loader
Majaliwa: Tutumie mwezi wa Ramadhan kuomba baraka

Majaliwa: Tutumie mwezi wa Ramadhan kuomba baraka

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasisiza Waislamu nchini watumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kumuomba Mungu aendelee kuibariki Tainzania, viongozi na wananchi wake wadumishe amani na mshikamano.

 Alitoa mwito huo jana katika fainali za mashindano ya 29 ya kimataifa ya kusoma Qur'an yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yalihusisha washiriki 15 kutoka nchi 11.

 Majaliwa pia alitoa rai kwa waumini wa dini ya Kiislamu waendelee kuyaishi mafundisho wanayoyapata katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan hata baada ya mfungo huo kumalizika.

"Natambua mchango mkubwa wa waumini katika kuienzi na kuitunza amani kwa kufuata miongozo ya viongozi wetu kupitia mafundisho ya Qur'an ambayo hututaka kuepuka kuivuruga amani," alisema.

 Waziri Mkuu alisema amani ni matokeo ya msingi imara iliyoachwa na waasisi wa taifa, hivyo Watanzania hawana budi kuienzi na kuilinda kwa faida ya nchi.

"Mwitikio mkubwa tunaouona kwenye mashindano haya ni kielelezo cha amani, umoja na mshikamano tulionao," alisema Majaliwa.

 Alisema ni vema vijana waliohifadhi Qur'an wakaendelezwa kitaaluma katika fani zingine za elimu kwani uwepo wao ni muhimu katika kujenga jamii bora yenye uadilifu.

 Alisema si jambo rahisi kumuona mtaalamu aliyehifadhi Qur'an akienda kinyume cha maadili ya taaluma yake kwa sababu Qur'an inatosha kumuwezesha awe muadilifu.

 Alitoa mwito kwa wadau waunge mkono juhudi za taasisi za kuhifadhisha Qur'an nchini katika kujenga taifa bora la vijana wenye maadili na kutoa wataalamu wa fani mbalimbali wenye hofu ya Mungu.

 Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Shehe Aboubakar Zuber aliwahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu kujenga utamaduni wa kuhifadhi Qur'an kwa kuwa ndiyo jambo muhimu kwao kwa sasa.

 Katika mashindano hayo, mshiriki kutoka Yemen, Mohammed Abdo Ahmed (22) alishinda nafasi ya kwanza katika upande wa kuhifadhi Qur'an na amepata zawadi ya dola za Marekani 5,000.

Mohammed Haruna Hassani (37) ameshika nafasi ya kwanza kwa upande wa kusoma Qur'an kwa njia ya Tajweed na kupewa zawadi ya Sh milioni mbili.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/734909920bddfbc6f157a3990f71606e.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi