loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukeketaji; hatari juu ya hatari  

NI kweli, zipo mila nyingi nzuri ambazo sisi kama Watanzania tunapaswa kuendelea kuzienzi kwa sababu zinatufaa. Lakini ziko za hovyo kama hii ya ukeketaji ambayo haina manufaa yoyote zaidi ya madhara.

Pamoja na ukweli huo, baadhi ya jamii zetu wakiwamo wakazi wa Tarime na wilaya za jirani mkoani Mara wameendelea kuzienzi.

Ukeketaji ambao pia unaitwa "tohara ya wanawake" kwa kufananishwa kitendo kinachohimizwa sana cha kutahiri wanaume, ni hatua ya kukata kwa makusudi sehemu za nje za viungo vya uzazi, hususan ‘klitori’ kwa sababu ambazoi si za kiafya.

Ukeketaji una madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu: Kwa kuanza na ya muda mfupi ni pamoja Kifo kutokana na kutoka damu nyingi na maumivu makali, Uharibifu mkubwa wa mfumo wa nje wa viungo vya uzazi na kuweza kupata maambukizi ya magonjwa kama ukimwi, pepopunda na kadhalika.

Madhara ya muda mrefu ni pamoja na maumivu makali ya muda mrefu, maambukizi – ikiwemo maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo, kupungua kwa raha ya kujamiiana na madhara ya kisaikolojia, kama vile msongo wa mawazo utokanao na maumivu

Madhara mengine ni kuongezeka kwa hatari za kujifungua kwa njia ya upasuaji, kuongezeka kwa vifo vya uzazi, uongezeka kwa hatari za vifo vya watoto wachanga, kuongezeka kwa hatari ya watoto kuzaliwa kabla ya muda, kutoka damu nyingi wakati na baada ya kujifungua, kuongezeka kwa hatari ya kuzaa watoto wenye uzito mdogo na

madhara zaidi kwenye njia ya mkojo kwa wagonjwa wenye fistula ambao walifanyiwa ukeketaji.

Hata hivyo, kuna nadharia zinazoonesha kwamba akina baba wenye wake waliokeketwa wanapokutana na wanawake wasiokeketwa hunogewa na kukimbia familia.

Lakini pamoja na madhara hiyo, Meneja wa Miradi wa Kituo cha Kupinga Ukatili wa Kijinsia cha Masanga kilichoko Tarime, Valerian Mgani anasema kwa kuenzi mila hiyo iliyojikita katika imani potofu, jamii iko tayari kuona hata uhai wa mtu unapotea bila kujali.

 

 

 

Mgani anatoa mfano wa binti mmoja ambaye sasa umri wa miaka 16, aliyenusurika kufa baada familia yake kumfanyia matambiko na kumtelekeza kwenye pori la Serengeti, mkoani Mara ili aliwe na wanyama wakali.

 

Anasema alifanyiwa hivyo baada ya kubainika alikuwa na ujauzito huku akiwa bado hajakeketwa, jambo ambalo jamii ya Kikuria inaaminishwa kwamba ni mkosi kwa familia na ukoo husika. Kwamba kama ataachwa hivi hivi baadhi ya mikosi ambayo familia itapata ni pamoja na kutokea vifo.

 

 

 

Mgani anasema wakati binti hiyo (jina linahifadhiwa) anategeshewa makusudi na wazazi wake kwa kushirikiana na ukoo ili aliwe na simba alikuwa na umri wa miaka 14.

 

 

 

Anasema katika kuepuka mkosi, wazee wa mila walimfanyia matambiko kabla hajapelekwa porini, katika mbuga ya Serengeti, kando ya mto na kuachwa hapo wakiamini angeliwa tu na simba.

 

 

 

“Tulimwokoa porini akiwa mjamzito, akajifungua mtoto wa kiume ambaye sasa ana umri wa miaka miwili na wala kwao hakuna vifo visivyoelekeweka ambavyo vimeshatokea mpaka sasa,” anasema Mgani.

 

Mgani anatoa simulizi hizo kwenye kituo cha Masanga wakati akizungumza na wawakilishi wa redio mbalimbali za kijamii, ambao walitembelea kituo hicho baada ya kushiriki warsha ya kujengewa uwezo wa kutafuta na kuchakata habari, zenye kuzuia ukatili kwa wanawake na watoto.

 

Warsha hiyo iliandaliwa na Shirika la Kusaidia Watoto Tanzania la C – Sema, likishirikiana na Mtandao wa Redio za Kijamii Tanzania (TADIO) kwa ufadhili wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

 

 

Mgani anasema walipigiwa simu na msamaria mwema, aliyewaeleza uwepo wa tukio hilo na mahali ambako binti huyo aliachwa na familia yake, ndipo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wilayani Tarime, walikwenda na kumpata akiwa katika hali ya kutojielewa.

 

 

 

“Inasadikiwa mtu anapofanyiwa matambiko kama alilofanyiwa, anapumbaa na ndiyo maana hubakia eneo aliloachwa mpaka anapokufa kwa kuliwa na wanyama pori… Hali hiyo imeendelea kumtoka taratibu kutokana na huduma anazofanyiwa ikiwamo ya maombi,” anasema Mgani.

 

 

 

Kwa sababu za kisheria na kulinda kesho yake na mtoto wake, kituo hakikutoa ruhusa kwa wanahabari kufanya mahojiano naye ingwa walimwona akiwa na mtoto wake kituoni hapo.

 

 

 

Akizungumzia kuhusu ujauzito aliokuwa nao binti huyo, Mgani anasema baada ya fahamu zake kurejea katika hali ya kawaida na kuweza kuhojiana na wataalamu wa afya ya akili kituoni hapo, binti aliwaeleza kuwa alibakwa.

 

 

 

“Bini anasema alibakwa akiwa anachunga mifungo ya nyumbani kwao,” anasema.

 

Mwanasheria wa Kituo cha Masanga, Dora Ringo anasema baadhi ya watu walioshiriki kumtupa porini binti hiyo, akiwamo mama yake mzazi binti walikamatwa na polisi siku hiyo.

 

 

 

Hata hivyo, anasema hawakuweza kuwafikisha mahakamani kwa sababu hawakuwa na ushahidi usiyoacha shaka kwamba walimpeleka kwenye pori hilo ili afe kwa kuliwa na wanyama.

 

 

 

Mwanasheria huyo anasema kituo kinafahamu umuhimu wa binti huyo pamoja na mtoto wake kuishi ndani ya familia yao na kwamba kwa muda wote huo, kimekuwa kikifanya mazungumzo na familia hiyo kwa lengo la kuifanya imkubali na kuishi naye lakini jitihada hizo hazijazaa matunda.

 

 

 

Anasema sharti lililotolewa na familia hiyo ili binti akubalike kwao ni kumkeketa, jambo ambapo ni kosa kwa mujibu wa sharia za nchi lakini pia binti hayupo tayari kukeketwa na hata kituo hicho hakipo tayari kwa hilo.

 

 

 

Sheria ya makosa ya kujamiiana (SOSPA) inaweka adhabu zifuatazo kwa mtu yeyote anayefanya na kupatikana na hatia ya ukeketaji nchiniTanzania:

 

 

 

Kifungo kisichopungua miaka Mitano na kisichozidi Miaka 15, faini isiyozidi Sh 300,000 au vyote viwili; faini na kifungo.

 

Mhalifu pia ataamriwa kulipa fidia kwa mwathiriwa wa uhalifu kwa kiasi kilichoamuliwa na mahakama.

 

 

 

Halikadhalika, mtu yeyote anayekiuka Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Mtoto ya 2009 atafungwa chini ya Kifungu cha 14 na atawajibika kulipa faini isiyozidi Sh milioni tano au kifungo cha muda usiyozidi miezi sita, au adhabu zote mbili kwa pamoja.

 

 

 

Kwa mujibu wa Ringo, ingawa kituo kinaendelea kushawishi jamii imkubali binti na mtoto wake ili arejee kuishi na jamii yake, kituo hicho kina mpango wa kumsomesha ili awe na ujuzi ambao baadaye utamwwezesha kumudu maisha ya kujitegemea na kulea mtoto wake.

 

 

 

Anasema akitimiza umri wa kujitegemea na akiwa na ujuzi, kituo kitamwezesha kuanza ukurasa mpya wa maisha kama ambavyo kimekuwa kikifanya kwa wengine ambao wamekataliwa na jamii zao na kukimbilia kwenye kituo hicho.

 

 

Uchunguzin unaonesha kwamba katika wilaya ya Tarime ipo dhana isiyosahihi kwamba mwamamke asiyekeketwa (msaghane) ni mkosi katika jamii, na kwamba akizaa mtoto wa kiume, hususan wa kwanza atakuwa akileta mikosi katika jamii na hawezi kufanikiwa.

 

Elimu inapaswa kutolewa katika jamii hii kwamba dhana hiyo ni udanganyifu mtupu kwa sababu katika jamii zisizokeketa hakuna mikosi yoyote na hata sasa kuna familia kadhaa miongoni mwa Wakurya hazikeketi mabinti zao na hakuna mikosi yoyote.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ina majukumu mbalimbali yakiwamo yanayohusiana na kukomesha unyanyasaji wa wanawake na wasichana Tanzania.

Ili kutekeleza hilo wizara imeweka bayana Mpango wa Taifa na Hatua za Kukomesha Unyanyasaji dhidi ya Wanawake na Watoto 2017–2022 na pia inayo mikakati yakukabiliana na matendo hatarishi, kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

 

Serikali inafanya kazi kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa na ya kitaifa ambayo hutekeleza hatua mbalimbali ikiwamo kampeni za uhamasishaji na semina za mafunzo katika jamii.

 

 

 

Maeneo mengi nchini tayari kuna makazi salama kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji

 

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Editha Majura

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi