loader
Dstv Habarileo  Mobile
Nyalandu aikimbia ‘nchi ya ugenini,’ arejea CCM

Nyalandu aikimbia ‘nchi ya ugenini,’ arejea CCM

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Lazaro Nyalandu amekihama chama hicho na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) akilinganisha chama hicho cha upinzani na nchi ya ugenini ambayo hakuweza kutimiza matakwa waliyohitaji.

Mwingine aliyekihama chama hicho ni Suleiman Luwongo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini na pia Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Lindi, aliyesema ameamua kwa ridhaa yake kurudi nyumbani kwa sababu kadiri anavyoendelea kuwa nje ya CCM anajihisi kuwa ana upungufu.

Viongozi hao walitangaza uamuzi huo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika jijini Dodoma jana kumuidhinisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa kufuatia kifo cha Rais na Mwenyekiti wa CCM, Dk John Magufuli, Machi 17, mwaka huu.

“Nakupongeza kwa dhati kwa niaba ya wengi kwa uongozi wako shupavu. Naomba nitoe pole kwako na kwa wana CCM wote na Watanzania wote kwa kuondokewa na rais wetu mpendwa, John Pombe Magufuli msiba ambao hakika uliigusa Tanzania na kuhuzunisha taifa,” alisema Nyalandu na kumpa pole pia mjane, Janeth Magufuli.

Aliendelea, “Kupitia mkutano huu maalumu wa CCM naomba kukushukuru sana kwa kukubali kunipokea, kunisamehe na kuniruhusu kurejea tena nyumbani. Kwani hakuna furaha izidiyo furaha ya mtoto arejeapo nyumbani…”

Akinukuu mistari minne ya kwanza kutoka kitabu Zaburi 137 katika Biblia, Nyalandu aliwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu kuwa katika nchi ya ugenini (Chadema) wimbo wa Bwana hauimbiki.

Alisoma mistari hiyo inayosema: “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka tuwatumbuize; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Twawezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni?”

Aliwataja wazee walio-

kuwa wanaCCM na baadaye wakakihama kuingia Chadema, lakini waliishia kurejea kwenye chama tawala kutokana na kile alichosema walimethibitisha kuwa wimbo wa Bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini.

“Mzee Lowassa (Edward) kama yupo, Mzee Frederick Sumaye baba yangu nakuona hapo, Mzee wetu Wilbrod Slaa hao ni mashuhuda wachache kati ya wengi ambao wamethibitisha kuwa wimbo wa Bwana hauimbiki katika nchi ya ugenini,” alisema Nyalandu aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Alimwambia Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia kuwa Watanzania wameiona nyota yake na wameguswa na kujawa na furaha na kupata matumaini juu yake kwa sababu Mungu alimuandaa kuja kuwa kiongozi wa taifa.

Alisema anaamini maneno ya Rais Samia yatawaponya Watanzania wote, kuwaunganisha na kuwaongezea tabasamu wananchi wote kwa misingi aliyoasisi Mwalimu Julius Nyerere ya umoja na mshikamano.

Naye Luwongo alisema ameamua kwa ridhaa yake kurudi nyumbani kwa sababu kadiri anavyoendelea kuwa nje ya chama hicho anajihisi kuwa ana mapungufu.

Mchezaji soka huyo wa zamani wa Tukuyu Stars, Yanga na Simba, alisema katika maisha ya siasa anaamini kuwa CCM ndicho chama pekee nchini kinachoweza kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania wote.

Luwongo aliyewahi kuwa Diwani wa Vijibweni wilayani Kigamboni kupitia CCM na mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Mtama mkoani Lindi, alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kufurahishwa na CCM kumchagua Rais Samia kuwa Mwenyekiti hivyo kumfanya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa katika chama.

Alimuahidi Mwenyekiti Rais Samia kuwa atamuunga mkono kwa nguvu zake zote na yuko tayari kuendeleza maendeleo yote yaliyoletwa na CCM.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/36faaabdf9a2b1410538401f74aec9ad.jpeg

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi