loader
Majaliwa awacharukia TRA bandarini Dar

Majaliwa awacharukia TRA bandarini Dar

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutokuwa kikwazo kwa wateja kuhudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na mfumo wao wa Pamoja wa Forodha (Tancis) kukatika katika.

Aliyasema hayo jana alipofanya ziara katika Bandari hiyo na kuzungumza na wadau wa bandari hiyo wakiwemo TRA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Kampuni ya upakuaji makontena bandarini (TICTS) na madereva wa malori.

Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu alibaini kuwa kitendo cha kukatika katika kwa mfumo wa Tancis wa TRA kunasababisha shughuli za bandari kusimama hali inayokwaza wateja.

“Kutofanya kazi vizuri

kwa mfumo wa Tancis ambao upo chini ya TRA kunakwamisha shughuli za bandari, kwa hiyo TRA hakikisheni mfumo huu unafanya kazi vizuri, msitucheleweshe, nchi nyingi zinatutegemea sisi,”alisema Majaliwa.

Pia aliwataka TRA kuwepo kwenye maeneo yote wanayotakiwa kuwepo bandarini hapo ili wateja wahudumiwe vizuri, lakini pia akawataka TPA na Tanroads kuhakikisha suala la mizani yao ya kupimia uzito wa magari bandarini hapo haiwi kikwazo kwa wateja.

Majaliwa pia aliitaka mifumo yote ya utoaji huduma bandarini hapo ukiwemo mfumo wa kuhudumia mizigo wa TPA (Cargo System) kufanya kazi kwa kusomana ili kusiwe na ucheleweshaji wa aina yoyote katika kuwahudumia wateja.

Aidha hakufurahishwa kuona meli nyingi zipatazo 14 zikisubiri kuingia bandarini kutokana na Wakala

wa Meli Tanzania (Tasac) kuchelewa kuwapa vibali vya kuingia bandarini.

Aliwataka Tasac kumpa maelezo kwa kuwa hawakuwepo kwenye ziara hiyo hali iliyomchukiza.

Majaliwa pia alisema alifika bandarini hapo kujiridhisha kama kweli kuna msongamano wa malori kama ilivyodaiwa na dereva mmoja aliyerusha video yake mtandaoni akidai inachukua hadi siku nne kuhudumiwa bandarini hapo.

“Wakati nakuja hapa nimezungumza na madereva wa malori huko njiani, wamenieleza kushangazwa na taarifa ya dereva mwenzao kwamba hawahudumiwi kwa haraka, wameniambia wanafurahishwa na namna bandari mnavyowahudumia katika kushusha na kupakia mizigo yao, wengi wamesema haiwachukui zaidi ya saa 24 kupakia mzigo,”alisema Majaliwa.

Pia aliwahakikishia wateja wa Bandari ya Dar

es Salaam kuwa serikali itazifanyia kazi changamoto zote ikiwemo upanuzi wa barabara inayoanzia Daraja la Mwalimu Nyerere hadi bandarini hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamisi alisema wakati mwingine msongamano husababishwa na shughuli za upanuzi wa bandari zinazoendelea kwa kuwa asilimia 40 ya eneo la bandari hiyo liko katika ujenzi na kuwataka wateja kuwa wavumilivu kwani ujenzi huo utakamilika Agosti na huduma zitatolewa kwa kasi zaidi kuliko ilivyosasa.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Operesheni wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo ya Omar Awadh Transport inayosafirisha shaba kutoka Zambia hadi bandarini hapo, Amer Ali Saleh, alisema tayari wamemtaka dereva wao aliyemtaja kwa jina la Mambo Omari Mambo kufika ofisini kwao kujieleza kwa nini alirusha video hiyo wakati muda

aliotumia kuhudumiwa bandarini hapo ulikuwa mfupi tofauti na madai yake.

“Hatujaonana na dereva huyo, tumeshamwita aje ofisini ajieleze kwa nini aliongea maneno yale ya kupotosha umma,tunamtaka aje ili tujue changamoto zake tumsaidie,”alisema Saleh.

Mkuu wa Operesheni wa Kampuni ya Reload Logistics Tanzania, Frank Mwilongo alisema magari yao hupakuliwa ndani ya saa 24 yanapoingia bandarini hapo.

Mwilongo alisema madai ya dereva Mambo kuwa wanachelewa kuhudumiwa bandarini hapo siyo ya kweli kwa kuwa Mambo alifika bandarini hapo Mei 10 mwaka huu na kuhudumiwa siku hiyohiyo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Idara ya Usafirishaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Abdulkarim Jaffer aliyesema madai ya dereva huyo kuwa kuna msongamano wa malori bandarini hapo siyo ya kweli.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a17401759faab847d7604f8751f06c5c.jpeg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi