loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia: Kitabu cha Mzee Rukhsa kimenitoa woga

Samia: Kitabu cha Mzee Rukhsa kimenitoa woga

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema aliposoma Kitabu cha maisha ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa mara ya kwanza aliyokutana nayo yalimshitua lakini alipokirudia, kimemtoa woga huku kikiacha mafunzo mengi kwa viongozi ikiwamo la kutambua kwamba uongozi si lelemama.

Akizindua kitabu hicho ‘Mzee Rukhsa, Safari ya Maisha yangu’ Samia alimtaja Mzee Mwinyi, maarufu Mzee Rukhsa kwamba ni Baba wa Mageuzi, alisema kitabu hicho ni fundisho kubwa kwake kama Rais kwani kinafariji, kinatoa mwongozo wa nini kinatakiwa kufanyika kwa kiongozi hasa wa ngazi kubwa ya urais.

Kitabu hicho kinachoelezea maisha ya Mzee Mwinyi aliyeongoza Tanzania tangu mwaka 1985 hadi 1995, kinaeleza tamu na chungu wakati wa uongozi wake.

“Nimekisoma kitabu chako mara mbili. Nilipokisoma mara ya kwanza, niliyokuta ndani nikashituka kidogo nikasema mtu wa maarifa na heshima zote , Mzee Mwinyi yamempata haya, mimi je?

Lakini kutokana na ufasaha wa lugha, nikakirudia na woga ukanitoka nikasema kazi iendelee,” alisema Samia.

Alisema kitabu hicho ni hazina kubwa kwa nchi na vizazi vijavyo kwani kimeeleza maisha yake yote ya kikazi na tangu akiwa mtoto mdogo hadi kuwa mkubwa na kuwa Rais wa nchi.

Baba wa Mageuzi

“Hivi punde tumesikia muhtasari wa kitabu cha Mwinyi lakini mimi pia nimekisoma, kimeshehemi mambo mengi… Kwa yeyote atakayekisoma atajifunza mambo mengi sana. Binafsi nimepata mengi ya kujifunza kama kiongozi kubwa kuliko yote. Ni kwamba Mwinyi ni Baba wa Mageuzi nchini,” alisema.

Alisema Mzee Mwinyi ndiye alisimamia mageuzi makubwa ya kiuchumi akisema: Na bahati nzuri ameeleza kwamba wakati anaingia madarakani, hali ya uchumi ilikuwa mbaya kutokana na matatizo mbalimbali ikiwamo kupanda kwa mafuta, ukame, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuibuka vita ya Uganda na masharti magumu kutoka kwa wafadhili na taasisi za kifedha mwaka 1980.

Alisema baada ya Mwinyi kuingia madarakani alianzisha mageuzi makubwa ya kiuchumi hususani kwa kuanzisha sekta binafsi kushirikiana na serikali kushirki shughuli za kiuchumi.

Samia aliendelea kumwelezea Mwinyi alivyoanzisha ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambayo mengi yalianzishwa kwa hasara na kubebesha serikali hasara miongoni mwake ikiwa ni Kiwanda cha Bia Tanzania. Mageuzi mengine ni katika sekta ya fedha na bima na yale ya kusimamia mageuzi ya kisiasa kwa kurudisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1994. “Ni sahihi kusema Mzee Mwinyi ni Baba wa Mageuzi nchini.”

Mafunzo ya kitabu

Rais Samia alisema mbali na kusimamia mageuzi, kitabu kinatufundisha mambo mengine mengi hususani kwa viongozi.” Kwanza, ametufundisha uongozi wa nchi hautafutwi bali unatoka kwa Mungu,” alisema akirejelea muhtasari wa maisha yake unaoeleza kuwa Mzee Mwinyi alizaliwa Mkuranga na kisha akapelekwa Zanzibar kuwa Shehe mkubwa.

Alieleza zaidi kuwa Mzee Mwinyi hakuwa muasisi wa ASP na wala hakushiriki Mapinduzi ya Zanzibar na nafasi pekee aliyoshika ilikuwa ni ukatibu wa ASP kwenye tawi. Alisema kwa kudra ya Mungu alikuwa Rais wa Zanzibar na Muungano bila kuhonga mtu yeyote jambo alilosisitiza kuwa ni fundisho kubwa kwa wenye dhamira ya kutaka kuongoza kwamba uongozi wowote ni kwa Kudra za Mwenyezi Mungu.

Funzo lingine ambalo Rais Samia amelitaja kutokana na kitabu hicho ni kwamba uongozi ni dhamana akirejelea uamuzi wa Mzee Mwinyi kujiuzulu kutokana na mauaji ya vikongwe. “Kitabu kinafundisha uongozi si lele mama. Utakumbana na changamopto mbalimbali,” alisema na kukumbushia changamoto alizokumbana nazo Mwinyi ikiwamo kuibuka kwa Ukimwi, migogoro ya kidini, kundi la G55, migomo ya wanafunzi na kuongeza kuwa uvumilivu na ustahimilivu ndiyo silaha pekee iliyomsaidia.

Funzo la nne alilokutana nalo ni umuhimu wa kukiri makosa. Samia alisema viongozi si malaika ni binadamu huku akipongeza kitendo cha Mwinyi kukiri baadhi ya makosa yaliyofanyika katika kipindi chake wakati wa kufanya mageuzi ya kiuchumi na hasa baada ya misamaha ya kodi kutumika vibaya na baadhi ya wajanja.

Rais alitaja funzo la tano ni la viongozi kupendana na kushirikiana kwa kutoa mfano wa Mzee Mwinyi kuondolewa kwenye nyumba ya serikali Oyster Bay jijini Dar es Salaam kwa vitimbwi lakini baadaye, alipopata urais wa Muungano, akamteua waziri huyo katika Baraza lake la Mawaziri.

Alisema alikuwa na vifaa vya ujenzi vilivyokuwa kwenye nyumba hiyo na waziri aliyechukua madaraka alimwondoa kwa nguvu na akashindwa kuvichukua lakini alipokuja kuwa Rais alimteua kuwa kati ya mawaziri wake.

“Waziri mpya alikuja akamtaka aondoke haraka .Alikubali kuondoka na kuacha vifaa vyake…Pamoja na kufanyiwa vitimbwi hivyo vyote, alimteua waziri kwenye Baraza la Mawaziri. Kama huyo waziri bado anaishi, sijui anajisikiaje huko aliko. Sina hakika wangapi kati yetu tungefanya aliyofanya Mzee Mwinyi,” alisema Rais Samia.

Akimwelezea zaidi Mwinyi ambaye ndiye Mtanzania pekee aliyeshika urais Zanzibar na Muungano kwa nyakati tofauti, Samia alisema, “Tunapata fundisho jingine kwamba sisi binadamu hatuna budi kupendana, kuheshimiana unayemfanyia vitimbi leo hujui kesho utamkuta akiwa nani. Ametufunza pia kutokuishi na visasi mioyoni mwetu.”

Rais Samia amewataka viongozi kuiga utendaji kazi wa Mzee Mwinyi kwa kuwa alikuwa mwenye hekima kubwa katika kuwahudumia wananchi na mwenye subira na maadili mazuri.

Aliwataka wananchi kukinunua kitabu hicho kwa kuwa kinaelezea mengi mbali na mafundisho ya kisiasa, pia kuna mambo ya kijamii na kiuchumi na historia..

Alisema kati ya mambo aliyojifunza katika suala la kuitikia mwito wa kazi ya Mungu ni pamoja na kusoma historia ya Mzee Mwinyi kuwa wakati akiwa na miaka minne alipelekwa Zanzibar ili kuja kusomea elimu ya dini awe Shehe mkubwa nchini lakini akaja kuishia kuwa mtumishi wa umma na Rais wa Zanzibar na Tanzania.

Pia alimwelezea Rais Mwinyi kama mtu mwenye bahati ya kuwa Rais wa Zanzibar na Tanzania Bara huku akimwombea kwa Mwenyezi Mungu ambariki aendelee kuishi kufikia zaidi ya miaka 100. Sasa ana umri wa miaka 96.

Wakati huo huo Serikali imemkabidhi zawadi ya gari jipya aina ya Mercedes Benzi imsaidie kwenye shughuli zake mbalimbali.Kwa mujibu wa Rais Samia, uzinduzi huo wa kitabu ulipangwa ufanywe Machi mwaka huu na Rais John Magufuli.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f3dd720b60f7c88fa911b8fc206c14e8.jpg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi