loader
Dstv Habarileo  Mobile
Leo siku ya mama, mthamini na umuenzi

Leo siku ya mama, mthamini na umuenzi

L

EO ni Siku ya Mama. Ni siku ya kuonesha heshima na thamani ya akina mama katika familia. Siku hii huadhimishwa katika mataifa mbalimbali tarehe tofauti lakini miezi maarufu zaidi ni Machi na Mei.

Ilianzia kusherehekewa nchini Marekani karne ya 20. Kabla ya hapo, kulikuwa na Siku ya Mama katika jamii mbalimbali kwa namna tofauti.

Baadaye katika baadhi ya nchi za Ulaya, hasa Visiwa vya Britania, Wakristo walianzisha Jumapili ya Mama Kanisa iliyokuwa ikiadhimishwa kutukuza na kulipa kanisa heshima kama mama wa waumini. Lakini baadaye ikawa ya kuheshimu akina mama.

Simulizi juu ya asili ya Siku ya Mama ya sasa haikamiliki bila kumtaja mwanamke Anna Jarvis aliyeibuni mwaka 1908 na hatimaye kurasimishwa nchini Marekani mwaka 1914 iadhimishwe kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei.

Anna alikuwa mmoja kati ya watoto 13 katika familia yake lakini wanne ndiyo waliishi mpaka kuwa

wakubwa. Wengi walifariki wakiwa wadogo kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Katika makala ya BBC Swahili iliyochapishwa mwaka jana ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mama, Profesa wa Chuo cha Wesleyan West Virginia, Antolini, anasema kampeni ya Anna ya kuadhimisha siku hii aliirithi kutoka kwa mama yake mzazi, Ann Reeves Jarvis aliyetumia maisha yake kushawishi akina mama kuwajali watoto wao.

Alianzisha Klabu ya Siku ya Kazi ya Mama iliyofanya kazi ya kufundisha wanawake namna ya kuhudumia watoto wao. Wakinamama walijifunza usafi kama vile umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa.

Baada ya Ann kufariki dunia mwaka 1905, Anna aliahidi kutimiza ndoto ya mama yake ingawa alitumia njia tofauti.

Kwa upande wa Ann, aliadhimisha kazi iliyofanywa na wakina mama kuboresha maisha ya wengine lakini kwa Anna alilenga mtoto wa kike na kaulimbiu ya Siku ya Mama ikawa ‘Kwa mama bora aliyewahi kuishi-Mama yako.’

Ujumbe huu uligusa pia

makanisa. Miaka mitatu baada ya kifo cha Ann, maadhimisho ya kwanza ya siku ya mama yalifanyika kwenye kanisa la Wamethodisti huko Grafton.

Anna alichagua Jumapili ya pili ya Mei kwa sababu ni karibu na tarehe 9, siku ambayo mama yake alifariki.

Anna alikuwa akiwapa mamia ya wakina mama waliohudhuria sherehe maua meupe ya carnations , yaliyopendwa zaidi na mama yake.

Kutokana na mafanikio ya Siku ya Mama ya kwanza, Anna ambaye hakuolewa na wala hakuwa na mtoto katika maisha yake, alijikita kuona sikukuu hiyo inaongezwa kwenye kalenda ya siku za kitaifa.

Anna alijenga hoja kwamba sikukuu za Marekani zimejikita kwenye mafanikio ya wanaume. Alianza kampeni ya kuandika barua kwenda 

kwenye magazeti, wanasiasa maarufu akiwataka kukubali kutenga siku ya kuthamini umama.

Mnamo mwaka 1912, majimbo, miji na makanisa yaliidhinisha siku kuadhimishwa kila mwaka na Anna alianzisha Umoja wa Kima-taifa 

wa Siku ya Mama

kumwezesha ku-

panua wazo lake.

Alipata malipo ya uvumilivu mwaka 1914 wakati Rais Woodrow Wilson aliposaini rasmi uanzishaji wa Siku ya Mama katika Jumapili ya pili ya Mei.

Awali, siku hii ilikuwa ni maadhimisho binafsi kati ya mama na familia. Ilihusisha uvaaji wa nguo nyeupe na beji ya ua na kutembelea akinamama au kuhudhuria 

ibada kanisani.

Lakini siku hii ilipotangazwa kuadhimishwa rasmi kitaifa, haikuchukua muda mrefu kabla ya wafanyabiashara wa maua, kampuni za kadi na wafanyabiashara wengine kuiteka na kuipa umaarufu kibiashara.

Mwaka 1920, Anna alichukizwa na maadhimisho hayo yalivyogeuzwa biashara. Alisihi jamii kuacha

kununua maua, kadi na pipi za Siku ya Mama.

Mwishowe aliamua

kufanya kampeni ya wazi

dhidi ya wanaofaidika kwa Siku ya Mama hususani wenye bidhaa za kuoka na wataalamu wa maua.

Pia alifungua madai ya kisheria dhidi ya vikundi vilivyotumia jina la ‘Siku ya Mama.’

Hadi anafariki mwaka 1948, Anna alikuwa amejivua suala zima la maadhimisho hayo na kushawishi serikali siku hiyo iondolewe kwenye kalenda ya Marekani.

Hata hivyo, mpaka sasa nchini Marekani inaendelea kusherehekewa kwa zawadi na maua kwa akinamama na wanawake wengine na imekuwa moja ya sikukuu kubwa zenye matumizi makubwa .

Katika maadhimisho ya mwaka jana yaliyofanyika Jumapili ya Mei 10, kulingana na Mtandao wa Habari wa Vatican News ulinukuu Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani (USCCB), linasema hii ni siku muhimu sana ya kuwaheshimu na kuwaenzi wanawake kutokana na mchango wao mzito katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza linasema siku hii ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea akina mama ambao wamepewa dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha injili ya uhai.

Kwa wale wanawake ambao wamepitia kipindi kigumu wakati wa ujauzito, wafarijike kwa sala na sadaka inayotolewa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kupitia mtandao huo wa Vatican News, Padre Richard Mjigwa, ananukuliwa akisema, kwa kuzingatia uzuri na utakatifu wa maisha, dhamana na wajibu wa akina mama katika maisha ya familia na jamii katika ujumla wake, Siku ya Mama Duniani ni muda muafaka wa kuwaenzi akina mama duniani.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/708e72c53505114cecb3500622ebf94a.jpeg

HIVI karibuni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafi ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi