loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia asikia kilio cha wafanyakazi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wafanyakazi nchini kwa kufanyia kazi maombi mbalimbali yaliyowasilishwa kwake ikiwamo kushusha kiwango cha kodi inayotozwa kwenye mshahara (PAYE) na kuwahakikishia kwamba mwakani atapandisha mishahara.

Kutokana na hatua hiyo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limemshukuru na kusema amefanyia kazi maombi yao kwa asilimia 99 huku wakisema, asilimia iliyobaki ambayo ni mishahara, hawawezi kushindwa kuvumilia.

Akihutubia jijini Mwanza wakati wa kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyokuwa na Kauli Mbiu ‘Masilahi bora, Mishahara juu, Kazi iendelee’, Rais alisema mwakani atapandisha mishahara.

“Niwahakikishe mwakani siku kama ya leo (Mei Mosi) nakuja na package nzuri ya kupandisha mishahara ikiwamo kuongeza kima cha chini kwa umma na sekta binafsi na katika hilo naagiza kuundwa kwa Bodi za Mishahara 

kuanzia sasa ili mwakani niwe najua napandisha kwa kiasi gani . Naomba niwape pole kwa hili lakini niwapongeze kwa hili nililochukua hatua,” alisema Rais.

Katika kufafanua sababu za kutopandisha mishahara mwaka huu, Samia alisema, “Ndugu zangu mimi ni Mama na mama ni mlezi. Lakini kuna msemo wa Kiswahili unasema masikini hapendi mwana. Maanake hata kama unataka mwanao apendeze utaonekana humpendi kumbe kuna uwezo wa kumfanya apendeze.”

“Kama nilivyosema awali na hili ni la msingi la kweli, mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu. Binafsi natamani kuona mwaka huu ungeongezwa, lakini kutokana na sababu mbalimbali nimeshindwa kutimiza matamanio yenu mwaka huu.”

Alisema kutokana na corona, kasi ya ukuaji uchumi imeshuka duniani na Tanzania kutoka asilimia sita hadi nne. Alisema kutokana hatua anazotarajia kuzichukua ikiwamo kufuta kodi na tozo , mapato yatokanayo na kodi yatapungua kwa muda ingawa yatapanda baadaye. “Imekuwa vigumu kwangu na kwa sababu ndio nimeingia sijajipanga vizuri lakini nimejitahidi kuangalia mengine,” alisema.

Kuhusu maombi mengine aliyoyapatia ufumbuzi ambayo TUCTA imesema ametekeleza kwa asilimia 99, ni pamoja na kusikia ombi la wafanyakazi la kutaka kupunguziwa kodi inayotozwa katika mishahara(PAYE) kwa kuagiza ipungue kutoka asilimia kutoka asilimia tisa hadi nane.

“Serikali imesikia ombi la kutaka kupunguziwa PAYE na kutokatwa kodi katika malipo ya stahiki nyingine zisizo za mshahara. Tumeamua kupunguza asilimia moja. Itatoka asilimia tisa na sasa tutakatwa asilimia nane. Tutaendelea kulitazama suala la makato yasiyo ya mshahara,” alisema.

Jambo lingine ni ucheleweshaji mafao kwa wastaafu ambalo Rais alisema linamsikitisha hivyo aliwaambia wafanyakazi kwamba kuanzia mwezi huu, serikali itaanza kuyalipa kila mwezi mpaka yaishe.

“Tatizo lipo na binafsi linanisikitisha sana. Natamani mtu akistaafu alipwe mara moja badala ya kuzungushwa. Nimeeleza mifuko kuhakikisha wanalipa mafao ya wastaafu. Taarifa ya faraja, wafanyakazi waliorundikana tunaanza kulipa mafao yao kuanzia mwezi huu tutalipa kila mwezi mpaka mafao yaishe,” alisema.

Kwa upande wa madai na madeni ya watumishi, alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kulipa na kuwahakikishia kuwa serikali itaendelea kulipa madeni yote.

Alionya viongozi wa taasisi mbambali kwa kuzitaka kuacha kuzalisha madeni mbalimbali bila sababu za msingi. “Watumishi waache kutengeneza madeni hewa. Inabidi tufanye tathimini tupitie tuhakikishe ni ya kweli. Kuna taasisi iliwasilisha deni la shilingi bilioni 40 na baada ya kutathimini, deni halisi ni Sh bilioni moja. Hali hii inachelewesha madeni.”

Alisema kwa kutambua umuhimu wa wafanyakazi serikali itachukua hatua mbalimbali za kuboresha maslahi kwenye mwaka wa fedha ujao ikiwamo kupandisha vyeo watumishi 85,000 hadi 91,000 hatua itakayogharimu Sh bilioni 449.

Serikali italipa malimbikio ya mishahara yenye thamani ya Sh bilioni 60, itafanya mabadiliko ya muundo wa kiutumishi yatakayogharimu Sh bilioni 120 na pia kuajiri watumishi wapya 40,000 ili kuwapunguzia mzigo wafanyakazi hususani katika sekta ya afya na elimu hatua itakayogharimu Sh bilioni 239.

“Mwaka huu tunakusudia kupunguza viwango vya kodi za mishahara kwa watumishi, tutaendelea kupunguza mfumuko wa bei. Ni matumaini jitihada hizi zitasaidia kupunguza ukali wa maisha ya watumishi,” alisema na kusisitiza kuwa mwakani atakuja na fungu zuri kupandisha mishahara na kuongeza kima cha chini.

Kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu, Rais Samia alisema serikali imeanza mjadala na ulifanyika mwezi uliopita kuliangalia na mwisho matakwa yatimie.

“Kwenye mjadala niliwaambia viongozi mtoto akililia wembe mumpe. Bodi mmeililia na baada ya kuundwa mnarudi nyuma kuwa hamuitaki na sisi tunawasikiliza tutalifanyia kazi pamoja na kwamba inaundwa kisheria hatuwezi kuwa watumwa wa sheria,” alisema.

Rais aliwataka wafanyakazi kuendeleza uadilifu sehemu ya kazi huku akisisitiza kuwa anafahamu maslahi ni madogo lakini wakiwa waadilifu na kufanya kazi kwa kujituma, tija itaongezeka na serikali kupata uwezo wa kulipa maslahi.

WATU wa kada tofauti wameelezea panga pangua ya ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Mwanza

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi