loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kodi ni kwa maendeleo yetu,  lakini fanyieni kazi haya

Kodi ni kwa maendeleo yetu, lakini fanyieni kazi haya

MWAKA 2007, mimi na rafiki yangu mmoja tulidhamiria kufungua biashara ya uchapishaji (printing). Tukachanga vijisenti vyetu kiduchu kutoka kwenye mishahara, kwani wote ni watumishi, tukaamini itatusaidia kuongeza kipato.

Tukashughulikia leseni, na kama ilivyo kawaida, hata kabla hatujaanza biashara tukakadiriwa mapato ya mwaka mzima na kuanza kulipa awamu ya kwanza ili tupate kile wanachoita Tax Clarence. Sijui Kiswahili chake.

Baadaye tulishughulikia leseni tukapata na kufungua biashara ambayo ilidumu kwa muda mfupi kutokana na tatizo la usimamizi. Kwa kweli, biashara nyingi zinakufa kutokana na usimamizi mbovu hasa pale mhusika au wahusika wa biashara wanapokabidhi majukumu hayo kwa watu wengine. 

Kwa hiyo katika biashara hiyo, walionufaika ni serikali kupitia kodi tuliolipa, halmashauri waliotupa leseni tuliolipia na wasimamizi tuliokuwa tunawalipa ndani ya miezi mitano ya uhai wa biashara hiyo. Sisi tuliotoa mitaji, tukaishia kumshukuru Mungu!

Kwa vile sisi Waafrika tuna tatizo kubwa la kutunza akiba, mimi na wenzangu kudhaa tulianza mchezo wa kupeana pesa kila mwisho wa mwezi. Michezo hii inasaidia sana kupata angalau akiba. Kutokana na michezo hii, nikaaamua kuanzisha biashara nyingine baada ya kujihakikishia kwamba hakutakuwa na tatizo la usimamizi.

Katika kupata maoni ya wafanyabiashara wengine, nikaanza kutishika waliponiambia kwamba kama nilifungua biashara mwaka 2007 na sijawahi kuandika barua Mamlaka ya Mapato (TRA) kwamba biashara ile ilishindikana, basi nikinusa tu pua yangu TRA ni naanza kukadiriwa mapato tangu mwaka huo ambayo sijalipia. Habari kwamba biashara ilishakufa siku nyingi wala hawatambui hilo.

“Duh! Tangu 2007 mpaka leo nakwambia ukienda TRA, utakuwa unadaiwa mlima wa pesa. Heri utumie TIN namba (namba ya mlipa kodi) ya mkeo au kama nayo ina tatizo ni heri ufungue mpya hata kwa jina la mwanao,” akanishauri mmoja wa wafanyabiashara, anayefanya biashara kama ninayotaka kufungua. Si huyo tu, wengi niliowaambia ninachotaka kufanya walinitisha hivyo hivyo!

Maelezo hayo yalinitisha nikafikiria kuacha kufungua biashara baada ya kukumbuka kwamba mke wangu pia aliwahi kufungua ofisi ya uhazili na vifaa vya maofisini (stationery) lakini nayo alishafunga ingawa yenyewe ilidumu miaka kadhaa. Kwamba kumbe naye akinusa pua yake TRA atapigiwa mahesabu ya mamilioni anayodaiwa!

Huku nikiwa nimepata mawazo ya kuachana na biashara, rafiki yangu mmoja alinishauri kwanza niende nikajiridhishe kuhusu hadhi ya TIN yangu. Nikaamua kwenda kwenye ofisi za TRA ambapo iligundulika kwamba TIN namba yangu haina deni la kutisha. Nikamshukuru Mungu huku nikijiuliza  ni wangapi wameshindwa kuanzisha biashara kutokana na hofu kama niliyokuwa nayo? Ni wangapi sasa wanafabyabiashara bila leseni kwa hofu ya kupigiwa mahesabu ya nyuma kwa sababu biashara zao za awali zilipokufa hawakuandika barua kuieleza TRA kuhusu hilo? Maswali ni mengi.

Hatua hiyo ilinifanya sasa nianze kushughulikia biashara kifua mbele. Lakini nilipokwenda ofisi za TRA pale Mbagala Ijumaa ya Aprili 23, nikakadiriwa mapato ya mwaka mzima na kutakiwa kulipa kwa awamu nne.

Hilo la kulipa kwa awamu si baya lakini kilichonishitua ni kutakiwa kulipa hata awamu ya Januari hadi Machi, muda ambao hata nilikuwa sijapata wazo la kufanya biashara!

Nikawa ninajiuliza kwamba hii si kodi ya dhuluma ambayo Rais wetu Samia Sulu Hassan amesema kwa kinywa kipana kwamba ‘hapana?’

Nilipomrudia ofisa aliyenikadiria kunipa ufafanuzi sikumkuta kwenye dawati lake lakini ofisa mwenziye akaniambia: “Kimsingi makadirio hufanywa kwa mwaka mzima. Hata ukija mwezi wa 12 (Desemba), sisi tutakufanyia makadirio ya mwaka mzima na utalipa mwaka mzima. Isipokuwa ofisa mkadiriaji atakupunguzia tu viwango kiutu tu. Yaani kama ulipaswa kulipa shilingi laki nane kwa mwaka, kwa mfano, anaweza kukudiria laki tatu.”

Nilipotoka pale, nikaenda kulipa. Lakini ofisa aliyeniandikia ile Tax Clarence akaniambia hii biashara unayotaka kuanza, lazima uwe na mashine ya kielektroniki (EFD). Nilipomuuliza bei ya hizo mashine akaniambia mashine ya bei ya chini kabisa ni Sh 500,000. 

Maelezo hayo yakanifanya nigundue kwamba kumbe biashara siwezi kuanza hadi nijichange tena kama mishahara mitatu ndio nipate pesa ya kununua hiyo mashine na kuanza biashara, ingawa tayari kodi nimeshalipa!

Aliponiona nimechanganyikiwa akaniambia: “Lakini unaweza kuandika barua kwa meneja ili akukubalie kutumia risiti za kawaida wakati unajipanga kununua EFD.”

Ingawa maneno hayo yalinipa ahueni kidogo lakini nilipomuuliza asilimia za kukubaliwa kutumia risiti za kawaida akasema ni asilimia hamsini kwa hamasini. Sasa ninajiandaa kuandika hiyo barua kwa meneja huku nikiwa sina hakika kama nitakuwa kwenye zile asilimia 50 za kubaliwa na sijui kama miezi minne nitakayoomba ya kutumia risti za kawaida nitakubaliwa.

Kimsingi, nimegundua kwamba Watanzania wengi wanapenda kuendesha biashara zao kwa uwazi na wakiwa na leseni pamoja na kulipa kodi. Katika miaka ya karibuni, Watanzania wameona namna kodi zao zilivyokuwa zinafanya kazi na hivyo wako tayari kulipa.

 

Lakini wakati mwingine, ukubwa wa kodi na mambo kama hayo ya kupigiwa mahesabu ya nyuma yanawafanya washindwe kuanzisha biashara mpya au kutafuta mbinu za kukwepa kodi.

Nina hakika Watanzania wengi, kama nilivyo mimi, hawana elimu kuhusu kuandika barua haraka pale biashara zao zinapoanguka ili wasiendelee kukadiriwa kodi baada ya biashara kufa. 

Hili naamini linahitaji elimu ya mara kwa mara labda kama tunaishi kwa kuviziana kwamba ‘ sisi TRA tutatumia kutoolewa kwako kukupigia mahesabu ya nyuma siku ukija kwetu kuanza biashara nyingine’. 

Kama TRA haiko pale kumkomoa mtu, ni vyema kila siku wawe wakiwakumbusha wale ambao biashara zimeanguka waandike barua ili wasiendelee kuonekana wanafanyabiashara. 

Ninashauri maofisa wa TRA wangekuwa pia wanatembelea eneo la biashara na kulitambua wakati mtu anapokuwa anaanzisha biashara mpya na kuendelea kulitambelea ili siku akijisahau kuandika barua, kama biashara imeanguka wawe wanajua kwamba fulani alishaanguka kibiashara. Au kwa vile wanabaki na mawasiliano yake ni vyema pia wakawa wanayatumia kuwakumbusha au kuwaeleza kama biashara imeshakufa watoe taarifa.

Halafu mtu aliyejisahau kuandika barua asikilizwe kama atasema biashara ilishakufa siku nyingi. Kama haaminiki basi maofisa wa kodi waende eneo kulikokuwa na biashara na kufanya uchunguzi, kukutana na watendaji, wajumbe wa nyumba 10 na wananchi kwa ujumla badala ya kuamini kinachoonekana kwenye makaratasi. 

Kwenye makadirio ya kodi ni vyema TRA ibadilike pia. Mtu akadiriwe kwa kiwango cha mwaka kilichobaki na kama ni mwaka mzima, basi uanzie pale alipokadiriwa. 

Bado sijajua mantiki ya kufuata mwaka wa kalenda badala ya mwaka kuhesabiwa tangu mfanyabiashara anapokadiriwa mapato. Yaani kama ni mwezi Aprili basi makadirio yake yawe hadi Aprili ya mwaka ujao na siyo kuishia Desemba ya mwaka husika. Hii huwezi kukwepa kusema ni kodi ya dhuluma.

Tukija kweye mashine za kielektroniki, inasemekana kuna tatizo kubwa fulanio kwenye mashine hizo kwa maelezo kwamba kuna wakati hazifanyi kazi au kukosa mtandao.

Katika hili kuna uwezekano kuwa ni kweli hizi mashine huwa zinakuwa na tatizo la mtandao na pili kuna uwezekano pia wafanyabiashara huwa na tabia ya udanganyifu hivyo kusingizia mashine ili wasilipe kodi halali. Ni vyema serikali ikalifanyia kazi hilo kwa kutafuta mashine zingine na bora zaidi ili zitumike kwa wafanyabiashara. 

Kama alivyowahi kujadili mtu mmoja kwenye mitandao ya kijamii, mashine hizo mpya ziwe na uwezo wa kufanya kazi hata kwa kuwekewa betri au mfumo mbadala wa nishati pale ambapo umeme hautakuwepo. 

Ni vyema pia mashine hizo ziwe na mfumo wa kutumia mitandao yetu ya ndani kwa ajili ya kupata mtandao na kuhakikisha mtandao unapatikana muda wote. Ziwe zinatumia hata laini za simu za mitandao ya ndani kwa ajili ya kupata mtandao.

 

Inashauriwa ikiwezekana mashine hizi ziunganishwe na mifumo ya mobile money ili kuongeza kiwango cha kodi kinachokusanywa hasa kwa wafanyabiashara ambao wanatumia mfumo wa mobile money kama njia yao ya kupokea malipo. 

Lakini kubwa zaidi, ni serikali kuhakikisha mfanyabiashara hanunui mashine hizi kwa bei kubwa. Ni vyema serikali ikawa na utaratibu wa kuzinunua yenyewe huku wafanyabiashara wakizilipia taratibu katika kipindi fulani na kwa bei ya nafuu kwa maana kwamba serikali iweke ruzuku na kama zinaingizwa kwa kodi basi iondolewe.

Nimalizie kwa kukukasilimia uliyesoma makala haya kwa jina la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Na jibu lako liwe: kazi iendelee ikiwa ni pamoja na TRA kufanyia kazi malalamiko ya wananchi nikiwemo mimi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ec355343aa59b35ca0f11c01bfb629a6.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi