasa ikuzongayo na hivyo kukupa nafasi ya kuburudika kiakili.

Pia vipo vitabu vilivyoandikwa kwa ajili ya kukuhamasisha au vilivyoandikwa maelezo ya watu waliofanikiwa na jinsi walivyopita kutoka changamoto moja hadi nyingine mpaka kufanikiwa kwao.

Katika ujumbe wake maalumu kuhusu siku hii Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Bi Irina Bokova anasema siku hii inatoa fursa ya kutafakari kwa pamoja njia nzuri za kuelimisha kuhusu utamaduni ulioandikwa vitabuni na kuruhusu watu wote wanaume, wanawake na watoto kupata ujumbe huo kupitia programu maalumu ya kufuta ujinga na kuunga mkono fani ya uchapishaji vitabu, maduka ya uuzaji vitabu, maktaba mbalimbali na pia shuleni.

Bi Bokova anaongeza kuwa vitabu ni mshirika mkubwa wa kusambaza elimu, sayansi, utamaduni na taarifa mbalimbali duniani kote, na hivyo siku hii ni mahsusi kwa ajili ya kuchagiza elimu na usomaji, lakini pia kulinda hakimiliki ya upatikanaji na utajiri wa vitabu duniani.

Hakimiliki ni utaratibu wa kisheria unaompa mmiliki wa kazi za akili (kama vile kitabu, sinema, picha, wimbo au tovuti) haki ya kujiamulia matumizi yake.

Sheria za hakimiliki zinalenga kukinga watunzi wa kazi za kiakili dhidi ya matumizi ya kazi yao na wengine wanaojipatia faida kwa njia hiyo bila kumzingatia mtunzi wa kazi husika anayeweza kukosa ruzuku kutokana na kazi yake.

Hakimiliki ni muhimu sana kwa waandishi kwa sababu inafanya umiliki wa kazi ya awali. Kuwa na umiliki ina maana unaweza kulinda kazi yako kama mali na udhibiti wa kiakili kwako na kwa wale unaowapa haki.

Watunzi wana hakimiliki kwa vitabu vyao; mkataba wa kitabu hudhibiti sehemu za matumizi ya haki hizo na malipo yaliyotolewa.

Chini ya sheria za hakimiliki, kazi ya kiakili inaweza kunakiliwa pekee ikiwa mmiliki anatoa ruhusa. Ikiwa mtu ananakili kazi bila kibali, anakiuka hakimiliki.

Kutegemeana na sheria za nchi mbalimbali mkiukaji anaweza kushtakiwa chini ya sheria za biashara au wakati mwingine sheria za jinai. Mkiukaji anaweza kuhukumiwa kulipa fidia au hata kwenda jela.

Kwa kawaida, sheria za hakimiliki hulinda haki za watunzi na warithi wao kwa kipindi fulani, katika sheria ya kimataifa angalau hadi miaka 50 baada ya kifo cha mtunzi. Nchi mbalimbali huwa na vipindi virefu zaidi.

Katika nchi zinazofuata zaidi sheria za Marekani kuna kanuni zinazorahisisha kampuni kushika hakimiliki badala ya wafanyakazi wake kama kazi ilitekelezwa ofisini.

Kutokana na umuhimu wa hakimiliki Serikali ya Marekani inatambua kuwa; “hakimiliki ni aina ya ulinzi na imewekwa katika Katiba ya nchi hiyo na kupewa sheria kwa kazi za awali za uandishi uliowekwa kati ya maneno ya kuonekana.”

0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi