loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumia fursa ya saumu  kuomba utakacho

HADITHI iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Huraira inasema Mtume Muhammad (SAW) amesema kwamba watu watatu ambao dua zao hazirejeshwi ni wafuatao; kiongozi mtenda haki, mwenye saumu wakati anapofungua na mwenyekudhulumiwa.

Hadithi hii imesimuliwa na Tirmidhi ni hadithi nambari (2525), na pia Albaani amesema ni hadithi sahihi.

Kutokana na hadithi ni dalili kuwa mwenye saumu anatakiwa akitumie kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kila anapokuwa anataka kufuturu aombe dua za heri, kwani Mwenyezi Mungu, kupitia kinywa cha Mtume wake (SAW) ameahidi kujibu dua zake.

Bora zaidi cha kusema wakati huo ni yale yaliyopokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Umar kwamba Mtume Muhammad (SAW) anapofungua saumu alikuwa anasema: Dhahaba al-dhamau’, wa abtallat al-‘uruuq wa thabata al-ajr insha Allah (Kiu kimeondoka, mishipa imelowana na ujira umethibiti, in-shaa-Allaah). Imesimuliwa na Abuu Dawuud (2357). Albaani anasema ni hadithi hasana katika Swahiyh Abi Dawuud (2066).

Baada ya hapo mwenye saumu aombe mambo mengine ya heri ayatakayo ikiwa ni pamoja na kuomba aachwe huru na moto. Maombi yanaweza kufanywa kwa lugha yoyote. Mwenye saumu anapoomba wakati huu, anatakikana ahudhurishe moyo wake na awe na yakini kwamba Mungu atamwitikia dua yake hiyo, kwani huo ni wakati wa udhalili na unyenyekevu mkubwa kwa Mungu.

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Saiyd Al-Khudriyy kwamba Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwenyezi Mungu anawaacha huru na moto kila siku ya Ramadhani usiku, na kila mja kati yao ana dua inayojibiwa.” 

Hadithi hii imesimuliwa na Ahmad (7401) na Albaani kasema ni sahihi katika katika kitabu chake cha Swahihy Al-Jaami’i (2169).

Ni vizuri mfungaji kuomba sana dua hii kwani hakuna mafanikio makubwa kama mtu kuwekwa mbali na moto wa jehanamu.

Mbali na mwenye saumu kuomba dua kwa moyo safi na maombi halali ya kisheria, ahakikishe kusiwe na kizuizi cha kukubaliwa dua kama vile mtu kufutru au kula chakula cha haramu na kadhalika. 

Mfungaji anatakiwa kuwajibika kwa kufuata ipasavyo maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake.

Ukimbukwe pia kwamba Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume wake katika Kurani kwamba: “Na watakapokuuliza waja wangu kuhusu mimi, basi mimi ni niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia dua ya mwombaji anaponiomba. Basi waniitikie mimi na waniamini mimi, wapate kuongoka. (Al-Baqarah: 186)

Kingine anachotakiwa mfungaji wa saumu kushikamana nacho ni kukithirisha kumtaja Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha mchana, kwani saumu humfanya awe karibu zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo wakati anapokuja kumwomba wakati wa kufungua saumu anakuwa tayari amekuwa karibu na Mwenyezi Mungu.

Swala za usiku

Swala iitwayo Tahajjud ni swala inayoswaliwa usiku na kwa jina lingine huitwa Qiyaamul-Lail (kimamo chama swali ya usiku). Nayo huswaliwa wakati wowote baada ya swala ya Ishaa mpaka karibu na alfajiri.

Ni vema zaidi mtu kupata fadhila nyingi zaidi kwa kuiswali katika theluthi ya mwisho ya usiku kama ilivyo katika hadithi ifuatayo iliyopokelewa na Abuu Hurayrah.

Mtume Muhammad (SAW) amesema: Mwenyezi Mungu huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu na ukubwa wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia theluthi ya mwisho ya usiku na husema: Nani ananiomba dua nimwitike? Nani ananiomba jambo nimpe? Nani ananiomba msamaha nimsamehe? (Hadithi inapatikana katika Bukhaari na Muslim)

Theluthi ya mwisho ya usiku ni kuanzia kwenye saa nane hivi usiku hadi karibu na swala ya alfajiri.

Idadi ya rakaa swala za usiku

Kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhari, swala za usiku ni rakaa mbilimbili kiasi cha uwezo wa mtu. 

Yaani kila baada ya rakaa mbili unatoa salamu na ukihisi alfajiri inakaribia basi unaswali  Witr.

Witr inaweza kuwa rakaa moja, tatu, tano, saba na kadhalika lakini kwa uchache ni rakaa moja.

Hata hivyo, ingawa unaweza kuswali rakaa nyingi kadri ya uwezo wako Suna ni kuswali rakaa kumi na moja (rakaa nane na witr rakaa tatu) na hii ni kutokana na hadithi ya Aisha kwamba: “Nabii (SWA) alikuwa akiswali za usiku rakaa 10, anatoa salaam baada ya kila rakaa mbili kisha anaswali Witr, rakaa moja.”   (Muslim).

Bibi Aisha akasema vilevile kwamba: “Hajapata Nabii (SAW) kuzidisha katika Ramadhani wala miezi mingine zaidi ya rakaa 11, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali tatu.”  (Bukhaari na Muslim).

Sura za kusoma swala za usiku

 Hakuna sura maaluumu ya kusomwa katika swala za usiku, bali ni vizuri sana kusoma sura ndefu kwa dalili ya hadithi ya Aisha iliyotangulia kwamba: “Wala usiniulize uzuri wake na urefu wake.”

Mama huyu alikusudia kuwa Mtume Muhammad (SAW) alikuwa akiswali swala kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine sura ndefu, rukuu ndefu, sujudu ndefu na kadhalika.

Hii pia inakwenda sambamba na na hadithi inayotaja fadhila za kusoma aya yingi katika swala za usiku:

“Atakayesimama (usiku) na aaya kumi hatoandikwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa aya mia ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu, na atakayesimama kwa aya elfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi (ya thawabu nyingi). (Abuu Dawuud na hadithi amesahihisha Al-Albaani.

Ama katika rakaa tatu za mwisho Imepokelewa kutoka kwa ‘Aisha akisema: “Nabii (SAW) alikuwa akisoma katika rakaa ya mwanzo (ya swala ya Witr) “Sabbihisma Rabikal-A'alaa” na rakaa ya pili “Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruun” na rakaa ya tatu “Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'uudhu mbili (Al Falaq na An Naas).”  [Tirmidhiy]

Rakaa hizi tatu za mwisho vilevile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo rakaa ya mwisho bada ya kuinuka katika rukuu usome du'aa ya Qunuut.

Au pia unaweza kuziswali zote tatu kwa Tashahhud moja ya mwisho na kisha kutoa salaamu, yaani bila kusoma taahiyaat kwenye rakaa ya pili.

Ulamaa wamesema kusema kuunga rakaa tatu kwa pamoja ni kuitofautisha na swala ya Maghrib ambayo unakaa tahiyatu baada ya rakaa mbili.

Sawa na kuswali usiku mzima

Ndugu zetu wanaojitahidi kuswali swala ya Tarawihi na Witr pamoja na imamu wanafanya jambo jema kwani wanahesabiwa kwamba wameswali usiku mzima.

Hii inatokana na haditi ya Mtume (SAW) ambaye amesema: “Yule mwenye kusimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi huandikiwa ameswali usiku mzima.”

Tazama katika Abu Dawuud (1375) na at-Tirmidhiy (806). Ni hadithi sahihi kwa mujibu wa al-Albaani.

Kwa hiyo, hata kama mtu hatosimama tena kuswali usiku ili kuzidi kujipendekeza zaidi kwa mola wake, itakuwa tayari ana malipo kwa kuswali usiku mzima.

Ni vyema isisitizwe hapa kwamba malipo haya hayapati yule atakayewahi kuondoka kabla imamu hajamaliza witr, hivyo ni muhimu sana watu kuhakikisha wanaswali na imamu hadi mwisho wa Witr baada ya sala ya Tarawihi. 

 Hili halijathibiti

 Kwa wale wanaoleta adh-kari baada ya kila rakaa mbili au nne, hakuna dalili ya hilo kuwa Nabii (SAW) au maswahaba walikuwa wakileta adhkari yoyote kila baada ya rakaa mbili katika Swalaah ya Tarawihi.

Kutoka Kitabu: Almad-khal cha Ibnul-Haaj Almaalikiy adhkaar zilizothibiti ni ambazo unatakiwa useme mwisho kabisa wa kumaliza swala yako ya usiku, yaani unapomaliza witr useme:

Sub-haanal-Malikil-Qudduwsi mara tatu (Utakasifu ni wa Allaah Mfalme, Mtakatifu) na Rabbil-Malaaikati war-Ruuh (Ee Rabi wa Malaika na wa Jibril).

Dalili ya kuleta adhkari hizo ni hadithi ya ‘Abdur-Rahmaan bin Abzay  An-Nasaaiy (3/244).

  Zingatia haya mwezi huu

Endelea kuzingatia kwamba mwezi huu mtukufu ni wa kwako kujihesabu, kutenda amali nyingi na kujirekebisha hali yako na uhusiano wako na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuufanya kuwa bora zaidi.

Kumbuka kwamba huu mwezi ni mgeni ambaye amekutembelea kisha ataondoka, hivyo baada ya kumpokea mgeni endelea  kumkirimu kwa mazuri yote anayostahiki.

Tahadhari na kutokufunga bila ya sababu au udhuru wowote, kwani kufanya hivyo, saumu yako haitolipika hata ukifunga mwaka mzima.

Jitajidi kuswali kwa wakati wake, usiache swala ikakupita. Elewa kuwa ukiwa unafunga bila kuswali, kama wanavyosema vijana ni sawa na kuchaji simu huku ndani jukiwa hakuna betri! 

Soma sana Kurani kadiri uwezavyo kwani ni mwezi ulioteremshwa Kurani. Kamilisha msahafu mzima japo mara moja, ukishindwa basi hata nusu yake au robo yake. Zidisha ibada za suna, kama suna zilizo zilizosisitizwa na zisizosisitizwa.

Wabillaahi Tawfiiq.

 

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi