loader
Dstv Habarileo  Mobile
…Aonya wanaopima kina cha maji

…Aonya wanaopima kina cha maji

RAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kushughulikia tatizo la ujambazi na vibaka lililoanza kuibuka akionya wote wanaojihusisha na vitendo hivyo wasijaribu kina cha maji.

Akizungumza jana na wazee wa Dar es Salaam kwa niaba ya wazee wote nchini,  Samia aliahidi kutekeleza kwa nguvu zote vipaumbele sita alivyozungumzia kwenye Bunge hivi karibuni ikiwemo suala la kudumisha amani na usalama.

“Na hili tutalisimamia kwa nguvu zote, tuna vyombo vya ulinzi na usalama na leo nimesoma kwenye vyombo vya habari mambo si mazuri kwamba Dar es Salaam wanajaribu mambo ya ujambazi na upokonyaji. Naomba nitoe ujumbe wasijaribu kina cha maji, IGP yupo hapa naomba mlishughulikie,” alisisitiza.

Aliwaomba wazee na vyombo vya dini kurejea tena kwenye mila, desturi na maadili kwani hali ngumu ya uchumi haifanyi mtu awe jambazi bali kuna mambo mengine yanamfanya mtu awe hivyo. “Tuwaangalie watoto wetu wakue kwa maadili. Serikali inawaahidi italisimamia hili kwa nguvu zote,”

Samia alisisitizia pia juu ya Watanzania kujenga utamaduni wa kuwalea wazee iwe ni wazazi wao au ndugu na kuacha tabia za kimagharibi za kuwatelekeza  na kusababisha kuishi kwenye vituo maalumu vya kuwalea vinavyojengwa na serikali.

Alisema suala la maadili linapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa kinachoendelea sasa kwa vijana kutoonesha nidhamu hususani kwenye usafiri wa umma ni dalili za kuwapo kwa dosari.“ Na dosari hii sijui tumeitoa wapi? Nyie mliotuzaa sisi tunaweza kuwapisha wazee lakini sio tuliowazaa sisi.”

Rais Samia pia aliahidi kuendelea kuboresha sekta za elimu, miundombinu, afya na maji huku akitoa matumaini kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa miradi miwili iliyopo inayoendelea kutekelezwa itakapokamilika mkoa huo utakuwa na huduma ya maji kwa asilimia 100.

Kuhusu tiba kwa wazee, alisema suala hilo litafanyiwa kazi kupitia marekebisho ya sera yanayokwenda kufanyiwa kazi na kuahidi kutanua wigo wa matibabu kwa wazee hao.

Alisema kwa sasa dunia iko kwenye janga la corona na waathirika wakuu ni wazee, na kwa kutambua hilo kamati aliyoiunda kushughulikia janga hilo, inakwenda vizuri na hivi karibuni itawasilisha ripoti kwake.

 “Yale yote yanayofanya wazee wawe kundi hatari tutayashughulikia na kuwafundisha mbinu za kujikinga,” alisema.

Kwa upande wa sheria ya wazee, alisema pamoja na kupitia sera, pia serikali itatunga sheria na mambo yote yanayohusu wazee yatawekwa vizuri. 

“Nasema hivi kwa sababu nasi ni wazee wa kesho. Nisipoweka vizuri nije nisiyakute sitakuwa na wa kumlilia kwamba nafasi nimeitupa mwenyewe,” alisema.

Kuhusu kuwezesha wazee, alisema mwaka huu kupitia Mfuko wa Jamii (Tasaf), utakwenda wilaya zote. Alisema pamoja na kwamba mfuko unakaribia kumaliza muda wake, utaanzishwa mwingine unaofanana na Tasaf na wazee wote wenye sifa wataingizwa kwenye mfumo huo.

Aliwaahidi wazee kuwa atalishughulikia suala la kuwalipa wazee wote pensheni hata wale wasiokuwa waajiriwa. “Jambo hili tulizungumza tangu 2004 tukaliangalia tukaona ni gumu kulitekeleza kifedha. Kwa hali ilivyo sasa sitaki kuwadanganya sasa na hali ya uchumi wetu pamoja na kupanda na kufikia uchumi wa kati, kwa sababu ya corona tumeshuka kutoka asilimia saba hadi asilimia 4.5,” alisema. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/2e253818ef2feebd83049838cb1cfd7b.jpeg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi