loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yataka maandalizi mapema Olimpiki

Serikali yataka maandalizi mapema Olimpiki

SERIKALI imeielekeza Kamati ya Maandalizi ya Olimpiki kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya michezo ya Olimpiki, michezo ya Afrika na Jumuiya ya Madola ili nchi ikafanye vizuri kwenye mashindano hayo.

Akizungumza baada ya kikao na kamati ya Olimpiki jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi alisema inatakiwa kuwe na mikakati mbalimbali itakayofanikisha ushiriki na ushindi wa nchi.

"Maandalizi yakianza mapema yanatoa nafasi kwa nchi kujiandaa vyema na mashindano na niwasisitize anzeni sasa," alisema Dk Abbasi.

Mashindano ya Olimpiki yatafanyika Agosti, mwaka huu Tokyo, Japan, Michezo ya Jumuiya ya Madola itafanyika Agosti, mwakani Uingereza na Michezo ya Afrika itafanyika 2023 nchini Ghana.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Dk Yusuph Singo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha.

Wakati huo huo, Dk Abbasi amezitaka kampuni za ubashiri wa michezo kuwa sehemu ya kuinua na kukuza michezo nchini na kuchangia maendeleo ya timu za taifa.

“Lengo la serikali ni kuwekeza kimkakati kwenye michezo, tuwe na mpango wa moja kwa moja wa kuzisaidia timu zetu za taifa kifedha, mimi naamini tukishirikiana kwa karibu tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya michezo,” alisema Dk Abbasi.

Alisema changamoto zilizopo katika kampuni hizo zitatafutiwa ufumbuzi kupitia vikao na njia mbalimbali baina ya serikali na kampuni hizo, ambapo alisisitiza ushirikiano kwa pande hizo mbili katika kusaidia nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Ubashiri wa Michezo Tanzania (TSBA), Jimmy Kenneth aliiomba serikali kutatua baadhi ya changamoto ikiwamo uwapo wa kampuni za ubashiri ambazo hazina usajili nchini zinazoisababishia nchi kukosa mapato na Dk Abbasi aliahidi kufanyia kazi.

Naye Mwakilishi wa Biko Sports, Goodhope Heaven alimshukuru Dk Abbasi kwa kukutana nao na kwa namna alivyoonesha moyo wa kusaidia sekta ya michezo nchini na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zao.

Wadau hao wameonesha utayari wa kuzisaidia timu za taifa, huku wakiiomba serikali kuweka msisitizo wa mazingira rafiki ya ulipaji kodi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/547b678277e8ea10cbf0b03103d4da7d.jpeg

YANGA leo saa 1:00 usiku itashuka dimbani kuikabili ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi