loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA: Hakuna msongamano bandarini Dar

TPA: Hakuna msongamano bandarini Dar

UWEKEZAJI mkubwa unaoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam sambamba na maboresho ya teknolojia na mashine za kisasa umeongeza kiwango cha ufanisi wa bandari hiyo na kuvutia wateja waliokuwa wakitumia bandari za nchi jirani kurejea tena kuitumia.

Moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele cha kwanza ni kipengele cha Huduma kwa Wateja na wateja wengi hivi sasa wanakiri kuwa bandari hii ni lango halisi la biashara za kitaifa na kimataifa kutokana na viwango bora vya huduma zinazotolewa na usalama wa uhakika wa mizigo ya wateja.

Ufanisi huu ndiyo umeifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa bora kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na upanuzi unaoendelea ukiwemo ujenzi wa gati namba moja hadi namba saba kwa kuongeza kina kutoka mita 8.5 za awali hadi kufikia mita 14.5. Hii ni pamoja na ujenzi wa gati jipya namba 0 la kushushia magari ambalo limekamilika na linafanya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Erick Hamissi, anasema asilimia 40 ya eneo la bandari hii liko kwenye shughuli za ujenzi wa upanuzi ambao utakamilika mwezi Agosti mwaka huu na kuifaya bandari ya Dar es Salaam kuwa  na viwango vya juu kabisa vya ubora katika kuwahudumia wateja wake.

Licha ya taharuki ya hivi karibuni iliyosababishwa na dereva mmoja wa lori aliyehojiwa na chombo kimoja cha habari hapa nchini na video yake kusambaa mitandaoni akidai kuwepo kwa msongamano wa malori bandarini hapo, Hamissi anasema taarifa hizi siyo za kweli.

Baada ya kusambaa kwa video ya dereva huyo wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo ya Omar Awadh Transport, TPA iliamua kuwaita waandishi wa habari bandarini hapo ili kushuhudia utendaji kazi wa bandari kwa lengo la kuujulisha umma hali halisi ambayo ni tofauti kabisa na tuhuma zilizotolewa na dereva huyo.

Wakati waandishi wakiendelea na kazi yao bandarini hapo, ndipo ikatokea ziara ya ghafla ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika kushuhudia kama madai ya kuwepo kwa msongamano wa malori bandarini hapo ni ya kweli au la.

Akiwa njiani kuelekea bandarini hapo, Waziri Mkuu anasema alipata fursa ya kuongea na baadhi ya madereva wa malori ambao wamemweleza kufurahishwa na huduma bora zinazotolewa na Bandari ya Dar es Salaam tofauti na madai ya dereva mwenzao.

Mmoja wa madereva aliyeongea na Waziri Mkuu anasema: “Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Bandari ya Dar es Salaam na sijapata changamoto yoyote kama ilivyo kwenye bandari za nchi nyingine ambako unaweza kukaa wiki nzima, Tanzania wanahudumia vizuri na kwa haraka.”

Majaliwa pia akamuhoji dereva mwingine kuhusu taarifa ya kuwepo kwa foleni kubwa  bandarini, lakini dereva huyo akasema: “Hapana, foleni siyo kubwa, kwa kawaida naweza kuchukua saa moja au mbili kuhudumiwa na kutoka bandarini, kwa ujumla utendaji wa bandari uko vizuri na hakuna malalamiko.”

Katika video hiyo, dereva huyo alidai kukaa bandarini hapo kwa siku nne kutokana na uwezo wa bandari katika  shughuli za upakiaji na ushushaji mizigo ya wateja, hali ambayo alidai inasababisha kero na hasara kubwa kwa wateja.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, amemweleza Waziri Mkuu kwamba madai ya dereva huyo siyo ya kweli kwa kuwa nyaraka zinaonesha aliingia bandarini hapo Mei 10 mwaka huu saa nane na kuanza kushusha mzigo wake saa 10 na ilipofika saa 11 alikamilisha kazi hiyo na kuondoka bandarini.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hakuna mteja yeyote aliyekaa hapa bandarini kwa siku tatu bila kupata huduma, kampuni ambayo dereva wake ametoa malalamiko ni mteja muhimu wa TPA ambaye amepewa eneo maalumu la kufanyia kazi zake pamoja na  vitendea kazi zikiwemo ‘Forklift’ nne kwa sababu tunajua umuhimu wa mzigo wa shaba na jinsi ambavyo tunataka tujenge uhusiano mzuri  kati yetu na nchi jirani,”anasema Hamissi.

Kutokana na ukweli kuwa chagamoto za hapa na pale katika utoaji huduma bandarini zinasababishwa na mradi wa upanuzi wa bandari unaoendelea ukiwa na nia ya kuongeza ubora na ufanisi, Mkurugenzi Mkuu wa TPA amewaomba wateja na wadau wao kuwa wavumilivu kwani ujenzi huo utakamilika mwezi Agosti mwaka huu ambapo huduma zinazotolewa zitaimarika zaidi na kutolewa kwa kasi inayokidhi matarajio yao.

Baada ya kujiridhisha na kutokuwepo kwa msongamano wa malori katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka Menejimenti ya TPA kuendelea kuimarisha huduma za bandari, kufanya kazi kwa saa 24 ili hata wateja wanaoingia usiku wa manane waweze kupata huduma huku akitoa wito kwa watumishi wote wa TPA kuzungumza lugha moja ya uwajibikaji unaozingatia weledi, uaminifu na uzalendo kwa nchi yao.

“Mambo haya yatatusaidia sana kwa sababu tunatuma ujumbe mzuri ili bandari yetu iendelee kuwa bora kwenye ukanda  huu wa mashariki, tusijiweke nyuma, tusiwe wavivu, nchi kadhaa zinatutegemea sisi,” amesisitiza Majaliwa

Anaongeza: “Wakati nakuja hapa nimezungumza na madereva wa malori huko njiani, wamenieleza kushangazwa na taarifa ya dereva mwenzao kwamba hawahudumiwi kwa haraka, wameniambia wanafurahishwa na namna bandari mnavyowahudumia katika kushusha na kupakia mizigo yao, wengi wamesema haiwachukui zaidi ya saa 24 kuingia bandarini, kupata huduma na kutoka bandarini."

Waziri Mkuu pia amewahakikishia wateja wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa serikali inazifanyia kazi changamoto zote ikiwemo upanuzi wa barabara inayoanzia Daraja la Mwalimu Nyerere hadi bandarini hapo ili iwe ya njia nne badala ya njia mbili za sasa.

Mkuu wa Operesheni wa Kampuni ya Usafirishaji Mizigo ya Omar Awadh Transport inayosafirisha shaba kutoka Zambia hadi bandarini hapo, Amer Ali Saleh, anasema tayari wamemtaka dereva wao aliyehusika na video hiyo kufika ofisini na kujieleza.

“Hatujaonana na dereva huyo, tumeshamwita aje ofisini ajieleze kwa nini ameongea maneno yale ya kupotosha umma, tunamtaka aje ili tujue changamoto zake tumsaidie,” anasema Saleh.

Mkuu wa Operesheni wa Kampuni ya Reload Logistics Tanzania, Frank Mwilongo anasema magari yao hupakuliwa ndani ya saa 24 yanapoingia bandarini hapo.

Kauli hii inaungwa mkono na Mkuu wa Idara ya Usafirishaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Abdulkarim Jaffer anayesema  kuwa madai ya dereva huyo kuwa kuna msongamano wa malori bandarini hapo siyo ya kweli.

Katika azma ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya viwango vya juu katika kutoa huduma bora, TPA inasema hadi kufikia sasa, Mkandarasi anayehusika na upanuzi wa bandari hiyo ameshakamilisha ujenzi wa gati la kushushia magari pamoja na gati namba 1-5 pamoja na eneo la kuegesha magari ambapo maeneo haya yote yanatumika.

Pia mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa kuimarisha na kuongeza kina cha gati namba sita na namba saba pamoja na sehemu ya eneo la kuegesha makasha ambapo mpaka sasa gati namba sita limekamilika kwa asilimia 96 na gati namba saba limekamilika kwa asilimia 70 na yadi ya kuhudumia makasha imekamilika kwa asilimia 10 huku ujezi ukiendelea kwa kasi kubwa.

Makala hii imetayarishwa na Ofisi ya Habari na Uhusiano, TPA Makao Makuu.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi