loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Mwigulu ataka tija sekta ya mifugo

Dk Mwigulu ataka tija sekta ya mifugo

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kusimamia kikamilifu sekta ya mifugo kwa kubuni njia mbali mbali zitakazoongeza tija katika sekta hiyo.

Dk Mwigulu ametoa ushauri huo Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa wizara hiyo ya Mifugo na Uvuvi pamoja na ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo ili iongeze mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

“Tutakavyoweka mipango ya kisasa ya kukuza uzalishaji katika eneo hili la mifugo, tutatengeza wigo mkubwa wa walipakodi, tutabadilisha maisha ya watu wetu, tutakuza uchumi na ajira,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema maendeleo ya sekta ya viwanda yanayokwenda kwa kasi nchini yanahitaji malighafi za kulisha viwanda hivyo na kwamba fursa zilizopo kwenye sekta ya mifugo ni kubwa na kushauri mbinu za kisasa za kuendeleza ufugaji ziwekwe bayana na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Alisema utaratibu wa sasa wa wafugaji kuhamahama na mifugo kutafuta malisho na maji umepitwa na wakati na kuahidi kuwa wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alimshukuru Dk Mwigulu kwa kukutana nao na kuahidi kuwa ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi kikamilifu, ambako ameunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuchambua mapendekezo mbali mbali yaliyotolewa katika kikao hicho alichosema kilikuwa ni cha muhimu.

“Tutaangalia namna ya kupanua na kuwa na  maeneo maalum ya malisho ya mifugo yetu pamoja na kuboresha ufugaji ili ubadilike kutoka ufugaji wa kiasili kwenda ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija,” alifafanua Ndaki.

Alisema wafugaji watakaokuwa tayari kubadilisha namna ya ufugaji wao watapelekwa kwenye maeneo hayo yatakayowekewa miundombinu yote muhimu ya ufugaji ikiwemo maji, majani ya malisho na maji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, aliishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha maeneo ya ufugaji (ranchi) kila mkoa na kujenga miundombinu itakayowasaidia wafugaji kufuga mifugo yao kisasa ili waongeze kipato chao, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na umaskini.

Naye Katibu Mkuu wa Mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha wizara yake kifedha ili kufanya utafiti katika sekta ya mifugo ili kuongeza mbinu za kisasa za kuongeza uzalishaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Allan Kijazi, alishauri kuwa ili sekta ya mifugo ipige hatua kubwa, suala la utafutaji masoko kwa ajili ya bidhaa za mifugo, kuongeza elimu kwa wafugaji, pamoja na kuwa na maeneo ya kimkakati ya viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo, ni muhimu likafanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Profesa Gabriel, Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Afrika ikiwa na ng'ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.65, punda 657,380, lakini tija yake bado ni ndogo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/620612e3b7be1a3f95575e24fb2517e6.jpeg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi