loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wodi mpya zinavyokwenda kuleta ahueni kubwa Mbeya  

“JENGO hili tunalotumia kwa ajili ya kitengo cha wazazi lilijengwa mwaka 1950, yaani kabla ya uhuru. Tangu kipindi hicho hakuna upanuzi wowote wa majengo uliowahi kufanyika. Na kwa kipindi chote uwezo wa vitanda vya kulaza wagonjwa umekuwa ni watu 172 pekee, tena kwa kujibana sana.”

 Hayo ni maneno ya mshitili, yaani msimamizi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa wodi ya kisasa ya Mama na Mtoto katika kitengo cha wazazi cha Meta ambacho ni sehemu ya Hospitali ya Kanda ya Mbeya, Dk Johnson Kamala, alipozungumzia mradi huo unaolenga kuleta unafuu wa utoaji wa huduma za afya kwa wajawazito na watoto wanaozaliwa.

 Hospitali ya Kanda ya Mbeya tunayoizungumzia katika makala haya inahudumia mikoa saba iliyopo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe na Mbeya yenyewe.

 Ukubwa wa eneo linalohudumiwa na Hospitali hii ulifanya jengo la kitengo cha wazazi Meta kuzidiwa na kusababisha msongamano mkubwa kwenye wodi. Kuna wakati wajawazito walifikia hatua ya kulala watatu watatu katika kitanda kimoja huku wengine wakilazimika kulala chini.

 Kutokana na hali hiyo, Serikali ya awamu ya tano chini ya iliamua kutenga shilingi bilioni 9.2 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mpya ya kisasa kwenye kitengo hiki muhimu.

 Dk Kamala anasema wazo la kupanua wodi hiyo ya wazazi ililitolewa tangu mwaka 2012 ili kuongeza vitanda kwa ajili ya kukidhi mahitaji yaliyokuwa yameongezeka maradufu lakini halikufanyiwa kazi.

 “Tunashukuru ilipoingia awamu ya tano, wazo letu hilo likaweza kufanyiwa kazi kwa maana ya kupatiwa fedha za kutekeleza mradi huu ambao upo mbele yetu. Ni mradi wa jengo la ghorofa sita ambao unatekelezwa kupitia fedha zilizotolewa na serikali,” anasema na kuongeza kwamba mradi huo ulioanzia Mei Mosi 2019, ulitakiwa kukamilika Ijumaa iliyopita, April 30.

 “Lakini kuna kazi za ziada ambazo zimeongezeka ikiwemo eneo la ndani la kuunganisha jengo la zamani na jipya na pia kutengeneza miundombinu ya nje. Hivyo muda umeongezeka na hivyo sasa tunatarajia kumaliza mradi huu mwezi wa saba,” anasema.

 Fundi mkuu katika mradi huu unaotekelezwa kwa akaunti ya dharura ni Suma JKT na mshauri mwelekezi ni MCB ambacho ni kitengo kilichopo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), wakati Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ikiwa mwakilishi wa wizara husika, ikisimama kama mshitili.

 “Ni jengo la kisasa ambalo litakuwa likitoa huduma mbalimbali. Litakuwa na vyumba vinane vya madaktari ikilinganishwa na vyumba vinne tu vilivyopo kwenye jengo la zamani… Kutakuwa na vyumba vitatu vya upasuaji ikilinganishwa na viwili vilivyokuwepo zamani na hivyo vitaongezeka hadi kufikia vitano.

 “Kutakuwa na wodi ya kujifungulia yenye uwezo wa vitanda 11 na kutakuwa na ICU itakayokuwa na uwezo watu 10. Hilo ni ongezeko kubwa sana ikilinganishwa na miundombinu iliyopo hivi sasa,” anasema.

 Kwa upande wa vitanda kwenye wodi za kawaida anasema vitaweza kulaza wagonjwa 144 kwa wakati mmoja na pia kutakuwa na wodi za daraja la kwanza zitakazokuwa na uwezo wa vitanda 58 na kwamba vyumba viwili miongoni mwa hivyo vitakuwa ni vya kifamilia (family suit).

 “Kwa hiyo vitanda vyote kwa ujumla vitafikia 213 ikilinganishwa na 172 kwenye jengo la zamani. Hilo ni ongezeko kubwa la karibu asilimia 100. Ujenzi unaendelea vizuri kama mlivyoshuhudia,” anasema mshitili huyo.

 “Tunategemea ujenzi tutaukamilisha kwa wakati. Jumla ya fedha ni Shilingi  bilioni 9.2  na kwa sasa tumekwisha pokea shilingi bilioni 6.48 ambazo zimekwishatumika na tumeomba fedha nyingine takribani Shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya kukamilisha mradi huu na shughuli nyingine mbalimbali zinazoambatana na mradi huu ambazo tunaamini tutazipata pia na tunaomba serikali iendelee kutusaidia kama ilivyofanya huko nyuma,” anasema.

 Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila anasema ujenzi huo ni jambo la kihistoria kwa sababu toka hospitali hiyo ianzishwe mwaka 1950 haijawahi kuongezewa jengo kwa ajili ya kulaza wagonjwa, hali ambayo imekuwa ikisababisha msongamano mkubwa huku wagonjwa wengine wakilazimika kulala chini.

“Katika kuupa uzito mradi huu, utekelezaji wake unafanywa kwa utaratibu wa “Force Account” ambapo hospitali hununua vifaa vyote vya ujenzi na kuajiri fundi mkuu pamoja na mshauri elekezi ambao wanashirikiana pamoja na kamati mbalimbali zilizoundwa kwa ajili ya mradi,” anasema Chalamila.

 Anasema kasi ya ujenzi ni nzuri na kwamba tayari ujenzi umefanyika kwa zaidi ya asilimia themanini na matumaini yake ni kukamilika ndani ya muda.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji anasema kwa ujumla hospitali hiyo inahudumia watu wapatao milioni nane, wakiwemo wajawazito na watoto.

Anasema majukumu makuu ya hospitali hiyo ya kanda ni kutoa huduma za tiba na mafunzo kwa kushirikiana na vyuo vikuu nchini pamoja na kufanya tafiti.

“Hospitali yetu kwa ujumla inahudumia wagonjwa wa nje (wanaotibiwa na kuondoka) na wagonjwa wa ndani (wanaolazwa). Katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2020 hadi kufikia Februari mwaka huu wa 2021, hospitali ilikuwa imeshahudumia wagonjwa 225,548; wa nje wakiwa 194,345 na wagonjwa wa ndani 31,203. Kati ya wagonjwa hao, 20,467 walitibiwa kwa msamaha.

Dk Mbwanji anasema kupanuliwa kwa jengo la wodi ya mama na mtoto, si faraja kwa wagonjwa pekee wakiwemo wajawazito wanaokwenda kupata huduma za kirufaa wakitokea kwenye maeneo yao mbali, bali pia kunawapa hamasa watoa huduma kufanya kazi vizuri zaidi kutokana na mazingira kuboreshwa.

“Sisi tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya kazi. Lakini pia imeonesha namna inavyowajali wananchi kwa kuwajengea mazingira rafiki wanapokuja kufuata huduma za tiba. Tunayo imani kubwa kuwa upendo huu wa serikali kwetu na wananchi kwa ujumla ni endelevu. Na tuna imani kubwa kwamba kama ilivyokuwa wakati wa Magufuli pia mambo mazuri yataendelea kufanyika chini ya mama yetu, Rais Samia Suluhu Hassan,” Alisema Dk Mbwanji.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ni miongoni mwa wiongozi waliowahi kutembelea na kukagua mradi huo.

Alisema serikali kupitia mradi huo imejipambanua katika kuonesha mahaba yake kwa wananchi wa Mbeya mikoa ya jirabi kwa kuwaboreshea miundombinu mbalimbali kupitia miradi inayotekelezwa.

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi