loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali kukomesha rushwa michezoni

Serikali kukomesha rushwa michezoni

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama inaweka mazingira wezeshi ya michezo nchini na kukomesha vitendo vya rushwa.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa wizara hiyo, Innocent Bashungwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM) aliyetaka kujua kwa kiasi gani serikali inakabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyoonekana kukithiri katika mchezo wa soka nchini.

Bashungwa alisema wizara yake inapambana na vitendo vya rushwa kwenye michezo kwa nguvu zote na kwamba haitaivumilia timu au mtu yeyote atakayetumia rushwa kujipatia ushindi.

Awali, akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi alisema serikali inatambua kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika sekta ya michezo hususan mchezo wa soka hali inayoathiri maendeleo ya mchezo huo kwa ujumla lakini pia kuikosesha serikali mapato.

Alisema serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekuwa ikikabiliana na vitendo vya rushwa kwenye mchezo wa soka kwa kufanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya viingilio katika mechi za mpira wa miguu.

“Matokeo ya uchambuzi huo yaliwezesha kubaini na kuziba mianya ya rushwa kwenye eneo hili, ambapo mapato yaliongezeka hadi kufikia Sh milioni 206 kwa watu 50,233 waliokata tiketi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Machi 2019 ikilinganishwa na mapato ya Sh milioni 122 kwa watu 47,499 waliokata tiketi kwa mechi iliyochezwa Januari 2019 kwenye uwanja huo,” alisema.

Ndejembi alisema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya michezo nchini, mwaka 2016 Takukuru iliunda timu maalumu ya uchunguzi kufuatilia na kuchunguza vitendo vya rushwa katika michezo, ambapo kesi tatu zimefunguliwa mahakamani na tuhuma saba zinaendelea kuchunguzwa.

Alisema semina zimetolewa kwa makundi mbalimbali ikiwamo Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (Tafca), waamuzi na makamisaa wanaotumika katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza na kufanya vikao na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu kuweka mikakati ya pamoja kuelimisha umma kupitia soka ili kukomesha vitendo hivyo.

Ndejembi aliitaka TFF, wasimamizi wa soka na viwanja vya michezo kuruhusu na kushirikiana na Takukuru kuweka matangazo ya kukemea rushwa kwenye soka na michezo kwa ujumla.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/69ef7375035090ef4e4e66beee4a00fc.jpeg

YANGA leo saa 1:00 usiku itashuka dimbani kuikabili ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi