loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwisho wa ngebe!

Mwisho wa ngebe!

MWISHO wa ngebe ni leo baada ya dakika 90 za mechi ya watani Simba na Yanga kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam. 

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara imekuwa ikisubiriwa na wengi kwa vile itatoa hatima ya ubingwa.

Huu utakuwa mchezo wa 108 kuwakutanisha miamba hawa ambapo katika michezo 107 Yanga ni kinara ikiwa imeshinda michezo 37, Simba akishinda mara 32 wakitoka sare mara 38.

Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, wanaingia kwenye mchezo wa leo, wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1  mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa  Novemba 7 mwaka jana. 

Aidha, Simba inaingia kwenye mchezo wa leo, ikiwa inaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 61 baada ya kushuka uwanjani mara 25 ikishinda mara 19 ikitoka sare michezo minne na kupoteza michezo miwili.

Wapinzani wao Yanga, wanashuka uwanjani kuwakabili Simba, wakiwa nafasi ya pili katika msimamo wakiwa wamejikusanyia pointi 57 wakiwa wameshinda michezo 16 sare mara tisa na kupoteza mara mbili.

Simba leo itamkosa beki wake Ibrahim Ame ambaye amefungiwa michezo mitatu  kwa utovu wa nidhamu, wakati Yanga ina majeruhi mmoja  wa muda mrefu, Mapinduzi Balama.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kocha mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi alisema kuwa  atakuwa na mabadiliko kadhaa baadhi ya maeneo kwenye kikosi chake kulingana na ukubwa wa mchezo husika.

"Naamini mabadiliko niliyofanya yatanipa matokeo mazuri, kwa sababu na maandalizi ambayo tumeyafanya kulingana na jinsi ambavyo Simba inacheza, najua ni timu nzuri ambayo imeonyesha kiwango kizuri katika michuano ya  Afrika.

"Naiheshimu Simba ni timu nzuri inafanya vizuri namjua Gomes (Didier kocha wa Simba) nimekutana naye mara moja katika michuano ya Afrika ni kocha mzuri natarajia mchezo wa kesho (leo)  utakuwa mzuri wa kiungwana kwa pande zote," alisema Nabi.

Nahodha wa timu ya Yanga, Haruna Niyonzima alisema kuwa yeye ni mchezaji mzoefu na michezo hii kwani sio mara yake ya kwanza amefanya hivyo akiwa na Simba na hivi sasa yuko Yanga, kazi yake kama mchezaji mkubwa ni kupunguza presha kwa wachezaji ambao huu ni mchezo wao wa kwanza.

"Siku zote mechi kubwa mara nyingi huamuliwa na wachezaji wakubwa sisi hatuna presha tunaendelea kujipanga kwaajili ya mchezo huu muhimu kwetu," alisema Niyonzima.

"Mimi nimecheza michezo hii nikiwa katika timu mbili ni mchezo mkubwa lakini sisi hatuna presha mwalimu amesema hatuwezi kuweka wazi mbinu tunazotumia kwani kufanya hivyo ni kuuza mbinu kwa adui," alisema Niyonzima.

Kocha msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, alisema michezo ya dabi mara nyingi imekuwa migumu lakini pamoja na ugumu wa mchezo huo wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo.

"Tunaenda kuwapa burudani wapenzi wa Simba wachezaji wangu hawana presha wanacheza michezo mingi mikubwa hivyo mashabiki wetu waje kwa wingi kutoa hamasa," alisema Matola.

Wakati huohuo Mwandishi Matern Kayera kutoka Dodoma anaripoti Spika wa Bunge Job Ndugai ameipiga kijembe Yanga akidai wajiandae kwa kufungwa mabao mengi leo.

Aliyasema hayo jana wakati akiahirisha Bunge hadi Jumatatu saa tatu asubuhi.

Ndugai alisema kwa kuwa leo ni mchezo wa watani hao wa jadi, alisema hakuna namna kwa Yanga isipokuwa wajiandae kupigwa mabao mengi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9ad20d2baa503a6521dce1d7883bc86b.jpeg

YANGA leo saa 1:00 usiku itashuka dimbani kuikabili ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa 

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi