loader
Mabadiliko yanakuja

Mabadiliko yanakuja

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake inakwenda kufanya mabadiliko ya kisera, kisheria, kitaasisi na kiuongozi ili kurahisisha uwajibikaji na kuhakikisha uchumi wa nchi unapanda na kuwaletea maendeleo wananchi.

Amesisitiza kwamba katika safu ya kujenga ya nchi, atachagua mtu yeyote kulingana na weledi wake na maadili bila kujali chama anachotoka ili mradi awe na mchango katika kuijenga nchi.

Rais Samia aliyasema hayo mkoani Dar es Salaam jana alipokutana na kuzungumza na wazee wa jiji hilo kwa niaba ya wazee wote nchini.

“Wazee wangu mtashuhudia mabadiliko ambayo nia yake ni kutengeneza na si kubomoa, mkiona tunaleta mabadiliko mjue tuna nia njema ya kujenga nchi na si kubomoa, katika mabadiliko haya kijana wako akiguswa basi mjue ni kwa nia njema tunataka tuipeleke Tanzania juu zaidi,” alisisitiza Rais Samia.

Aliwaomba wazee waiunge mkono serikali katika mabadiliko hayo, ili itimize dhamira ya kuendelea kuiletea nchi maendeleo. “Tutawasikiliza bila bezo wala dharau yale yote mtakayotuambia na kuyafanyiakazi yale mliyotufikishia,”

Alisema serikali yake imejipanga kuendeleza kazi nzuri iliyoanza na awamu zote za nyuma ambayo ni pamoja na kujenga barabara, madaraja, reli, bandari, kutengeneza meli na vivuko, mambo yote yanayohusu usafiri, usafiri wa watu na bidhaa.

Alisema mambo yote hayo na mengineyo yataendelezwa kwa nguvu kubwa ili ishajihishe biashara na kujenga uchumi wake.

“Tupo uchumi wa kati lakini tuna kazi kubwa ya kuinua uchumi wetu ufikie kule kulikotuingiza uchumi wa kati. Kila mtanzania anapaswa kuchangia katika ujenzi wa uchumi bila kujali tofauti za kabila, dini, rangi au imani ya siasa lazima tuchangie katika kujenga uchumi wetu,” alisisitiza.

Alisema ametoa kauli hiyo kwa kuwa huko mbele katika uongozi wake, safu za kujenga uchumi hatachagua, bali atachagua Mtanzania yeyote mwenye weledi anayeweza kujenga uchumi wa nchi. “ Sitaangalia anatoka katika chama kipi,”

Mtangulizi wake, Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, katika mabadiliko ya kiuongozi aliyofanya na ambayo yalionekana mageni kwa wengi katika ulingo wa siasa, ilikuwa ni kuteua wanasiasa kutoka baadhi ya vyama vya upinzani na wengine wakiwa na muda mfupi wamehama vyama hivyo kuingia Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli alimteua Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Aprili mwaka 2017, Magufuli alimteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambaye wakati wa uteuzi, alikuwa mwanachama wa ACT Wazalendo. 

Vile vile alimteua aliyekuwa mgombea wa urais mwaka 2015 kupitia ACT Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro nafasi ambayo anaishikilia mpaka sasa. 

Katika uteuzi aliofanya Julai mwaka 2018, Magufuli alimteua  David Kafulila aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini (NCCRMageuzi), Moses Machali (Kasulu Mjini, NCCR Mageuzi), na Patrobas Katambi (aliyekuwa mwenyekiti Baraza la Vijana la Chadema) kuwa viongozi serikalini. Wote walikuwa wamejiunga na kuwa ndani ya chama hicho kwa muda usiozidi mwaka. 

Katambi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Machali wilaya ya Nanyumbu na Kafulila aliteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe.

Wengine waliokuwa wana Chadema kabla ya kuhamia CCM wakapata ubunge  na kisha wakateuliwa na Magufuli kuwa mawaziri/naibu waziri ni Mwita Waitara, David Silinde na Pauline Gekul  ambao mpaka sasa wapo kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Samia. 

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi