loader
Dstv Habarileo  Mobile
Utafiti waibua walioathirika  zaidi na corona mwaka jana

Utafiti waibua walioathirika zaidi na corona mwaka jana

“MTU niliyefanya naye mahojiano alikuwa anafanya kazi kwenye hoteli moja ambayo wageni wake wengi siyo wakazi wa kisiwani Mafya. Ni msichana tu bado lakini ana watoto wawili anaowalea mwenyewe. Baada ya corona kuingia nchini (mwaka jana), hoteli aliyokuwa akifanya kazi iliyumba, akawa miongoni kwa walioachishwa kazi.

“Aliniambia kwamba alijikuta ana hali mbaya sana kiuchumi katika kulea wanawae. Akaawa anashindwa kula milo mitatu kwa siku bali mmoja tu, yeye na wanawe. Mwanae mmoja ambaye alikuwa anamsomesha kwenye shule ya kulipia amesimamishwa shule. 

“Shughuli anayofanya kwa sasa angalau kumudu huo mlo mmoja kwa siku yeye na wanawe ni kufuma makuti ya kuezekea nyumba ambapo kuti moja, anapotokea mteja, analiuza kwa shilingi 300.”

Huo ni moja ya ushuhuda uliotolewa kwenye warsha ya siku moja na Zuwena Nyundo, mmoja watu walioshiriki kufanya utafiti kuhusu madhara ya korona kimapato na kuangalia kama kuna hatua zilizochukuliwa na serikali na wadau wengine katika kusaidia kipato kwa waathirika wa corona kimapato, hususani vijana. 

 

Matokeo ya utafiti huo na ushauri unaotolewa kwa wadau na serikali yaliwekwa hadharani wiki iliyopita kwenye warsha hiyo ya vsiku moja jijini Dodoma.

Utafiti huo ulifanywa na Shirika la Actionaid Tanzania mwezi Machi mwaka huu kupitia mradi wa kuwezesha vijana wa Youth Empowerment and Influence in Tanzania (YEI) ukilenga kuangalia machapisho mbalimbali na mahojiano na vijana katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mkoa wa Pwani.

Ingawa kuna vijana wachache wabunifu walionufaika na corona, lakini masimulizi mengi kutoka kwa watu waliokwenda kuzungumza na vijana ambao pia walitoa ushuhuda wakati wa kuwasilisha matokeo ya utafiti, yanaonesha kwamba vijana wengi na akina mama waliathirika vilivyo kimapato na corona huku serikali ikiwa haina mkakati wowote wa kuwasaidia.

Kwamba kuna walioanguka mitaji tangu mwaka jana na hadi sasa wamekuwa tegemezi na kwamba endapo kungekuwa na sera maalumu za kuwasaidia, wangenyanyuka haraka na kuendelea kutoa mchango wao kwa taifa, hasa kwa kuzingatia kwamba zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni vijana.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Neema Ole Ndemno kutoka Taasisi ya Haki za Binadamu ya Afrika Mashariki (East African Human Rights Institute- EAHRI), anasema waliangalia sera na sheria na kugundua kwamba sera nyingi za Tanzania hazijielekezi katika kutatua matatizo ya vijana na wanawake kimapato wakati wa majanga.

Kwa nini vijana?

“Tunataja haya makundi, yaani vijana na wanawake, kwa sababu ndio makundi yaliyoathirika sana na corona. Sekta isiyo rasmi kama machinga, mama lishe na hata kilimo, wengi walioko huko ni vijana na wanawake. Na hapa tunazungumzia ile corona ya kwanza, yaani iliyopiga mwaka jana kati ya Machi hadi Juni hivi,” anasema.

Anaongeza kwamba utafiti wao ulioegemea kwenye kusikiliza zaidi masimulizi (case stories) na machapisho, si wa kisayansi kwa asilimi 100 lakini unasaidia kutoa picha halisi ya hali ilivyokuwa.

Neema anasema, mbali na sekta isiyo rasmi, sekta zingine  zilizoathirika zaidi ni za utalii, viwanda, sekta zinazotegemea uwekezaji kutoka nje, sekta ya usafirishaji wa bidhaa nje na sekta ya usafiri kwa ujumla, hususani usafiri wa anga na wa maji.

Anasema watu walioathirika kwenye sekta rasmi walijaribu kukimbilia kwenye sekta isiyo rasmi ambako pia walikuta mambo si mazuri.

Anasema maeneo ya utalii kama Zanzibar na Arusha yaliathirika sana na kwamba hata kama Tanzania haikufungia watu ndani moja kwa moja kama nchi zingine lakini athari za corona, hasa ile ya kwanza zipo katika kila eneo ingawa wao wameiangalia zaidi kwenye kipato cha vijana.

Mapitio ya sera na sheria

Ndemno anafafanua kwamba utafiti ulianza kwa kuangalia sheria, sera na miongozo mbalimbali iliyopo Tanzania kuhusu vijana na majanga na kwamba ingawa hazijielekezi moja kwa katika kusaidia vipato vya vijana wakati wa majanga, utafiti pia unaonesha kwamba hakuna sheria wala sera ambayo iliandaliwa au kurekebishwa baada ya kuibuka kwa janga la corona ili kuendeana na hali hiyo.

Sheria ya majanga 

Ndemno anasema Sheria ya Majanga ilitumika wakati wa janga la corona lakini ilijielekeza zaidi kwenye kupambana na ugonjwa wenyewe kwa maana ya matibabu, vipimo, na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo lakini haikujielekeza kwenye athari za vipato kwa waathirika.

Baadhi ya wachangiaji wanasema kinachoonekana ni kwamba Mfuko wa Majanga ambao uko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, umekuwa ukisaidia wanaoathirika na majanga kama ya mafuriko kwa maana ya kupewa chakula, malazi, dawa na hata vitendea kazi lakini kwenye corona haukuona kwamba kuna watu waliohitaji misaada ya kifedha na hata chakula ingawa hakukuwa na kufungiana ndani (total lockdown).

 

Mchangiaji mmoja alisema: “Ingawa serikali haikutamka kufungia watu ndani, lakini ukweli ni kwamba kuna watu walijifungia kwa hofu. Tuliona hata wabunge, hususani wa upinzani wakitoka bungeni na kujifungia ndani. Tulisikia pia habari za watu kufanya kazi wakitokea nyumbani. Shule zilifungwa na zile za binafsi bila shaka ziliathirika sana.”

Kusaidia wenye shida

Kwa mujibu wa Neema, Tanzania haikuwa na sera maalumu ya kusaidia waathirika wa corona (stimuli package) kwa suala la kipato wakiwemo wale ambao wajikuta hawana chakula.

Lakini anasema ziko nchi kama Rwanda, Kenya na Uganda ambazo zililalizimika kutoa aina fulani ya ahueni ikiwemo chakula kwa waathirika wa kipato kutokana na corona.

Anaamini kwamba Tanzania ilichukulika kwamba kwa kuwa hakukuwa na hatua ya watu kufungiwa ndani,  hivyo hakukuwa na haja ya kutoa chochote lakini utafiti unaonesha wapo watu ambao walihitaji msaada wa kifedha au chakula.

Je, ni ushauri gani unatolewa kwa serikali na watafiti pamoja na washiriki wa warsha kuhusu ripoti hiyo? Tutaangalia katika makala zijazo. 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1556ca05504c587025af00728d30522a.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi