loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Madiwani Tanga wataka makusanyo 100% ifikapo Juni

BARAZA la Madiwani la Halimashauri ya Jiji la Tanga limeitaka Idara ya Fedha na Mipango kujiwekea malengo na mikakati ya kuhakikisha mpaka ifikapo mwezi Juni iwe imefikishia asilimia 100 ya makusanyo yake.

Agizo hilo limetolewa na Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Abdulrahman Shiloo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri hiyo na alisema kuwa mpaka sasa makusanyo yameweza kufikia asilimia 66 wakati kipindi kama hicho mwaka jana yalikuwa ni asilimia 75.

Meya huyo alitoa mapendekezo ambayo yatasaidia kufikisha lengo la makusanyo kwa wakati na  aliishauri idara hiyo kufanya vikao vya kamati ya fedha kwa wakati.

Aidha aliishauri  idara hiyo iwe na mpango kazi na kujifanyia tathimini ili kujipima kama wamefikia malengo na kufanyia kazi kwa haraka changamoto zinazokwanisha kufikia lengo la makusanyo.

Hata hivyo Meya Shiloo aliagiza  fedha zinazoletwa na serikali kwenye Halmashauri hiyo  kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali taarifa zake ziwekwe wazi na zieleze ni mradi gani unaokusudiwa kutekelezwa ili iwe rahisi pale wananchi watakapotaka kuhoji. 

“Serikali Kuu imekuwa ikituletea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwahiyo naagiza kiasi cha fedha kitakacholetwa aina ya mradi unataka kutekelezwa taarifa zote hizo ziwekwe wazi kwenye mbao za matangazo ili wananchi wajue serikali yao inawafanyia nini,” alisistiza Meya Shiloo. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo Daudi Mayeji  alilishauri baraza hilo kuona, namna ya kupitia upya maeneo ya mwambani ambayo yalimilikishwa kwa wananchi miaka ya 90 na kushindwa kuyaendeleza ili yarudi kwa halmashauri na kuyagawa kwa watu watakaoweza kuyaendeleza. 

Alisema tayari wameanza kupitia upya ramani ya eneo hilo ili kuona michoro na matumizi ya kila kiwanja yaliyoombwa ili kuleta mapendekezo hayo katika baraza na yakiridhiwa waweze kuweka utaratibu mpya katika eneo hilo lakini sio kubadilisha matumizi ya awali. 

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa aliwaasa madiwani kutoa elimu kwa wananchi wao ya umuhimu wa mipango miji ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima katika maeneo yao. 

Mwilapwa alisema lengo la serikali ni kupunguza migogoro na kuondoa uvamizi wa maeneo usio wa lazima unaofanywa na wananchi katika maeneo yao hivyo amewataka madiwani wasaidie serikali katika kuwaelimisha wananchi wao kufuata sheria na taratibu za umiliki wa ardhi. 

Diwani wa kata ya Tangasisi, Ahmed Mwinjanga alisema maeneo mengi ya kata yake yamekuwa na changamoto ya migogoro ya ardhi kutokana na maeneo mengi kutopimwa hivyo aliiomba Halmashauri kuona ipo haja ya kupima maeneo hayo ili kupunguza changamoto ya migogoro hiyo. 

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ...

foto
Mwandishi: Amina Omari, Tanga

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi