loader
Dstv Habarileo  Mobile
Makocha Simba, Yanga  watunishiana misuli

Makocha Simba, Yanga watunishiana misuli

KOCHA wa Simba, Didier Gomes na wa Yanga, Nassredden Nabi kila mmoja ametamba kuibuka na ushindi katika mechi itakayozikutanisha timu zao kesho.

Miamba hiyo ya soka nchini itakutaka kuanzia saa 11:00  jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi inayosubiriwa kwa hamu na wengi kwani itatoa picha halisi ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha wa Simba, Gomes alisema jana kuwa, kikosi chake ni lazima kiibuke na ushindi kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya, lakini pia ubora wa wachezaji wake.

Hata hivyo, alisema pambano hilo litakuwa mgumu, lakini kutokana na mbinu alizowapa wachezaji wake mazoezini, ana amini watapata matokeo ambayo yatazidi kuwaweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.

“Ni mchezo mgumu kucheza na mpinzani wako kwenye ligi siyo jambo dogo lolote linaweza kutokea sababu tunakutana na timu yenye malengo kama yetu ya kutwaa ubingwa, lakini najivunia ubora wa wachezaji wangu na maandalizi tuliyofanya na kiwango tulichonacho hivi sasa hasa ikizingatiwa tumepata uzoefu mkubwa kupitia mechi za kimataifa,” alisema Gomes.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema amepanga kuitumia Yanga kama mazoezi kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika  dhidi ya  Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Gomes alisema amewafuatilia Yanga kwenye mechi mbili walizocheza hivi karibuni ikiwamo dhidi ya Tanzania Prisons na amepata mbinu za kuwadhibiti ingawa anatarajia watabadilika zaidi kutokana na kuwa chini ya kocha mpya Nabi ambaye ameiongoza timu hiyo kwenye mechi mbili tu mpaka sasa.

Alisema mpaka sasa jeshi lake lote lipo sawa kuelekea mchezo huo na wachezaji wamemwonesha matumaini makubwa ya kupata pointi zote tatu mbele ya Yanga ambayo imepoteza michezo miwili kama walivyo wao.

Gomes alisema ingawa yeye ni mara yake ya kwanza kukutana na Yanga akiwa kocha wa Simba, tayari ameona presha ilivyokuwa juu kwa mashabiki, wachezaji na hata baadhi ya viongozi  hivyo amepanga kuhakikisha anawapa furaha na yeye kuingia kwenye rekodi ya kuifunga Yanga.

Naye kocha wa Yanga, Nabi alisema pamoja na kuwa na muda mfupi tangu akabidhiwe timu hiyo, hatakubali kupoteza mchezo huo kutokana na ufundi aliowapa wachezaji wake tangu kumalizika kwa mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons.

Kocha huyo raia wa Tunisia,  alisema kuelekea mchezo huo haoni sababu ya kuweka presha juu isipokuwa cha msingi ambacho anakifanya ni kuwapa wachezaji wake mbinu mbadala zitakazowasaidia kuibuka na ushindi.

Alisema ameshakutana na Simba mara mbili (kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa Al Merrikh ya Sudan) na amewaona wakicheza mechi mbalimbali za ligi pamoja na michuano ya kimataifa, hivyo amewasoma vizuri mbinu na mifumo wanayotumia na tayari amewaandaa watu maalumu wa kuwadhibiti wachezaji wao hatari akiwemo Luis Miquissone na Cletous Chama.

“Hakuna ubishi kwamba tunakwenda kucheza na timu bora kwenye ligi ya Tanzania, timu ambayo inaongoza ligi, lakini wajue kwamba Yanga ni timu kubwa na inahistoria yake kwenye soka la Tanzania, ninachofanya ni kuwapa mbinu ambazo zitawaweka katika wakati mgumu wapinzani wakati huo huo tukitengeneza mashambulizi ambayo yatakuwa na madhara makubwa kwao,” alisema Nabi.

Kocha huyo alisema anatambua kwamba endapo watapoteza mchezo huo watakuwa wametoa nafasi kubwa kwa wapinzani wao Simba kutwaa ubingwa, hivyo kwa mbinu alizopanga kuzitumia anaamini watapata ushindi na wachezaji wake wamempa matumaini makubwa ya kushinda mchezo huo kutokana na kushika haraka kile anacho waelekeza mazoezini.

Naye Selemani Nzaro anaripoti kuwa, Jeshi Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama katika mtanange huo wa watani wa jadi utakaopigwa kesho Jumamosi saa 11:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kwa waandishi wa habari, ilisema jeshi hilo limepanga kuimarisha ulinzi kwa kuweka askari wa kutosha katika maeneo yote yanayozunguka uwanja wa Mkapa na barabara zinazoingia na kutoka uwanjani hapo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c24352ca0188db635c7ba8b5235f0b56.jpeg

YANGA leo saa 1:00 usiku itashuka dimbani kuikabili ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi