loader
Dstv Habarileo  Mobile
SMZ yakiri mchango wa dini kukabili Ukimwi

SMZ yakiri mchango wa dini kukabili Ukimwi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema inatambua mchango unaotolewa na tasisi za dini pamoja na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya virusi vya vkimwi (VVU) na Ukimwi kwa kuwawekea wananchi mazingira wezeshi kupata elimu hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), Dk Ahmed Mohammed Khatib, alibainisha hayo katika uzinduzi wa machapisho ya uhamasishaji wanaumme na watoto kutumia huduma za VVU na Ukimwi kupitia taasisi za kidini Zanzibar.

Alisema taasisi za dini zina mchango mkubwa kwa mafanikio yaliyofikiwa katika mwitikio wa kitaifa nchini katika kupambana dhidi ya ugonjwa huo.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 0.4 ya Wazanzibari wanaishi na VVU ukilinganisha na asilimia moja kwa mwaka 2012.

Hadi kufikia Machi mwaka huu, kulikuwa na watu wanaoishi na vvu 8,147 ambao wanaopata huduma katika vituo vya huduma, kati yao wanaume 2,526 na wanawake 5,621 na 292 (asilimia nne) ni watoto chini ya miaka 14.

Alisema utafiti wa viashiria vya VVU na Ukimwi (THIS) wa Mwaka 2016/17 ulionesha kuna maeneo yenye upungufu yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa ushirikikiano wa wadau wote, zikiwemo taasisi za dini. 

Ilibainika kuwa, upungufu mwingine upo kwa wanaume na watoto kuwa nyuma katika upimaji wa VVU, uanzaji wa dawa za kufubaza virusi (ARVs) na ufuasi endelevu wa dawa hizo.

Takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonesha kuwa, asilimia 41 ya wanaume wanaoishi na VVU hawajawahi kupima VVU nchini, hivyo hawajui hali zao, lakini wanaojijua wana tatizo la kuanza dawa mapema au kutokunywa dawa, hivyo husababisha ongezeko la vifo vinavyotokana na Ukimwi na VVU.

“Miongoni mwa vifo vinavyojitokeza vingi vinahusisha wanaume kuanzia umri wa miaka 15 ambao ni 12,000 hufariki kwa mwaka ukilinganisha na wanawake, baadhi ya familia, wazazi wanaoishi na VVU hawajawapima watoto wao walio chini ya miaka 15 na kwa walezi wanaoishi na watoto wenye maambukizi ya VVU, hawajawapeleka watoto hao kuanza huduma za tiba na matunzo kwa ustawi wao,” alibainisha.

Mkurugenzi Utawala na Rasilimali Watu, Shekh Othman Mohammed Saleh kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, alisema machapisho hayo yamekuja wakati mwafaka ili kufikia lengo la serikali kumaliza Ukimwi na VVU ifikapo mwaka 2030.

Alisema tasisi za dini ambazo viongozi wake wapo karibu na wananchi katika nyumba za ibada, wanaweza kufikisha elimu hiyo.

Naye Msaidizi Meneja wa Kitengo Shirikishi Ukimwi, Homa ya Inni, Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Issa Abeid Mussa, aliomba kusimamiwa jambo hilo kwa dini zote ili kuleta matumaini mapya kwa jamii na kufikia lengo la serikali kuondoa maambukizi mapya.

Mshauri Mwandamizi wa Elimu ya Mabadiliko ya Tabia na Masuala ya Ukimwi na Kifua Kikuu katika Mradi wa USAID Tulonge Afya, Michael Luvanda, alisema machapisho hayo yameandaliwa kwa ushirikiano wa Tume ya Ukimwi ya Zanzibar, Wizara ya Afya Zanzibar, wadau watekelezaji wa mkakati wa kushirikisha viongozi wa dini, taasisi na mashirika ya kidini Zanzibar kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Taasisi wa Marekani wa Kudhibiti Ukimwi (PEPFAR) kupitia USAID ili kutumiwa na viongozi wa dini kuhamasisha na kuongeza ushiriki wa wanaume na watoto kupata huduma za Ukimwi.

Mchungaji Nuhu Sallanya kutoka Kanisa la Anglikana, alisema kila mmoja analazimika katika mapambano hayo na wasikubali kurudi nyuma hasa kwa waumme ambao wameonekana kuwa nyuma.

Machapisho yaliyoandaliwa ni pamoja na Mwongozo wenye ujumbe wa matumaini kwa ajili ya viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikristo, Kalenda ya Majilio na Hijja, Mpango wa Wiki Nne wa kila mwezi na mabango yenye ujumbe unaohamasisha upimaji wa VVU, kuanza huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU, matumizi sahihi ya dawa za ARV, kuanza na kutumia dawa kinga ya Kifua Kikuu (IPT), kupima wingi wa virusi mwilini na matibabu ya VVU kwa watoto.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f4bac13196b7c6020ca5e62bfd2492ad.jpeg

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Zanzibar

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi