loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wadau wa Kiswahili wanavyomkubuka JPM 

Wadau wa Kiswahili wanavyomkubuka JPM 

Wadau mbalimbali wa Lugha ya Kiswahili wameeleza hisia zao kufuatia kifo cha Rais John Magufuli (JPM) kilichotokea 17 Machi 2021. Wadau hao wameeleza kifo hicho kuwa ni pigo kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu yeye pia alikuwa ni mdau namba moja katika harakati za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Wadau wa Kiswahili waliozungumza na mwandishi wa makala haya wanamzungumzia Rais John Magufuli kwa namna mbalimbali.  Kwanza, Happylight Joseph, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Umahiri ya Kiswahili kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam akiongea kwa sauti ya upole na kuonesha kuguswa na msiba anasema: 

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kifo cha Rais wetu mpendwa, Dk Johhn Magufuli kwani alikuwa ni rais ambaye alijivunia lugha ya Kiswahili. Ukiangalia katika mikutano ya kampeni za uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani za mwaka 2015 na 2020 muda wote alizungumza na wananchi kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika kuomba kura. 

Happylight, anaendelea kueleza kuwa Magufuli alitoa mchango mkubwa wa kushawishi Kiswahili kitumike kama moja ya lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) inayoundwa na nchi wanachama 16. Pia tutamkumbuka Magufuli kwa kuibua misimu mbalimbali ya Kiswahili kama vile “tumbua jipu”, “watumishi hewa n.k.” alifanunua Happylight. .

Mwingine ni Keflin Bunani, mwanafunzi wa mwaka wa pili kutoka Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu, Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam anayesema: “Kifo cha Rais JPM ni pigo katika Kiswahili na nitamkumbuka kwa kutuanzishia mchakato wa fursa za ajira nje ya nchi kwani kuna baadhi ya nchi za Afrika wakati wa uhai wake alizihamasisha kutumia Kiswahili”.  

Keflin anatoa mfano wa nchi kama vile Zimbabwe na Afrika ya Kusini ambazo Magufuli alikabidhi vitabu vya Kiswahili kwa marais wao.

Watatu ni Majid Mswahili, mwandishi mashuhuri wa vitabu vya Kiswahili hapa nchini anayeeleza: “Mchango wa Hayati JPM haujifichi, alikuwa akisema waziwazi kuwa anataka Kiswahili kitumike kiwe lugha ya Afrika.” 

Anaendelea kusema kwamba Magufili alikwenda Afrika ya Kusini, Zimbabwe Namibia na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika kutafuta fursa kwa maana ya kutaka Kiswahili kifundishwe kwenye shule zao, hatua ambayo ni fursa kwa Watanzania kwenda kufundisha Kiswahili katika nchi hizo.  

Pia anasema Magufuli aliweza kutoa zawadi za vitabu na kamusi za Kiswahili katika nchi za Zimbabwe na Afrika ya Kusini. Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa alikubali kuingiza lugha ya Kiswahili katika mitaala ya elimu ili kiweze kufundishwa nchini humo. 

Majid anaendelea kueleza kuwa, hivi karibu, kabla ya kifo chake, Magufuli alipigia chapuo Kiswahili kitumike kama lugha ya sheria na kuagiza sheria zote zilizo katika lugha ya Kiingereza zitafsiriwe kwa Kiswahili. 

Haya anasema ni maendeleo na mafanikio makubwa aliyotuachia, kwa kweli tutamkubuka daima. 

Baadhi ya Vitabu vya Kiswahili vilivyoandikwa na Bwana Mswahili ni Nje Ndani (Tamthiliya), Kizungumkuti (Tamthiliya), Hadithi fupi kwa Ufupi (Hadithi fupi), Kijalunga (Tamthiliya) na Dunia Ndivyo Ilivyo (Riwaya) inayotarajiwa kutoka hivi karibuni. 

Mdau mwingine ambaye hapendi kutaja jina lake anasema hatua ya Magufuli kuzungumza kwa Kiswahili kwenye mikutano ambayo kuna wageni mbalimbali ilibadilisha mwenendo ambao watangulizi kuna wakati walishindwa.

“Ungeweza kukutana kuna mgeni kaja Tanzania, labda kufungua maonesho ya sabasaba, Rais anazungumza KIngereza wakati asilimia zaidi ya 95 ya wasilililizaji wakiwa Watazania ambao hawajui Kingereza,” anasema. 

Magufuli atakumbukwa kwa ushirikiano na nchi kama vile Ethiopia, Afrika Kusini na Morocco ambazo zilihitaji wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili kutoa elimu kwa wananchi wao. Alisaini makubaliano na Afrika Kusini ya kutoa wataalamu wa Kiswahili.

Magufuli alizaliwa 29 Oktoba 1959 huko Chato mkoani Geita.  Alipata elimu yake ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Baaada ya hapo alijiunga na Chuo cha Ualimu Mkwawa na kutunukiwa Diploma ya Ualimu katika masomo ya Kemia na Hisabati mwaka 1979 hadi 1981.  

Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa Shahada ya Awali ya Ualimu katika masomo ya Kemia na Fizikia. Kati ya mwaka 1991 na 1994 alisoma Shahada ya Umahiri ya Sayansi, masomo ya Kemia na Fizikia Chuo Kikuku cha Salford, Uingereza programu iliyotolewa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.   

Magufuli alihitimu shahada ya uzamivu ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2009.  

Aliwahi kuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2000 hadi 2005 na mwaka 2010 hadi 2015. Wakati wa uongozi wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) 2019 hadi 2020. 

Akiwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , amedumu madarakani kuanzia 2015 hadi alipofariki dunia tarehe 17 Machi 2021 katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam kutokana na tatizo la moyo. 

Magufuli alizikwa tarehe 26/03/2021 nyumbani kwao Chato, mkoa wa Geita.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1b9b7a53efd018364cb44c5120da48c0.jpg

WAFUGAJI wa ng'ombe wa maziwa nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ...

foto
Mwandishi: Rajabu Kiswagala

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi