loader
Dstv Habarileo  Mobile
Malecela, Warioba wamsifu Mwinyi kwa ujasiri

Malecela, Warioba wamsifu Mwinyi kwa ujasiri

VIONGOZI wastaafu waliofanya kazi na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wamemzungumzia kuwa ni kiongozi aliyewajibika kwa kuchukua hatua ikiwemo kujiuzulu nyadhifa mbalimbali hata kama  matatizo yaliyotokea hakuhusika nayo.

Hayo yameelezwa na viongozi hao wakielezea wanavyomfahamu Mzee Mwinyi baada ya uzinduzi wa Kitabu chake cha Mzee Rukhsa; Safari ya Maisha Yangu, mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar e Salaam.

Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wakati wa Utawala wa Rais Mstaafu Mzee Mwinyi, John Malecela alisema wakati kiongozi huyo akiwa madarakani, hali ya uchumi ilikuwa ngumu na aliingia kipindi ambacho hata fedha za kigeni nchi ilikuwa haina na kulikuwa na tabu kupata bidhaa.

“Mzee Mwinyi aliingia madarakani wakati nchi inapitia kipindi kigumu, mfano tu nchi haikuwa na fedha za kigeni za kununua bidhaa na mahitaji muhimu, ilikuwa ili kupata mahitaji lazima upange mstari,”alisema Malecela.

Alisema alikuwa ni kiongozi aliyejitahidi kuona uamuzi anaouchukua una manufaa kwa wananchi na alikuwa mtu wa kweli, mwaminifu na aliyeguswa na matatizo ya wananchi wake.

“Aliamua kujiuzulu baada ya mauaji ya Shinyanga, ulikuwa ni uamuzi mgumu sana wakati huo Mzee Mwinyi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka (1975-1977),ulikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu kile kitendo hakikufanywa na yeye, walifanya baadhi ya watu kule Shinyanga na walijulikana ila alichofanya Mwinyi ni  ule utaratibu wa demokrasia kwa waafrika kuwajibika hata kama huna hatia,”alisema.

Kuhusu mauaji hayo, Mzee Mwinyi katika Kitabu chake hicho Sura ya 11 anasema anakumbuka akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani  kati ya mwaka 1975 hadi 1977 kulitokea mauaji ya kutisha ya vikongwe katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza kwa kuhusisha na imani za kishirikina, viongozi wa juu wa wakati huo akiwemo Waziri Mkuu, Rashid Kawawa na wenzake waliitisha kikao kujadili kadhia hiyo.

Alisema iliamuliwa kuanzishwe operesheni maalumu lengo likiwa kuwakamata watuhumiwa lakini kwa bahati mbaya utekelezaji wake haukuwa nzuri kwa sababu watu wasio na hatia pia waliteswa na wengine kuuwawa.

“Sikujua hilo mpaka Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa rais wakati huo na akaunda tume ya uchunguzi, nikajihisi nina wajibu wa kujiuzulu ili kulinda heshima ya serikali na kiongozi wake, nikamwandikia barua Mwalimu, naye akaridhia,”alisema Mzee Mwinyi.

Alisema alifanya hivyo sio kwa kushinikizwa na yeyote bali aliona ana wajibu wa kuwajibika na wenzake ambao walikuwa wakuu wa mikoa hiyo nao wanajiuzulu.

Akielezea jinsi alivyomfahamu Mzee Mwinyi, Balozi Ombeni Sefue ambaye amehusika na uandishi wa kitabu hicho, alisema Mzee Mwinyi alikuwa kiongozi msikivu na amefanya naye kazi hivyo hakupata  kigugumizi alipomwambia  aandike  kitabu chake.

Balozi Sefue alisema wakati akiandika kitabu hicho cha Mzee Mwinyi, alikuwa akipata maelezo kutoka kwa mzee mwenyewe, na wakati mwingine alipata maelezo kwa watu wake wa karibu na wale waliofanya kazi pamoja akiwemo Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba , Pius Msekwa na Kingunge Ngombale Mwiru.

“Ila sehemu ya maisha yake ya utotoni nilikaa naye akanisilimua na tukarekodi kisha naenda kusikiliza nikiwa na msaidizi wangu tunaandika, tukimaliza tunazileta kwake anazisoma hatimaye kitabu kikapatikana,”alisema Balozi Sefue.

Alisema katika kitabu hicho walishauriana mambo gani ya kuandika na mengine yaachwe kwa sababu kama wangeandika yote, ingebidi wachapishe vitabu viwili.

Kwa upande wake Jaji Mstaafu  Joseph Warioba alimzungumzia Mzee Mwinyi na kusema alikuwa na uwezo wa kuwaweka watu pamoja  na aliwapa uhuru wa kuzungumza huku akisikiliza  matatizo yao na alipenda suluhu ya matatizo hayo ipatikane haraka.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7d2a0632bb0d946ce6d324b22b261b67.jpeg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi