loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hili la ujali mbaya   jamii ijifunze

Hili la ujali mbaya  jamii ijifunze

SIO mara ya kwanza kwa wataalamu wa afya kusisitiza jamii juu ya kuzingatia ulaji bora na wenye afya kwa mustakabali wa afya ya mwili wa binadamu.

Mara nyingi wataalamu hao wakiwemo wa lishe wa ndani na hata nje ya nchi wamekuwa wakielimisha jamii kwa njia mbalimbali kuhusu mlo bora uliokamilika, lakini wengi wetu hatuzingatii wala kuona umuhimu wake.

Juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi alitoa tahadhari kwa umma juu ya ulaji mbaya kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na sikukuu nyingine za mwisho wa mwaka.

Amesema katika kipindi hiki kumekuwa na ongezeko la tatizo la mshtuko wa moyo kwa sababu ya kula chakula kingi na wakati mwingine mtu hula hadi kuvimbiwa.

Katika ushauri wake, Profesa Janabi ameshauri watu kula mlo kamili na wenye mchanganyiko wa makundi yote ya chakula, yaani protini zaidi, wanga kiasi, mafuta kiasi, mboga za majani za kutosha na matunda.

Amesema hayo kwa sababu matatizo mengi ya mshtuko wa moyo yanatokana na ulaji mbaya wa vyakula hasa kwa kula vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi, mafuta na kutofanya mazoezi.

Hayo ni baadhi tu ya matatizo ya ulaji mbaya na kusisitiza ulaji mzuri unaozingatia makundi tajwa ya vyakula. 

Tukirudi kwenye familia zetu, tumejenga mazoea ya kula zaidi vyakula vya wanga na mafuta mengi, huku tukishindilia sukari na chumvi tena ile mbichi ya kuongezea mezani jambo ambalo linahatarisha afya zetu.

Wataalamu wa afya wanatusisitiza siku zote jinsi ya kula mlo kamili kuwa ni ule wenye protini zaidi na vyakula vya protini ni pamoja na samaki, dagaa, maharagwe, nyama, kuku, mayai, maziwa na vitu vingine vya aina hiyo.

Kundi la wanga ni pamoja na wali, ugali, mihogo, tambi, chapati na vingine vya aina hiyo. Kundi jingine ni ulaji wa vyakula vyenye mafuta kwa wingi ambavyo ni pamoja na ulaji wa nyama zenye mafuta, siagi na vingine vya aina hiyo.

Kwenye ulaji wa vyakula vya mafuta, jamii inashauriwa kutumia zaidi mafuta ya mimea kama ya alizeti, ufuta, mawese na mengine ya aina hiyo kwa sababu hayana tabia ya kuganda mwilini na kuleta shida kiafya.

Ulaji wa mafuta ya wanyama kwa wingi huganda kwenye mishipa ya damu na kuufanya mwili kuwa na lehemu nyingi ambayo ina madhara na kusababisha matatizo ya mshtuko wa moyo, magonjwa ya moyo na mengine hatari.

Ulaji wa vyakula vya wanga kwa wingi na vyakula vyenye sukari nyingi vinaongeza kiwango cha sukari kwenye damu zaidi ya kiwango ambacho mwili wako unaweza kuhimili.

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), limesema vyakula vyote vya jamii ya kunde ni nafuu na vitamu vikiwa na kiwango kikubwa cha protini na hivyo vinaweza kutumiwa badala ya nyama .

Hivyo, jamii ibadilike katika uandaaji wa chakula cha kila siku, tujenge tabia ya kupika mboga za majani nyingi na protini zaidi, huku ulaji wa vyakula vya wanga ukiwa mdogo.

Mfano halisi na rahisi ni huu wa chakula rahisi lakini chenye afya, songa ugali wa dona au hata wa sembe kidogo, pika mboga za majani nyingi, maharage ya kutosha, uwe na matunda ya msimu na maji ya kunywa.

Chakula hicho ni rahisi na iwapo utakula hivyo umekula makundi yote muhimu ya vyakula.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5625669ef1078a949d6217830e53ff77.png

LIGI Kuu ya Tanzania inaelekea ukingoni ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi