loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rais Samia, Kenyatta wakubaliana mambo 11

RAIS  Samia Suluhu na mwenyeji wake Rais wa Kenya,Uhuru Kenyatta wameingia makubaliano 11 ikiwa pamoja na kusaini mkataba wa ujenzi wa Bomba la  Gesi kutoka Dar es Salaam mpaka Mombasa Kenya.

Marais hao kwa pamoja  wamesema wameingia makubaliano kuhusu ujenzi huo wa bomba la gesi baada ya majadiliano ya  muda mrefu.
Wamefikia tamati na kusaini mkataba tayari kwa ujenzi huo.

Mbali na ujenzi wa bomba la gesi makubaliano mengine yaliyofikiwa ni kudhibiti janga la Corona kwa kufuata taratibu za kimataifa za upimaji Covid 19  kwa haraka kwa wafanyabiashara mipakani, kuimarisha hali ya usalama na kupambana na ugaidi, kuimarisha masuala ya kijamii, utalii na  kitamaduni.

Aidha makubaliano mengine waliyoingia ni   kuimarisha masuala ya anga kwa pande zote mbili, kuondoa vikwazo vya kodi mipakani, kuimarisha masuala ya Kilimo, Uvuvi, Utalii na Viwanda.

Pia kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuhimiza nchi wanachama kulipa michango ya  uwanachama ili jumuiya hiyo iweze kusimama imara.

Akifafanua zaidi makubaliano hayo, Rais Samia   alisema “ Kenya ni ndugu zetu, ukiangalia katika nchi ambazo zimeizunguka Kenya,  mpaka wa Tanzania ndio umechukua eneo kubwa, watu wanaoishi mipakani wapo  Kenya na Tanzania  hivyo hawa ni ndugu zetu.

“Kwa uwekezaji  Kenya inashika nafasi ya tano Kiulimwengu kuwekeza Tanzania na inashika nafasi ya kwanza kwa Jumuia ya Afrika Mashariki, imewekeza miradi 513 inayofikia Dola Bilioni 1.7 , imetoa ajira kwa watanzania 51,000,” amesema Rais Samia

Aidha Kampuni za Tanzania zilizowekeza Kenya ni 30 ambazo zimewekeza mtaji ndani ya Kenya wenye thamani ya shilingi za Kenya Bilioni 19.330  na kutoa ajira 2, 640 .

“Nimemuhakikishia kaka yangu Rais Kenyatta, Tanzania sasa tutakuja kuwekeza kwa nguvu zote,ili kukuza ujazo wa biashara, ambayo kwa sasa wastani wa thamani ya biashara zetu ni shilingi za Kitanzania Trilioni 1, bado sio kubwa ila tumekubaliana kuikuza.” alisema

Pia alisema watatumia fursa za Kilimo, viwanda, uvuvi, na utalii  kukuza uchumi wa nchi zote mbili.

Kuhusu changamoto za vikwazo vya kodi alisema wamekubaliana kuviondoa na wameziagiza Tume za pande zote mbili za usuluhishi ziwe zinakaa na kutoa suluhu ya vikwazo vinavyotokea.

Amesema pia amekubaliana na suala la Mawazi wa Afya wa pande zote kukaa na kurahisisha mfumo wa kupimwa vipimo vya Covid 19 na watu wapewe huduma kwa haraka ili waweze kuvuka na kufanya biashara zao.

Aidha amesema miradi mingine ya kimkakati  ukiachilia mbali la nishati ya umeme na gesi ambayo wamesaini mkataba, mingine mazungumzo yanaendelea na pia amemualika Rais Uhuru Kenyatta kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, yanayoadhimishwa Desemba 9, kila mwaka.

Naye Rais Kenyatta akizungumzia makubaliano hayo alisisitiza kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Kenya na kuimarisha na kutekeleza yale yote ambayo wamekubaliana.

“Kenya tupo na furaha tele siku ya leo, uhusiano wa nchi zetu mbili utaendelea kuimarika, tutaendelea kufanya kazi hapa kwa hapa mpaka kukuza uchumi mwema kwa Wakenya na Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.” alisema Kenyatta.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi