loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia azikaribisha kampuni za Uingereza

Samia azikaribisha kampuni za Uingereza

RAIS Samia Suluhu Hassan amezikaribisha kampuni za Uingereza kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali yenye fursa na ameelezea kufurahishwa na ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo anayeshughulikia masuala ya Afrika, James Duddridge ambao utafungua milango zaidi.

Rais Samia akizungumza na Duddridge Ikulu, Dar es Salaam jana, alisema Serikali ya Awamu ya Sita ipo tayari wakati wote kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na amebainisha kuwa tayari imeanza kuchukua hatua za kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuweka sawa masuala ya kikodi na vivutio vingine ili wawekezaji wengi zaidi wajitokeze.

Aliiomba Uingereza iendelee kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za maendeleo na kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na masuala ya mazingira.

Duddridge alisema ana imani kubwa na uongozi wa Rais Samia kuwa utaendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Dk John Magufuli na amemhakikishia kuwa Uingereza itaendelea kushirikiana na Tanzania na kampuni za Uingereza zitaongeza uwekezaji nchini.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Dk Natalia Kanem jana.

Katika mazungumzo yao, Rais Samia ameishukuru UNFPA kwa ushirikiano wake mzuri na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na ujauzito kwa mabinti wadogo, vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, kukabiliana na ukatili wa kijinsia na ukeketaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Samia amemhakikishia Dk Kanem kuwa atakuwa balozi mzuri wa kuhakikisha juhudi za kuwanusuru wanawake wanaojifungua wasipoteze maisha na kupiga vita mimba za utotoni na ameiomba UNFPA kuendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo kufadhili miradi ambayo inatekelezwa nchini.

Dk Kanem amesema Umoja wa Mataifa wana matumaini makubwa na uongozi wa Rais Samia na amemhakikishia kuwa UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali shirika hilo.

Aliongeza kuwa kwa kutambua umasikini unaozikabili familia nyingi hasa vijijini UNFPA inatekeleza Mkakati wa Sifuri Tatu ambao kwanza inawasaidia wanawake na wanaume kushirikiana kupanga familia zao vizuri ili kujenga familia imara na zenye furaha, pili ni kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kuhakikisha wanawake wanajifungua katika vituo vyenye huduma, mabinti wadogo hawabebi ujauzito wakiwa na umri mdogo na kukomesha ukeketaji, na tatu ni kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f280478ef36ba0e1a191d5f27451b701.jpeg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi