loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Matumizi ya sayansi katika kilimo na tija kwa mkulima

SAYANSI ya kilimo ni tawi la biolojia linalohusisha elimu mbalimbali zinazotumiwa katika kuboresha kilimo. Mara nyingi huhusisha elimu ya kilimo cha mimea, elimu ya mifugo na uchumi wa kilimo na tiba ya mifugo.

Sayansi ya kilimo ni pamoja na utafiti na maendeleo kama vile ukuzaji mimea na magonjwa, kilimo cha bustani, sayansi ya udongo, elimu ya wadudu, uhifadhi wa nyuki na mbinu za uzalishaji  kwa maana ya umwagiliaji na matumizi ya mbolea.

Sayansi hii pia huhusisha uboreshaji na uzalishaji wa kilimo kwa viwango na ubora, yaani uteuzi wa mazao na wanyama, wanyamapori katika kuvumilia ukame, kuanzisha dawa mpya na teknolojia ya kuboresha mavuno.

Hali kadhalika ni sayansi inayojikita katika kupunguza athari za magugu, vimelea vya magonjwa, minyoo-kuru kwenye mifumo ya uzalishaji wa mazao au mifugo, kubadilisha bidhaa asilia kuwa bidhaa zitumiwazo na wanunuzi wa mwisho yaani uzalishaji, uhifadhi, na ufungaji wa bidhaa za maziwa na kinga dhidi ya athari mbaya za mazingira kwa maana ya uharibifu wa udongo na taka za plasiki.

Kilimo cha kisayansi ni chenye tija kwa mkulima mdogo na mkubwa pale kinapozingatia misingi hiyo ya kitaalamu na soko la uhakika na hivyo ni ufumbuzi wa maisha bora hasa kwa mkulima mdogo wa kijijini.

Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Mazao ya Kilimo na Ufugaji Nyuki katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mkabwa Manoko anasema elimu inayotolewa kwa wanafunzi katika idara hiyo ni pamoja na ya vitendo.

Anasema wanafunzi hupelekwa katika shamba darasa chuoni hapo kwa ajili hiyo.

Dk Manoko anasema kwa njia hiyo ya masomo ya vitendo vijana wanaangalia na kupewa elimu ya kisayansi, hatua ambazo mkulima akizifuata anafanikiwa kutokana na kulima kisanyansi.

Anasema Idara hiyo haipo kwa ajili ya wanafunzi pekee bali poa kwa wakulima wanaohitaji ushauri na namna ya kuanzisha kilimo, ufugaji wa nyuki mjini, ufugaji wa samaki nk bila malipo ya aina yoyote.

Dk Manoko anasema ili kumsaidia mkulima nchini, idara hiyo inatarajia kutoa elimu zaidi ya kilimo cha kisayansi kwa kutumia wanafunzi na mwalimu kwa mkulima mmoja mmoja.

Anasema elimu ya uzalishaji wa mazao ya chakula ni muhimu kwa wakulima nchini kutokana na kwamba kilimo cha Tanzania ndicho mpaka sasa kinawalisha Watanzania kwa asilimia 100.

Hivi sasa chakula ni biashara kubwa duniani na kwamba bado wazalishaji wakuu wa chakula ni pamoja na mataifa ya China, India, Brazil, Marekani na Umoja wa Ulaya.

Anasema serikali haina budi kuongeza fedha katika vyuo vikuu hususan idara zinahusiana na masuala ya kilimo nchini ili kusaidia mafunzo yatakayochangia kubadilisha kwa haraka kilimo cha Tanzania.

Anasema sayansi anuwai zinazohusiana na kilimo na mazingira kama vile sayansi ya udongo, taaluma ya hali ya hewa kwa kilimo na kadhalika ni lazima ziwe na wataalamu wa kuwasaidia wakulima.

Mengine yanayohitaji watalaamu anasema ni biolojia ya mazao ya kilimo na mifugo, nyanja kama uchumi wa kilimo na sosholojia ya vijijini pamoja na taaluma mbali mbali zilizojumuishwa katika uhandisi wa kilimo

Anasema hadi miaka ya 1850 baadhi ya mataifa yalikuwa na ufanisi wa kutosha kugharamia utafiti katika kilimo, utafiti ambao umeendelea kuleta mabadiliko hadi sasa.

Anatoa mfano kwamba wazalishaji wa mimea wamechunguza mbegu za urithi na kuzalisha mimea inayoweza kuzaa sana na kustahimili magonjwa na ukame.

Watafiti pia wamegundua mchanganyiko unaofaa wa nitrati na fosfati kwa ajili ya mimea na udongo wa aina mbalimbali.

Magugu yalisababisha vibarua wawe na kazi ngumu ya kuyaondoa wengi wao walipoteza kazi baada ya wanasayansi kugundua dawa za kuua magugu.

Wadudu, minyoo na fukusi wamekuwa adui wa mkulima tangu jadi na kwamba sasa wakulima wanaweza kuchagua kemikali mbalimbali za kuua wadudu waharibifu na visumbufu vingine.

Katika nchi zilizoendelea maisha ya wakulima na wafugaji pia yamebadilika, mashine za kulisha na kukamua maziwa zimewawezesha wachungaji na wasaidizi wao kuchunga takribani ng’ombe 200 katika eneo maalumu.

Wafugaji wanaweza pia kunenepesha ndama na nguruwe haraka kuliko ilivyokuwa zamani kwa kuwafuga kwenye zizi badala ya kuwapeleka kondeni na uwezo wa kudhibiti chakula na joto la wanyama hao.

Mara nyingi matokeo ya ukulima wa kutumia mbinu za kisayansi umekuwa wa kustaajabisha kwa kuongeza uzalishaji maradufu kuliko kutegemea kilimo cha kimazoea.

Katika nchi nyingi duniani, mkulima ni mfanyabiashara mwenye elimu ambaye amebobea katika kuzalisha kwa wingi mazao au zao moja, jambo ambalo Tanzania pia linahitajika sana.

Serikali pia zina dhima ya kuwaaidia wakulima kwenyue soko kwani wanatumia pesa nyingi kununua mashamba, majengo na mashine lakini bado anawategemea watu wengine kupanga bei ya mazao yao.

Kampuni kubwa za kusindika vyakula na maduka makubwa huamua bei, aina, ukubwa, na rangi ya mazao ya mkulima.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili.

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Maria Inviolata

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi