loader
Dstv Habarileo  Mobile
Fukwe za Z'bar na athari   za mabadiliko ya tabianchi

Fukwe za Z'bar na athari  za mabadiliko ya tabianchi

ZANZIBAR, katika visiwa vyake viwili vya Unguja na Pemba inakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ambapo kasi ya maji ya bahari yameanza kuvamia makazi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

Hatua hiyo inatajwa kusababisha athari kubwa za kiuchumi na uwekezaji huku watu waliokuwa wakiishi maeneo ya asili ya wazazi wao kuanza kuyakimbia kutokana na kasi ya maji ya bahari huku wawekezaji waliojenga hoteli za kitalii karibu na fukwe za bahari nao wakijionea athari hizo.

Hatua hiyo imeanza kuwashtua viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kutoa maagizo mbalimbali kwa watendaji wa taasisi zinazojishughulisha na kukabiliana na mazingira. 

Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amezitaka mamlaka za usimamizi wa mazingira na idara ya mazingira kufanya upembuzi yakinifu wa kitaalamu wa athari za mabadiliko ya tabianchi ili kubaini maeneo ambayo yameathirika na kuchukua hatua za marekebisho.

Othman amesema hayo alipofanya ziara ya kutembelea Idara zilizo chini ya ofisi yake na kufanya mazungumzo na watendaji pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika.

Anasema maeneo mengi yameathirika na mabadiliko ya tabianchi na hivyo anawataka wataalamu hao kutumia uwezo wao ili kuyalinda maeneo hayo, hususani maeneo ya makazi ya watu pamoja na shughuli za kilimo sambamba na fukwe za baharini.

Anatoa mfano wa maeneo ya kaskazini mwa kisiwa cha Pemba ikiwemo Msuka pamoja na Kisiwa Panza na Mtambwe Juu ambavyo vimeathirika na kutishia wananchi kuvikimbia huku minazi iliopo pembezoni mwa fukwe z bahari ikianguka.

''Hili ni tatizo kubwa ambalo linatishia mustakabali wa maisha ya wananchi pamoja na sekta ya uwekezaji. Yapo maeneo Unguja na Pemba wananchi wake wameanza kuyakimbia kutokana na tishio la kasi ya maji kuvamia maeneo ya makaazi ya wananchi," anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo ipo haja ya kutumiya wataalamu wa ndani na nje kuongeza Ardhi ya Zanzibar na kutoleya mfano ujenzi wa kufukiya bahari uliofanywa na kampuni ya Salim Said Bakhresa katika eneo la Maruhubi.

Kwa mfano Othman anasema wakati umefika kwa watendaji wa Idara ya Mazingira katika ofisi yake kutoa elimu kwa wananchi kuhusu njia za kukabiliana na athari za mazingira ikiwemo kuotesha miti inayodhibiti kasi ya maji kuingia katika maeneo ya wananchi.

Ameiagiza idara hiyo kuvikusanya vikundi vya wana mazingira na kutoa elimu na ujuzi juu ya kuotesha miti aina ya mikoko ambayo ni maarufu kwa ajili ya kudhibiti maji ya bahari kuingia katika makaazi ya wananchi.

Anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kukata mikoko kwa matumizi ya kuni, mbao au kuezekea nyumba.

Anasema kumejitokeza pia tabia ya baadhi ya watu wanaoishi katika maeneo ya baharini kuchota mchanga wa pwani kwa matumizi yao kitendo ambacho hakikubaliki katika kutunza mazingira.

''Unapochota mchanga wa pwani maana yake unaruhusu maji ya bahari kupanda juu kwa kasi na kusababisha athari za kimazingira," anasema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja anasema idara yake inazifahamu changamoto zote hizo ambazo zinatishia mustakabali mzima wa maisha ya wananchi na maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Anafahamisha kwamba kilichofanyika katika hatua za awali ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mikakati ya kukabiliana na athari za mazingira ikiwemo kuotesha miti mbalimbali pembezoni mwa fukwe kwa wananchi wanaoishi jirani na bahari.

''Zanzibar inakabiliwa na athari kubwa za kimazingira ambazo zimesababishwa na mabadiliko ya tabianchi huku bahari ikivamia kwa kasi kubwa maeneo ya pembezoni mwa fukwe na kuwalazimisha baadhi ya wananchi kuhama makaazi yao ya kudumu'," anasema.

Mjaja anasema yapo zaidi ya maeneo 160 ambayo yako hatarini kutokana na  kuathirika na mabadiliko ya tabianchi huku wakazi wake wakiwa wameyakimbia kwa kuogopa maafa zaidi.

Anatoa mfano wa Kisiwa Panza kilichopo mkoa wa Kaskazini Pemba kwamba kimeathirika upande wa mashariki ambapo kasi ya maji na mawimbi ya bahari yamesababisha wakaazi waliokuwa wakaiishi karibu na pembezoni mwa bahari kuyakimbia.

Anazitaja baadhi ya sababau zilizosababisha athari hizo ikiwemo wananchi kukata miti aina ya Mikoko ambayo ni maarufu kwa kuzuwia kasi ya maji ya bahari pamoja na tabia ya wananchi kuchota mchanga wa pwani kitendo ambacho huruhusu maji ya bahari kuingia katika maeneo ya nchi kavu.

''Tumeshuhudia baadhi ya maeneo ya Kisiwa Panza wananchi wameanza kuyakimbia huku makaburi yakifukuliwa na wakazi wa Mtambwe Mkuu nusu yake wamekimbia kisiwa hicho,'' anasema.

Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imejipanga kuyafanyia kazi zaidi ya maeneo 160 yaliopo Unguja na Pemba ambayo yameathirika na kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya fukwe na makazi ya wananchi kutokana na mabadiliko ya tabianchi huku hoteli za wawekezaji pia zikiathirika.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Riziki Pembe Juma alitembelea eneo la ufukwe wa kijiji cha Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuhusu tishio la maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi yao.

Pembe anasema kasi ya  maji ya bahari kuvamia maeneo ya fukwe ni sehemu ya athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yameikumba dunia kwa ujumla wake.

Kwa mfano, anasema utafiti uliofanywa na mamlaka ya mazingira ya taifa ya Zanzibar umegundua  yapo maeneo 160 ambayo yameathirika na mabadiliko ya tabianchi huku maji ya bahari yakitishia maisha ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa bahari.

Anasema athari kama hizo zipo kubwa katika kisiwa cha Pemba ikiwemo visiwa vidogo vidogo kama Kisiwa Panza, hali iliyosababisha baadhi ya wakazi wake kuanza kuhama maeneo hayo mapema.

Haji Iddi, mwekezaji wa hoteli ya Jambiani Visitor Inn anasema kasi ya maji ya bahari yanatishia uhai wa maendeleo ya sekta ya utalii katika ukanda wa Mkoa wa Kusini Unguja.

''Uhai wa hoteli za kitalii zilizopo pembezoni mwa fukwe za bahari maeneo ya Jambiani zipo hatarini kutokana na kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo hayo,'' anasema.

Annaster Poter, raia kutoka Norway anayemiliki nyumba ya kulala wageni anashauri miongoni mwa njia ya kukabiliana na kasi ya maji ya bahari katika kijiji hicho ni kujengwa kwa ukuta utakaozuwia kasi ya maji kuvamia maeneo ya nchi kavu.

''Zipo njia nyingi za kukabiliana na kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi. Moja ni kujengwa kwa ukuta utakaozuwia kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo,'' anasema.

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika kijiji cha Jambiani maeneo ya pembezoni mwa bahari tayari wamehama na kuhamia maeneo ya juu yenye asili ya jiwe ambapo maji ya bahari sio rahisi kushambulia makazi ya wananchi.

''Mimi tayari nimehama katika eneo lililokuwa likimilikiwa na wazazi wangu miaka mitatu iliopita kutokana na tishio la maji ya bahari kuvamia makazi yetu,'' anasema Haji Pandu.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya alipata nafasi ya kutembelea Zanzibar na kujionea hali halisi ya athari za kimazingira.

Kuhusu njia za kukabiliana na changamoto hizo alisema wakati umefika kwa Tanzania kuomba zaidi misaada ya kitaalamu ya kukabiliana na athari za kimazingira kama wanavyofanya nchi nyengine za Bara la Afrika ambazo zinanufaika na mpango huo.

“Nimekuja Zanzibar kujionea mwenyewe hali ya athari ya mazingira. Sasa Tanzania inalazimika kuomba misaada ya kitaalamu katika kukabiliana na janga hilo,” anasema.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7feee933f31130eb946208180fbaccb1.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi